CORONA: Ukaidi wa Wakenya unavyolemaza juhudi za kupunguza maambukizi
Na GEOFFREY ANENE
Serikali ina kibarua kigumu kushinda vita dhidi ya maambukizi ya virusi hatari vya corona, ambavyo vimefika visa 81 nchini Kenya na 912, 565 duniani tangu mkurupuko uanze mjini Wuhan nchini Uchina mapema mwaka huu.
Kafyu, kupunguza idadi ya abiria katika vyombo vya usafiri kama magari na treni, kutosalimiana kwa mikono, kutopiga pambaja, kunawa kwa kutumia jeli maalumu (sanitizer) na kupiga marufuku mikusanyiko mikubwa ni baadhi ya mbinu serikali inatumia kuzuia uenezaji wa virusi hivyo.
Hata hivyo, katika uchunguzi, mwandishi huyu aligundua kuwa serikali italazimika kufanya kazi ya ziada katika vita dhidi ya virusi hivyo.
Ikikaribia wiki moja tangu serikali itangaze amri ya kutotoka nje kwa nyumba kutoka saa moja usiku hadi saa kumi na moja asubuhi, Wakenya wamekuwa wakisumbua maafisa wa usalama katika kutekeleza amri hizo.
Mnamo Jumatano, maafisa wa polisi walilazimika kurusha kitoamachozi katika baa moja mtaani Kariobangi South Civil Servants baada ya kugundua wanywaji ‘werevu’ walijifungia mle.
Mita 100 hivi kutoka baa hiyo, watu pia walijifungia kwenye baa moja karibu na barabara ya Mutarakwa kabla ya askari kugundua watu walikuwa mle baada ya mmoja waliokuwa wakibugia pombe kukohoa.
Katika steji ya mwisho ya matatu zinazohudumu katika barabara ya Kariobangi South Civil Servants hadi mjini Nairobi, matatu moja ya nambari 36 zinazohudumu barabara ya Dandora hadi City Stadium ilionekana ikiwa imebeba dereva na watu wengine watatu kando yake katika chumba cha dereva badala ya dereva na mtu mmoja.
Magari haya pia yanasemekana yanavunja sheria za kubeba abiria wachache, hasa saa ya mwisho kabla ya kafyu kuanza. Yanajaza abiria hadi wengine wanasimama baada ya kukosa viti vya kukalia.
Alipopanda basi moja kutoka barabara ya Ronald Ngala mjini Nairobi, ambalo linapitia barabara ya Juja Road hadi mtaani Dandora, ambayo barabara inaotumiwa na matatu ya nambari 32, mwandishi huyu alijionea mambo.
Katika basi hilo, kiti anachofaa kukalia utingo kilikuwa na abiria wawili naye utingo pamoja na abiria wengine wawili walikuwa wamejificha nyuma ya mlango uliofungwa.
Baada tu ya basi kutoka mjini, bila ya abiria yeyote kushuka, utingo alielekeza dereva asimamishe basi kwenye stegi ya karibu na kituo cha kujazia mafuta cha Amana kubeba abiria mmoja.
Cha kushangaza hakuna abiria alishuka hadi stegi ya Wamwaris alikoshuka mwandishi huyu. Hata hivyo, basi hilo liliongeza abiria wawili katika steji hiyo, ambayo si ya mwisho.
Aidha, kwenye steji nyingi tu, wahudumu wa magari ya abiria, ambao hawakuwa na magari walionekana wakiwa katika vikundi vikubwa kama kwamba hawafahamu amri ya kutofanya mikusanyiko mikubwa.
Inasemekana kuna watu ambao bado wanaenda katika sehemu za kuabudu kisirisiri kinyume na sheria zinazokataza mikusanyiko ya watu wengi.
Pia, Wakenya bado wanasalimiana kwa mkono na kupigana pambaja. Kuna watu wengine walio na imani ya kuchekesha na kwa wakati huo huo, ya kuhuzunisha.
Mwandishi huyu alisikia mtu mmoja akisema kuwa ugonjwa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, hauwezi kushika watu kutoka jamii moja.
Alijigamba hivyo baada ya kusalimia kwa mikono jamaa anayeaminika kuwa damu sawa na yake.
Kabla ya kafyu kuanza Jumatano saa moja jioni, saa ambayo hata hivyo haijakuwa ikizingatiwa mtaani Kariobangi South Civil Servants, imekuwa ikichelewa kuanza kwa karibu dakika 30, raia kadhaa walisikika wakisema, “Tunalipa ushuru na lazima serikali inunue tear-gas.”
Matamshi hayo yanamaanisha kuwa wataendelea na shughuli zao za nje ya nyumba kama kawaida hadi pale watakapoona maafisa wa usalama na kufurushwa.
Mamia ya Wakenya pia wanasafiri kutoka mijini hadi mashambani licha ya kukatazwa kufanya hivyo ili kuzuia uenezaji wa virusi hivyo.
Tabia hizi za kushangaza huenda ndizo zimesukuma serikali kuonya Jumatano kuwa italazimika kuchukua hatua kali zaidi kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona iwapo kutakuweko na ongezeko la visa vya maambukizi kutokana na wananchi kuendelea kuvunja amri hizo.
Mwandishi huyu pia aliona kisa cha kutia moyo. Alishuhudia kiasi kizuri cha watu waliovalia barakoa (mask), ambazo pia ni njia moja ya kuzuia maambukizi. Hata hivyo, tatizo ni kuwa karibu asilimia 50 ya watu walioonekana wamevalia barakoa hizo, walikuwa na mzaha mtupu.
Badala ya kuvaa barakoa ifunike pua na kinywa, walikuwa wamefunika kidevu ama wamevaa kwenye shingo kama kwamba ni tai.
Wengi sana walionekana wamefunika kinywa pekee, huku pua zikiwa nje.