Makala

CORONA:  Hali si hali baadhi ya wakazi wa mijini wakihamia nyumba za kodi nafuu

July 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

HUKU watafiti wataalamu wa masuala ya matibabu, Wanasayansi na madaktari ulimwenguni wakipambana usiku na mchana kutafuta chanjo na tiba ya Covid-19 ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona, visa vya maambukizi nchini Kenya vimepita 7,000

Kisa cha kwanza hapa nchini kiliripotiwa mnamo Machi 13, 2020, na sawa na mataifa mengine, Kenya inazidi kuhisi athari za ugonjwa huo.

Sekta mbalimbali zimeathirika kwa kiasi kikuu, baadhi ya biashara zikifungwa na maelfu ya watu kupoteza ajira.

Kimsingi, uchumi unazidi kuzorota kufuatia athari za corona, homa ambayo sasa ni janga la kimataifa.

Kaunti ya Nairobi na ambayo inaongoza kwa visa vya maambukizi, wakazi hasa wanaoishi mitaa ya mabanda na vilevile ya kadri wenye mapato ya chini wameendelea kulemewa na kodi ya nyumba.

Mwishoni mwa mwezi Juni 2020 na mwanzoni mwa mwezi huu wa Julai, katika nyingi ya ploti baadhi ya wapangaji wameonekana wakihama.

Mfano, katika eneo la Carwash Thika Road, Kasarani, mkazi anayejitambulisha kama Peter kwenye mahojiano na Taifa Leo, amesema Mei 2020 pamoja na wafanyakazi wenza, walisimamishwa kazi jambo ambalo limechangia maisha kuwa magumu.

“Kwa sasa sina chanzo kingine cha mapato, nyumba niliyokuwa nikiishi ya Sh7,000 kwa mwezi nimelazimika kuihama Julai ili kukodi nitakayomudu. Covid-19 imeniathiri kwa kiasi kikuu,” Peter akasema.

Mkazi huyo ambaye pia ni baba wa mtoto mmoja anasema kwa sasa anategemea vibarua vya hapa na pale, ikiwamo ujenzi, kukithi familia yake riziki na pia kujiendeleza kimaisha.

“Licha ya kujieleza kwa landilodi, alisema naye pia ana majukumu hivyo basi sikuwa na budi ila kuhama,” mkazi huyo akasema.

Kilio chake kinawiana na cha Samuel Waithaka, anayeshangaa atakavyolipa kodi ya mwezi huu wa Julai.

“Mimi ni DJ, na nilikuwa nikitumbuiza katika hafla mbalimbali kujipa kipato. Makongamano yalipigwa marufuku kwa muda usiojulikana, kazi ikasimama,” Bw Waithaka ambaye pia ni baba wa mtoto mmoja akalalamika.

Kulingana na Daisy Wanjiru, ambaye ni fundi wa kochi, biashara zinaendelea kudorora na hali ikiendelea inavyoshuhudiwa huenda karakana aliyoajiriwa ikafungwa.

“Mshahara tunalipwa kwa awamu na baada ya fanicha tunazounda kununuliwa. Mapato tunayopokea ni ya kula pekee, wateja wamepungua kwa kiasi kikuu,” Daisy akaeleza katika mahojiano.

Wakazi hasa waliopoteza nafasi za ajira, wanaendelea kuhangaika licha ya serikali Juni 2020 kuzindua mpango wa ‘Kazi Mtaani’, ambao kulingana na serikali unalenga kusaidia wanaoishi mitaa ya mabanda kujiendeleza kimaisha wakati huu virusi vya corona vinatesa.

Kuhusu suala la nyumba za kukodi, Rais Uhuru Kenyatta alisema hana mamlaka kisheria kushinikiza malandilodi kupunguza kodi au kuifuta kwa muda hadi Covid-19 itakapodhibitiwa.

Kiongozi wa nchi alisema hayo miezi kadhaa iliyopita katika mahojiano na vituo vya redio vinavyopeperusha matangazo kwa lugha ya Kiswahili, huku akihimiza wamiliki wa nyumba za kukodi kuwa na utu na ubinadamu kipindi hiki kigumu.

Kuna malandilodi wachache waliojitokeza kueleza kuondolea wapangaji wao kodi kwa muda, na wengine kuipunguza.

Aidha, kilio cha wakazi kinajiri huku Rais Kenyatta wiki ijayo akisubiriwa kuona iwapo atalegeza kamba zaidi sheria na mikakati iliyowekwa kuzuia msambao wa corona na pia kufungua uchumi.