CHOCHEO: Uhusiano unaozaa ndoa bora huanza kwa urafiki
Na BENSON MATHEKA
DEBORAH anajuta kwa kukataa kuolewa na Sammy ambaye ni rafiki yake wa miaka mingi.
Mwanadada huyo anasema sio kwamba hakuwa akimpenda Sammy lakini alimkataa kwa sababu hakutimiza vigezo ambavyo alitaka kwa mume.
Alimchagua Deno kwa sababu alikuwa na mali na alipenda kusafiri kwenda kujivinjari katika maeneo ya burudani tofauti na Sammy ambaye hutumia muda mwingi akiwa kazini.
“Makosa niliyofanya ni kufikiri pesa za Deno na hulka yake vingenihakikishia furaha katika ndoa. Baada ya miaka minne, niligundua nilikosea nikaanza kujuta kwa kumkataa Sammy ambaye sasa ninaamini angekuwa mume mzuri hata kama hana mali nyingi,” asema Deborah, kauli ambayo Silvia Wariara, mwanasaikolojia katika kituo cha Maisha Mema, jijini Nairobi anakubaliana nayo.
“Ukitaka maisha mazuri ya ndoa, oa au olewa na rafiki yako wa dhati. Mtu akikosa kuwa na urafiki na mchumba wake, maisha ya ndoa huwa jinamizi,” asema Wariara.
Deborah anasema hakuweza kuelewana na Deno na walikuwa wakiishi ulimwengu tofauti ndani ya nyumba moja hadi akaamua yametosha na kuomba talaka.
“Ilikuwa jehanamu,” asema.
Wataalamu wa masuala ya ndoa wanasema kwamba kinachofanya ndoa iliyojikita katika misingi ya urafiki wa dhati kunawiri ni kwa sababu wachumba huwa wanaaminiana.
“Wanandoa wanafaa kuaminiana na hii inawezekana tu kwa marafiki. Uaminifu ukikosa, na hauwezi kununuliwa kwa mali, sura au umbo, ndoa inakuwa balaa,” asema Wariara.
Anasema kwamba umuhimu wa urafiki katika ndoa ni kuwa kila mchumba anamjali, kumwelewa na kumheshimu mwenzake.
“Mtu anapopata shida, huwa anampigia simu rafiki yake kwanza. Kwa marafiki, hakuna siri na hii ni moja ya vigezo muhimu vya ndoa yenye furaha. Kufichana mambo kumetambuliwa kama sumu katika ndoa. Rafiki wa dhati hatakuficha chochote,” asema Peter Simbi, mshauri wa wanandoa katika kanisa la Life Center, jijini Nairobi.
Simbi anasema kuwa raha ya marafiki wanaooana huchangiwa na wepesi wa mawasiliano kati yao.
“Ukosefu wa mawasiliano umetambuliwa kuwa sumu ya ndoa. Rafiki ni mtu unayefurahi kuwa karibu naye bila masharti. Mnayefaana wakati wa raha na wakati wa dhiki. Ukioa au kuolewa na mtu kama huyo na muendelee kupalilia urafiki wenu, utatoboa katika ndoa,” aeleza Simbi.
Uchu
Anasema inasononesha kuishi katika ndoa na mtu anayekuchangamkia wakati wa uroda pekee. “Ulaji uroda sio dhihirisho la urafiki. Kuna tofauti ya uchu na urafiki. Watu wengi huwa wanaolewa kwa sababu ya uchu, yaani tamaa ya kimwili na kisha kujipata wakiishi kwa dhiki,” asema.
Wariara anakubaliana na kauli hii akisema kinachofanya ndoa kati ya marafiki kushamiri ni kwa sababu huwa na tabia sawa na wanachangamkia vitu vinavyofanana.
“Marafiki huwa wanafunguliana roho, jambo ambalo ni muhimu sana katika ndoa. Kuwa na hulka zinazofanana kunarahisisha maamuzi ya mambo,” aeleza.
Wanasaikolojia wanasema kwamba kwa sababu ya kufahaminiana, kuaminiana na kuelewana, huwa ni vigumu kwa marafiki kukosana wakioana.
“Oa au olewa na rafiki yako. Ukishindwa kupalilia urafiki kati yako na mpenzi wako, usipige hatua ya kuoelewa. Utajipata katika balaa,” asema Isabel Kakui, mshauri wa shirika la Abudant Love Care, jijini Nairobi.
Anasema ni rahisi kubaini ikiwa mtu ni rafiki yako kwa kuwa marafiki huzungumza lugha moja.
“Ikiwa lugha ya mpenzi wako ina kuudhi, ni ya ukali na hakuelewi au analazimisha mambo kumfaa badala ya kuwafaa nyinyi wawili, basi epuka ndoa,” asema.
Kakui anasema rafiki hufanya mtu acheke na sio kulia, kuchangamka na sio kununa. “Hata kama watu wengine hawakuchamgamkii, ukiwa na rafiki mnaweza kucheka na kutaniana. Olewa na mtu kama huyo,” asema.
Wataalamu wanasema kwamba hata wakigombana, marafiki huwa wanazika tofauti zao, kutafuta suluhu na kusameheana.
“Kinachofanya ndoa kati ya marafiki kuwa ya kipekee ni kwa sababu wanasaidiana kwa hali na mali. Hii ndio hufanya ndoa kushamiri kwa kuwa wanaweza kupanga na kutekeleza mambo yao pamoja,” asema Wariara.