• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 1:22 PM
CHOCHEO: Mke ana haki kunyima mumewe unyumba?

CHOCHEO: Mke ana haki kunyima mumewe unyumba?

Na BENSON MATHEKA

WANAUME wengi hufikiria kuwa wake au wapenzi wao wanaowanyima tendo la ndoa huwa na mipango ya kando.

Hii imekuwa ikisababisha migogoro katika familia na kusababisha hasara na hata mauti.

Hata hivyo wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema kuna sababu nyingi zinazoweza kufanya mwanamke kumnyima mtu wake tendo la ndoa. Wanasema sio lazima mtu awe na hamu ya kushiriki uroda kila wakati mpenzi wake anapotamani.

“Wakati mwingine unagundua kuwa ni mwanamume anayefanya mke au mpenzi wake kumkausha chumbani. Hii inaweza kuwa kwa kutomridhisha wakati wa shughuli au kwà kutomuandaa mtu wake kwa tendo lenyewe,” asema Ivy Nyawira, mwanasaikolojia wa kituo cha Maisha Mema, jijini Nairobi.

“Hakuna kitu ambacho wanawake huchukia kama mwanamume kuamsha hanjamu zake na kushindwa kuzizima. Hii inaweza kumfanya mwanamke kukataa kabisa kumpa uroda. Kwa kifupi ni ujuzi wa mwanamume chumbani unaomfanya mwanamke kuchangamkia tendo la ndoa,” asema Bi Nyawira.

Wataalamu wanasema mwanamke akianza kusingizia uchovu ili kukwepa tendo la ndoa, ni ishara kwamba mtu wake huwa anajikwaa wakati wa shughuli.

“Sio kwamba wanawake huwa hawachoki kutokana na shughuli za kila siku. Lakini uchovu ukiwa ndio sababu ya kutompa mumewe haki yake ya ndoa kila wakati, basi kuna zaidi ya hali hiyo,” asema Nyawira.

Wanasaikolojia wanasema wanaume wengi wamekuwa wakipatwa na mfadhaiko baada ya wachumba wao kuwakausha chumbani wakishuku wana mipango ya kando.

“Kinachomjia mwanamume akilini mkewe anapoanza kumnyima tendo la ndoa ni kuwa anahanya. Kuna baadhi ya wanaume wanaofadhaishwa sana na hali hii mpaka wanashindwa kutekeleza majukumu mengine hasa wale wasiopenda kusaliti wapenzi wao. Kuna mabarobaro ambao huwa wamewekeza mno muda na mali kwa wachumba wao na wanapoanza kulegea katika uroda, huchukua hatua zinazosababisha maafa,” aeleza Nyawira.

Anasema baadhi ya wanaume huwa hawaweki mazingira yanayofaa kwa tendo la ndoa kama vile kudumisha hali ya juu ya usafi. “Mwanamume anayejibwaga kitandani akinuka shombo kutokana na jasho, kinywa kutoa uvundo kwa kutopiga mswaki na harufu ya pombe au sigara, hawezi kutarajia mkewe achangamkie tendo la ndoa. Uvundo unaweza kumfukuza mwanamke kutoka kitanda cha ndoa,” asema.

Kulingana na Dkt Simon Tuju mwanasaikolojia wa shirika la Love Care, jijini Nairobi, wanaume wanafaa kujipeleleza kwanza kabla ya kulaumu wachumba wao kwa kuwanyima tendo la ndoa.

“Kuna maandalizi ya kisaikolojia yanayohitajika kumfanya mwanamke kuchangamkia tendo la ndoa na sio tu kuamini kuwa ni haki ambayo wanandoa wanapaswa kutimiziana. Kila mtu anavyolitekeleza, mazingira na uhusiano wa wachumba huwa muhimu sana,” asema Dkt Tuju.

Anasema ingawa kukausha mwanamume kwa uroda kunaweza kumsababishia mfadhaiko hasa kwa wanandoa na mabarobaro wanaowekeza kwa wachumba wao wakilenga kuchovya asali, kuna haja ya kufanya mazungumzo ya wazi kwa nia njema na katika mazingira yanayofaa ili kuboresha tendo la ndoa.

“Daima dawa ya kuimarisha shughuli chumbani na uhusiano kwa jumla ni kupitia mawasiliano ya wazi. Tafuteni mazingira mazuri na kila mmoja afungue moyo wake kwa nia njema na kwa kufanya hivi suluhisho litapatikana,” asema.

Makosa wanayofanya wengi ni kuwekeana masharti. “Ikiwa utamwekea mume au mchumba wako masharti, basi yawe ni ya kuimarisha uhusiano wenu chumbani kama vile kumtaka apige mswaki au kuacha kuvuta sigara lakini isiwe ni kuhusu unyumba,” aeleza Nyawira.

Wataalamu wanasema ikiwa mwanamume anajikwaa wakati wa shughuli, mwanamke anaweza kumweleza kuwa haridhishwi na nderemo zake kisha wajadili jinsi ya kurekebisha hali ikiwa pia ni pamoja na kutafuta ushauri kutoka kwa wataalamu wa masuala ya ndoa au madaktari.

You can share this post!

FUNGUKA: ‘Nawavizia kuku wageni kazini’

SoNy katika hatari ya kuondolewa KPL isipocheza leo Jumamosi

adminleo