Makala

CJ Koome alivyozima maandamano ya mawakili

March 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

CHAMA cha Mawakili Kenya (LSK) kimefutilia mbali maandamano ambayo kilikuwa kimepanga kufanya leo, Jumatatu, Machi 3, 2024 baada ya Jaji Mkuu (CJ) Martha Koome kusimamisha utekelezaji wa mpango waliolalamikia.

Mawakili walipanga kuandamana kulalamikia mpango wa Idara ya Mahakama kuzindua vituo vya usajili katika Vituo vya Huduma kote nchini.

Hatua hiyo ilikuwa imezua mvutano mkubwa baina ya Idara hiyo na mawakili.

Hata hivyo, Jaji Mkuu Martha Koome alisimamisha utekelezaji wa mpango huo, kufuatia mkutano uliopangiwa kufanyika Alhamisi wiki hii baina ya idara hiyo na uongozi wa LSK.

Kwenye taarifa, LSK ilisema idara hiyo imekubali mazungumzo kuhusiana na suala hilo tata, na wanachama wake wameamua kutoa nafasi kwa mashauriano hayo kufanyika.

Kwenye mpango huo, Idara ya Mahakama ilikuwa imepanga kubuni vituo vya usajili katika Vituo vya Huduma kote nchini, huku vituo vya kwanza vikipangiwa kuzinduliwa jijini Nairobi na mjini Thika.

Baadaye, vituo hivyo vingezinduliwa kote nchini.

Kwenye mpango huo, idara hiyo ilikuwa imesema lengo lake kuu ni kuhakikisha imewarahisishia Wakenya utaratibu wa kupata haki kupitia teknolojia.

Ilisema ilikuwa ikitumia vituo vya Huduma, kutokana na mafanikio makubwa ambayo vimepata tangu kuanzishwa kwake.

Hata hivyo, mawakili walipinga vikali hatua hiyo, kupitia kiongozi anayeondoka wa LSK, Bw Eric Theuri. Walisema kuwa kuna uwezekano mpango huo ukaingiliwa na wadukuzi wa mitandao.

Pia, walizua swali kuhusu utenganisho wa kimajukumu baina ya Afisi ya Rais na Idara ya Mahakama. Walisema majukumu baina ya matawi hayo mawili ya serikali yanafaa kutoingiliana.

Vituo vya Huduma vinasimamiwa na Wizara ya Utumishi wa Umma, iliyo chini ya Afisi ya Rais.

Bw Theuri alisema uamuzi huo uliharakishwa, akieleza kwamba kulikuwa na uwezekano wa kuingiliwa na watu walaghai, ambao wangeipaka tope idara hiyo.

Alisema wanachama wake kote nchini walihofia kulikuwa na hatari kubwa mpango huo ungeongeza visa vya ukiukaji wa kimaadili. Aliomba utekelezaji wake usimamishwe kwa muda hadi pale kutakuwa na mashauriano ya kutosha.

Matokeo ya mvutano baina ya taasisi hizo mbili yalikuwa ni kesi kadhaa kuwasilishwa mahakamani. Kwenye kesi yake, LSK iliitaka mahakama kusimamisha utekelezaji wa mpango huo kwa muda.

Kwenye kikao cha kujadili suala hilo, kilichoongozwa na Jaji Kimondo, LSK iliirai mahakama kusimamisha utekelezaji wa mpango huo hadi pale masuala tata yatakapojadiliwa na muafaka ufaao kupatikana.

Jaji Kanyi alisema Idara ya Mahakama ilikuwa imebuni makubaliano na Wizara ya Utumishi wa Umma na Idara ya Utumishi wa Umma kuhusu utekelezaji wa mpango huo.