Makala

Dai wabunge wanaomfukuza Gachagua ‘wamelazimishwa’

Na CHARLES WASONGA October 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MASWALI yameibuka baada ya baadhi ya wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya, waliotia saini hoja ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua kubadili msimamo wao na kuipinga.

Wabunge hao wanaotoka ngome ya Bw Gachagua ya Nyeri ni Geoffrey Wandeto wa Tetu, Njoroge Wainaina (Tetu) na Mbunge Mwakilishi wa Nyeri Rahab Mukami.

Mbunge mwingine ambaye amepinga hoja hiyo inayodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, baada ya kuitia saini ni Mbunge Mwakilishi wa Embu Pamela Njoki.

Wanne hao ni miongoni mwa wabunge 291 ambao majina yao yalisomwa na Bw Mutuse bungeni Jumanne alasiri akisema wanataka Bw Gachagua ang’atuliwe afisini kwa tuhuma za kutenda makossa 11 ukiwemo ukiukaji wa Katiba.

Kimsingi, wabunge hawa walisema walibadili msimamo wao baada ya kusikiza hisia za wakati wa maeneo wanayowakilisha bunge ambao wanapinga kutimuliwa kwa Bw Gachagua.

Aidha, walidai walichukua hatua hiyo baada ya kuisoma hoja hiyo na kubaini kuwa tuhuma dhidi ya Naibu Rais hazina mashiko.

“Baada ya kujisaili na kusoma hoja hiyo kwa undani, nimegundua kuwa haya ni mambo ambayo naibu raia na rais wanaweza kuketi na kusuluhisha kwa sababu Kenya ni kubwa kuliko sote. Aidha, nimesikiliza hisia za watu mashinani na kung’amua kuwa watu wa Nyeri wanapinga kuondolewa kwa Naibu Rais, Bi Mukami akasema mjini Nyeri siku moja baada ya hoja hiyo kuwasilishwa rasmi katika bunge la kitaifa.

Kwa upande wake Bw Wandeto akasema hivi: “Tulipowauliza watu wetu wanasema hawaoni kama suala hili la kumtimua Naibu Rais linapasa kupewa kipaumbele. Wanahisi tunapaswa kuelekeza nguvu zetu katika changamoto zingine zinazowasibu. Kama wawakilishi wa watu ni wajibu wetu kuwakiliza watu wetu na kufanya wanavyotaka. Kwa hivyo, Jumanne nitapiga kura ya ‘LA’ kwa hoja hiyo.”

Bw Wainaina na Bi Njoki pia walisema waliamua kupinga hoja hiyo baada ya “kusikiza sauti za watu wetu”.

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Herman Manyora hatua ya wabunge hao kubadilisha misimamo yao sio jambo geni bali linaakisi mienendo ya wanasiasa nchini.

Hata hivyo, anasema kuwa sababu kuu iliyochangia wabunge hao kupinga hoja hiyo ni haja ya kudumisha mustakabali wao wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

“Ukweli ni kwamba masaibu yanayomzonga Bw Gachagua yamemfanya kuwa maarufu hata zaidi hasaa katika eneo la Mlima Kenya Magharibi. Wakazi wanahisi kuwa ‘anasulubiwa’ kwa kutetea masilahi yao serikalini. Kwa hivyo, wanawasawiri wabunge wanaounga mkono hoja ya kumtimua Bw Gachagua kama adui wao mkubwa,” anaeleza Profesa Manyora ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

“Hali itakuwa mbaya zaidi haswa kwa wabunge kutoka kaunti  ya Nyeri alikozaliwa Naibu Rais na ndio maana akina Wandeto na Bi Mukami wameamua kujitenga na hoja hii,” anaeleza, akaongeza kuwa wengi wa wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya wataendelea kujitenga na hoja hiyo.

Kwa upande wake, wakili James Mwamu anasema kuwa huenda idadi kubwa ya wabunge 291 waliotiwa saini zao kwa hoja hiyo walishawishiwa kufanya hivyo.

“Madai ya wabunge kutishwa na hata kuhongwa ili kupishwa miswada na hoja mbalimbali kulingana na matakwa ya rais yamekuwepo. Kwa mfano, mwaka huu Rais Ruto mwenyewe amewahi kutoa vitisho kwa wabunge wake wa Kenya Kwanza akiwataka kupitisha miswada iliyodhaminiwa na serikali kama vile Mswada wa Fedha wa 2024 uliokataliwa na vijana wa Gen-Z,” anaeleza.

Itakumbukwa kuwa mnamo Jumamosi, Septemba 28, Bw Gachagua mwenyewe alidai, bila kutoa ithibati yoyote, kwamba wabunge walihogwa Sh5 milioni ili watie saini hoja ya kumbandua afisini.

“Njeri aliitwa na wakajaribu kumuuzia woga kwa kumshurutisha atie saini hoja hiyo lakini akakataa. Alipewa Sh5 milioni na akakataa. Seneta Jame Murango pia alipewa pesa lakini akakataa,”  Bw Gachagua akaeleza alipowahutubia wakazi wa Mwea, Kaunti ya Kirinyaga.

Bi Njeri (jina halisi, Jane Njeri Maina) ni Mbunge Mwakilishi wa Kirinyaga naye Bw Murango ni Seneta wa Kaunti hiyo hiyo.