Makala

CHOCHEO: Kuwa singo ni raha tele!

June 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

JITEGEMEE uwe na maisha ya raha kuliko kuolewa na usononeke, baadhi ya wanawake utawasikia wakisema hivi.

Usijute kwa kuamua kuwa huru, singo au kukosa watoto.

Wataalamu sasa wanasema wamegundua kwamba wanawake wanaojitegemea au kuchagua kuishi bila kuolewa huwa na furaha maishani na wanaishi maisha marefu. Wanasisitiza kwamba hii ni kwa wale wanawake wanajionea fahari kuitwa mwanamke.

Kulingana na Profesa Paul Dolan, mtaalamu wa masuala ya hulka za binadamu katika chuo cha London School of Economics, wanawake wanaoamua kutoolewa na kujitegemea ndio wenye furaha maishani na wanaishi maisha ya raha kuliko wale walio katika ndoa na walio na watoto.

Mtaalamu huyo anasema japo wengi huwa wanaamini maisha ya ndoa yana raha, furaha yao huwa wakiwa na wachumba wao na uhusiano wao ukiwa mwema.

“Watu walio katika ndoa ndio wenye furaha kuliko watu wengine lakini raha huwa ni wakati ambao wachumba wao wako pamoja nao. Wakiwa peke yao maisha huwa ni giza tele,” Profesa Dolan alisema kwenye makala yaliyochapishwa mtandaoni.

Ingawa watu wengi wanaamini furaha maishani hupatikana kwa kuolewa na kupata watoto hasa wanawake, Prof. Dolan anasema kwamba ni wanawake husononeka sana wakiwa na watoto na wasipokuwa nao huhisi hawana mzigo unaoweza kuwakosesha furaha maishani.

“Tuko na ripoti za utafiti tuliofanya kwa miaka mingi na ninaweza kusema kuwa ikiwa wewe ni mwanamume na unatafuta furaha maishani, oa lakini ikiwa wewe ni mwanamke, ninasema usiolewe au kusumbuka ukitafuta mume na utakuwa na furaha na maisha marefu,” asema Dolan.

Maisha ya raha

Utafiti uliofanywa Amerika mwaka 2018 unaofahamika kama American Time Use Survey (ATUS), ulionyesha kuwa wanawake singo wanaishi maisha ya raha, uhuru na mepesi kuliko walio katika ndoa, waliopata talaka, waliotengana na wachumba wao na wajane.

Kulingana na Elyakim Kislev mwandishi wa kitabu kinachofahamika kama Happy Singlehood: The Rising Acceptance and Celebration of Solo Living, kuna manufaa mengi ya mwanamke kuwa singo ikiwa ni pamoja na kuepuka presha za ndoa.

Lakini Dkt Susan Kamotho wa shirika la Maisha Mema jijini Nairobi, anasema kuwa inategemea na maisha ambayo mtu anachagua ikiwa ni pamoja na kuchagua mchumba. “Mwanamke akichagua mume kwa kuzingatia mambo ya kumpa raha kwa muda mfupi kama vile mali pekee, kwake ndoa itakuwa jahanamu. Ukichagua mume ukizingatia tabia nzuri na uchangie kujenga ndoa yako, basi ni vigumu kujuta,” asema Dkt Kamotho.

Kulingana na mwanasaikolojia Bella dePaulo wa Muungano wa Wanasaikolojia wa Amerika, watu singo wana maisha mazuri na ukuaji thabiti wa kisaikolojia kuliko watu walio katika ndoa.

Kwenye makala yaliyochapishwa katika gazeti la the Guardian, Bella anasema wanawake wanaoishi bila kuolewa wana uhusiano thabiti na marafiki na familia zao ilhali wale walio katika ndoa hutumia muda wao mwingi na wachumba wao na watoto.

Mtaalamu huyo anasema wanawake singo wanaojitegemea hawapati matatizo ya kisaikolojia yanayoweza kufupisha maisha yao.

“Hii ni tofauti kwa wanawake wanaojitegemea kifedha lakini wako katika ndoa. Huwa wanasumbuliwa na mfadhaiko na kukosa furaha,” aeleza.

Dolan anasema kinachowafanya wanawake singo na wasio na watoto kukosa furaha ni bezo za watu. “Wanawake wengi wakifikisha umri wa miaka 40 bila kupata watoto huwa wanabezwa. Hata hivyo, ni bora kukosa kuolewa kuliko kuolewa na mwanamume atakayekukosesha furaha maishani na kukuachia watoto usumbuke ukiwatunza,” aeleza.

Anasema wanawake wengi huwa wanakufa mapema kwa kukosa furaha hata baada ya kuolewa na wanaume walio na mali nyingi.