Makala

Chimbuko la utamaduni wa silaha haramu uliogeuka janga kwa wakazi

May 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA OSCAR KAKAI

UJIO wa bunduki haramu katika Kaunti ya Pokot unakisiwa kuanza zaidi ya miaka 60 iliyopita.

Awali wakazi wa eneo hilo walikuwa wakitumia mikuki na ngao kushambulia wapinzani wao ambao walikuwa wakiwavamia na mikuki zenye sumu.

Hata hivyo, baada ya uhuru, jamii za Pokot na Karamojong zilihusika kwenye mila za kuibiana mifugo na ujangili.

Mwaka wa 1967, wafugaji walianza kununua bunduki zao za kwanza ambazo zilikuwa zimezeeka, nzito aina ya Lee-Enfield ambazo zilitumika kwenye Vita vya Pili vya Dunia na bei yake ilikuwa juu. Zilikuwa zinauzwa moja kwa ng’ombe 60. Kufikia mwaka wa 1986, bei ya bunduki ilikuwa imefika ng’ombe 15 na zilikuwa nzito kuliko aina ya AK-47.

Hata hivyo, silaha hizo ambazo walikuwa wamepata miaka ya 1960 ziliachwa miaka ya 1970 na kuchukua AK-47. Nchi za Uhabeshi na Somalia zilikuwa kwenye vita kutumia silaha za Kalashnikov hivyo nazo zikaingia Kenya. Silaha zingine aina ya  AK-47 zilinununuliwa kutoka nchi jirani ya Sudan ambapo kulikuwa na vita pia.

Kuchukua silaha haramu kulikuwa kwa lengo la kulinda utamaduni wao lakini sasa imegeuka kuwa kero kwao.

Kulingana na aliyekuwa chifu mkuu wa zamani eneo la Pokot ambaye sasa ni mwenyekiti wa baraza la jamii ya Pokot, Mzee John Muok, Wapokot walianza kununua silaha haramu kutoka Uganda wakati wa uongozi wa Jenerali Idi Amin Dada ambaye alikuwa amepindua Rais wa wakati huo Milton Obote.

“Walikuwa wananunua bunduki moja kwa ng’ombe 25,” anasema Mzee Muok.

Alisisitiza kuwa kuwa idadi kubwa ya silaha ilitoka Uganda ambapo kiongozi wa kiimla Idi Amin aliufungua njia ya silaha haramu kwa wakazi.

Bw Muok anasema kuwa mnamo Aprili 1979, wamorani kutoka jamii ya Karamojong walivamia kambi ya jeshi ya Moroto na kunyakua bunduki ambazo ziliuziwa jamii ya Pokot huku jamii ya Turkana ikianza kununua silaha kutoka Uhabeshi.

Hii ilichangia silaha haramu kusambaa kote nchini kutoka Uganda na kuacha shida kubwa eneo la Kaskazini mwa Bonde la ufa suala ambalo limekuwa gumu kwa serikali zote kutatua.

Inakadiriwa kuwa, kambi hiyo ya jeshi ilikuwa na bunduki 15,000 na risasi milioni 2 za Wasovieti kabla ya kiongozi wa kiimla wa Uganda kubanduliwa mamlakani.

Mtawala huyo wa zamani anasema kuwa nchi ya Uhabeshi ilikuwa makao ya silaha baada ya vita vya Ogaden.

“Wanabiasharia wa Somalia walipata biashahra za kuvuma. Bei ya bunduki ilirudi chini baada ya kuondolewa kwa Idi Amin,” anasema Bw Muok.

Mzee Muok anasema kuwa serikali inafaa kuwaponyoka silaha haramu wakazi wote katika jamii hasimu ambao wanazimiliki.

“Jamii za Pokot na Turkana zina silaha haramu na kupokonya jamii moja pekee ni hatari. Silaha ndio shida yetu kubwa inayotukumba,” anasema.

“Haina maana kuondoa silaha ilihali mipaka ziko wazi, bunduki zaidi zinaendelea kuingia nchini,” anasema.

Anasema kuwa matumizi ya bunduki na raia ndio serikali inafaa kuangamiza kabisa katika eneo hilo.

Siku za hivi sasa, bunduki haramu zimekuwa na athari mbaya kwa uchumi, kijamii, kitamaduni na kisiasa eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Watu wengi wamepoteza maisha, mali kuharibiwa na wakazi kupoteza makazi.

Kuongezea, kumekuwa na raslimali finyu huku maeneo ya Pokot na Turkana yakitengwa kisiasa kuhusu masuala kama elimu, barabara, na afya.