• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
COVID-19: Likizo iliyopitiliza yafanya wanafunzi, aghalabu wenye umri mkubwa, waanze biashara

COVID-19: Likizo iliyopitiliza yafanya wanafunzi, aghalabu wenye umri mkubwa, waanze biashara

Na LYDIA OMAYA

SERIKALI imelazimika kurefusha likizo ya wanafunzi haswa wale wa shule za misingi na upili hadi mwaka 2021 kufuatia janga la corona humu nchini.

Vyuo vikuu huenda vitafunguliwa mwezi Septemba ikiwa vitaweza kuzingatia mwongozo utakaotolewa au uliotolewa na serikali.

Hali hii inatatanisha lakini wanafunzi hawana budi kusalimu amri na kukaa nyumbani.

Huenda jambo hili la likizo lisionekane kuwa pigo kubwa kwa wanafunzi wa chuo lakini ukweli ni kuwa wameathirika pakubwa.

Baadhi wamechoshwa na nyumbani. Wengi wameanzisha biashara angalau wapate kujikimu kimaisha.

Agizo la kukaa nyumbani kwa muda zaidi kutoka kwa serikali limesambaratisha ndoto za wanafunzi wengi. Kuna wale waliotarajia kupiga hatua ya masomo lakini sasa hawana budi kusubiri. Kuna wale waliokuwa karibu kutamatisha, imewalazimu kukaa nyumbani.

“Hatuwezi kukaa nyumbani na kuosha mikono tu. Baadhi ya mipango yetu imeharibiwa,” mwanadada Lydiah Mong’ina ambaye ni mfanyabiashara na mwanafunzi alisema.

Akaongeza: “Hii likizo iliyopitiliza inamaanisha kuahirishwa kwa karibu kila kitu kuanzia kukamilisha kwetu kwa masomo kiwango chetu, kupata ajira na hata kuanza maisha ya ndoa. Tutazeekea kwa akina baba zetu!”

Hili linaonyesha kuwa wanafunzi wengi hawawezi wakasubiri elimu yao au ujuzi wao wa shuleni kuwapa ajira mapema jinsi walivyotajaria hapo awali. Ngojangoja huumiza matumbo ndiposa wamechukua hatua ya kujitafutia ajira au kitu cha kujishughulisha.

Wazazi wamekiri kwamba mahitaji ni mengi wanayokuwa nayo watoto wao haswa wa vyuo na mara nyingi huwa wanawategemea wanapokuwa shuleni kukirimia mahitaji hayo. Itakuwa vigumu kuyapata sasa ikiwa wataketi nyumbani tu kwa sababu hakuna pesa wanazopokea toka kwa wazazi.

Wanafunzi wengine wanajihusisha na biashara ili kutafuta karo na pesa za matumizi shuleni siku za usoni na hivyo basi kwao hii ni nafasi inayowafaa sana.

Wazazi wengi wamewaanzishia watoto wao biashara na wengine kujiunga na biashara za wazazi ili kufanikisha lengo la kutafuta karo na hata kodi shuleni.

Hali hii ya biashara inazua hofu hata ingawa inafaidi wanafunzi kwa njia moja au nyingine kwa sababu itakuwaje likizo ikimalizika na wasione haja ya kurudi shuleni tena?

Litakuwa jambo gumu kwa vile idadi ya wanafunzi kuacha shule itaongezeka na hiyo ni ishara ya hatari kubwa kwa siku zijazo.

Mwandishi ni mtafiti

  • Tags

You can share this post!

Sitabomoa makaburi ya Waislamu, Gavana aahidi

Wakuzaji pamba kufaidi baada ya Rivatex kushirikiana na...

adminleo