• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Clarence Mwangi: Kutoka shamba boi hadi mmiliki wa kampuni

Clarence Mwangi: Kutoka shamba boi hadi mmiliki wa kampuni

Na SAMMY WAWERU

AKIVUTA mawazo yake nyuma, anaona  maisha yaliyojawa na pandashuka chungu nzima kufuatia milima na mabonde aliyopitia.

Hata hivyo, Mungu si Athumani, siku yako ya kujaliwa mema ikitimia hakuna atakayezuia baraka zako kukufikia.

Bw Clarence Mwangi kwa wakati mmoja alikuwa shamba boi, na kwa sasa anamiliki kampuni ya kurembesha vikombe, kuvitia nembo, na majina.

Endapo una shule, chuo, kampuni, kanisa, duka la kijumla, na ungetaka vikombe viandikwe kulingana na majina ya taasisi yako, majukumu hayo Bw Mwangi anayaelewa barabara.

Yeye ndiye mwanzilishi na mmiliki wa kampuni ya Glatex Images iliyoko jijini Nairobi na tawi jingine Ruiru, kaunti ya Kiambu.

Anakumbuka kana kwamba ilikuwa jana 2009 alipohitimu kwa Shahada ya Maswala ya Biashara katika Chuo Kikuu cha Kimathi kilichoko Nyeri, kazi ya kwanza aliyopata ilikuwa ya kulima shamba yaani shamba boi.

“Licha ya kuwa na shahada, niliajiriwa kazi ya shamba na mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) jijini Nairobi,” afichua Bw Mwangi.

Kibarua cha kulima shamba

Mchagua jembe si mkulima, Mwangi alifanya kazi hiyo pasi kujali kiwango chake cha masomo au elimu.

Anasimulia kuwa alikuwa akilipwa Sh200 kwa siku, hesabu hiyo ikikokotolewa mshahara aliopokea ulikuwa Sh6, 000 kwa mwezi.

Hata hivyo, anaeleza kwamba mhadhiri huyo alikuwa mkwasi wa utu na aliyemshika mkono kama mzazi kwani alikuwa akimtia motisha kuwa juhudi zake zisingeambulia patupu.

“Nilifanya kazi kwa bidii nikiwa mwingi wa matumaini nyota yangu ya jaha siku moja itaangaza,” aema mjasirimali huyu.

Miaka miwili baadaye mwaka 2011, kwa mtaji wa Sh2, 000 pesa alizokuwa ameweka kama akiba Bw Mwangi alianzisha biashara ya kutia nembo na majina kwenye mavazi hasa tishati kwa kutumia mashine ya kujitengenezea inayojulikana kama Skrini.

Safari ya kuimarisha biashara hiyo haikuwa rahisi, na kulingana naye ni kwamba alikuwa akisafiri masafa marefu akitafuta shule, makanisa na hata makampuni auze kufanya oda.

“Baadhi ya shule na kampuni nilizozuru nisingeruhusiwa kuingia na walinzi wao. Hata hivyo, sikufa moyo,” asimulia baadhi ya masaibu aliyokumbana nayo.

Atafutaye hachoki na akichoka keshapata, kijana huyo anaendelea kueleza kwamba alijikaza kisabuni kusukuma gurudumu la maisha na kazi yake ya kutia nembo na majina kwenye mavazi ilishika kasi kiasi cha kuanza kupokea oda tele.

Jitihada kunoga

Anasema kwamba taasisi mbalimbali za elimu na kampuni, wote walitambua kazi yake ilikuwa shwari na kumtegemea awachapishie majina na nembo kwenye majezi na hata mavazi yao maalum.

Akiwa katika harakati za kuhudumia wateja wake, baadhi yao walimpa mawaidha ya kuboresha kazi yake ambapo walimsihi ajifunze kuandika majina na kutia nembo kwenye vikombe.

Alitumia mashine hiyo hiyo ya Skrini aliyokuwa akitumia kwa mavazi, kujaribu wazo la vikombe.

“Biashara iliimarika, kando na mavazi nikawa nikiwarembeshea vikombe kwa nembo za shule na kampuni zao,” adokeza Bw Mwangi.

Nyota yake ya jaha ilitua 2016 aliponunua mashine ya kisasa inayojulikana kama ‘Large Format Printer’ na iliyomgharimu kima cha Sh1.2 milioni.

Aidha, mashine hiyo ndiyo huitumia kuandika majina na kutia nembo kwenye vikombe.

Hali kadhalika, 2017 alinunua mashine kadhaa za kuchapisha vibango, na kutia nembo mavazini.

Anachojivunia zaidi mfanyabiashara huyu ni kuwa miongoni mwa waliobuni nafasi za kazi, kwani kufikia sasa ameajiri zaidi ya vijana 20.

Wakati wa mahojiano na Taifa Leo alisema lengo lake ni kuhakikisha kampuni ya Glatex Images imepata matawi mengine katika karibu kila pembe ya nchi ili kuwapa nafasi za kazi vijana waliofuzu vyuoni na katika taasisi za juu za elimu lakini hawana mahala pa kuzimbulia riziki.

You can share this post!

MOTO SANA: Arsenal moto kwa Valencia, yatinga fainali ligi...

MWANAMUME KAMILI: Ukware wa wanaume wa leo umechangia aibu...

adminleo