Makala

Dalmas Otieno ndiye mwasisi wa huduma dijitali serikalini

Na KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK May 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

DALMAS Anyango Otieno, aliyekuwa kibaraka sugu wa Kanu wakati wa utawala wa Moi, machoni pa wanasiasa wa upinzani alionekana mtu mwenye kutafuta fursa za kisiasa wakati wa uchaguzi wa vyama vingi.

Hata hivyo, Rais Mwai Kibaki alipomteua kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma katika Serikali ya Muungano wake na Raila Odinga, alimtegemea mno kwani alikuwa amebobea sana katika masuala ya uongozi wa serikali.

Otieno alikuwa amehudumu kama waziri kwa takribani miaka 10 na alikuwa anaifahamu vizuri mifumo ya utumishi wa umma, na hivyo aliweza kurekebisha sehemu zilizokuwa zimedhoofika.

Ingawa alikuwa mwaminifu kwa Kanu kwa muda mrefu, alielewa kuwa alikuwa anahudumu chini ya serikali ya mageuzi na alianza kufanya mabadiliko; mojawapo ikiwa ni kuweka huduma za serikali katika mfumo wa kidijitali.

Mwaka 2007, Bw Otieno alijiunga na chama cha Orange Democratic Movement (ODM) cha Raila Odinga kama njia rahisi ya kurejea kwenye siasa baada ya kutengwa kwa miaka mitano. Hatua hii ilimrudisha serikalini kama waziri katika Serikali ya Muungano iliyoundwa baada ya uchaguzi tata wa mwaka huo.

Licha ya kuwa alitoka chama cha upinzani, Rais Kibaki alimkubali kwa urahisi kutokana na uzoefu wake mkubwa serikalini na upole wake. Hakumwangusha. Alifanya mageuzi mengi muhimu katika Wizara ya Utumishi wa Umma, ambayo ilikumbwa na ufisadi na uzembe uliorithiwa kutoka enzi za Kanu.

Bw Otieno alielewa mahali ambapo matatizo yalikuwepo, akiwa mmoja wa washauri wakuu wa Rais Moi. Katika mahojiano, alieleza kuwa chini ya Kibaki, kulikuwa na msisitizo mkubwa kwenye utendaji na ufanisi, na alitekeleza falsafa hizo ili kuhakikisha huduma bora kwa wananchi.

Alikuwa akikutana na Rais Kibaki karibu kila siku katika Harambee House kwa mashauriano. Aliongoza pia wizara nyingine kama Viwanda (1988–1991), Kazi na Maendeleo ya Wafanyakazi (1991), na Uchukuzi (1991–1996).

Mbali na uongozi, Bw Otieno aliheshimika kama mpatanishi hodari katika vikao vya ushauri.Mwaka 2008, Prof Anyang’ Nyong’o akipata matibabu, Bw Otieno alisimamia Wizara ya Afya na kubatilisha mpango wa bima ya afya kwa wagonjwa wa nje uliokuwa umeanzishwa.

Alipinga mpango huo kwa msingi wa takwimu zisizotosha na kusisitiza haja ya uchambuzi wa kitaalamu kabla ya utekelezaji.

Mojawapo ya mafanikio yake makubwa yalikuwa uzinduzi wa Mfumo wa Kudhibiti Kumbukumbu Serikalini (IRMS) Desemba 2011, hatua muhimu iliyoweka msingi wa mfumo wa ofisi usiotegemea karatasi, kama ilivyoainishwa katika Ruwaza ya Maendeleo ya 2030.

Pia alisaidia nchi jirani ya Sudan Kusini kuanzisha mfumo wa utumishi wa umma kwa kuwapeleka watumishi 72 wa Kenya Juba kutoa mafunzo. Bw Otieno alizaliwa Aprili 19, 1945, mwaka uliojaa matukio makubwa duniani kama kumalizika kwa Vita Kuu vya Pili vya Dunia.

Alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Makerere mwaka 1971 na kuwa mmoja wa watu waliojivunia elimu na hadhi kijijini kwao Kengeso, Kamagambo, eneo linalojulikana kwa ushawishi wa Waadventista Wasabato.

Aliwahi kufanya kazi kwenye sekta ya bima, kuwa mwenyekiti wa KCB, na kuanzisha kampuni yake binafsi ya ushauri kabla ya kuingia kwenye siasa mwaka 1988, ambapo alichaguliwa kuwa mbunge wa kwanza wa Rongo kupitia chama cha Kanu.

Baadaye alipoteza kiti hicho mwaka 1992 kwa mjomba wake Linus Aluoch Polo wa Ford Kenya. Mwaka 1997 alipoteza tena kwa Ochilo Ayacko.

Hata hivyo, Moi alimteua kuwa kuwa mbunge maalum na akakwezwa kuwa waziri.Alituhumiwa kwa kutumia utawala wa mikoa kuendeleza mgawanyiko wa kisiasa Suba na Kuria katika maeneo ya Nyanza.

Pia alikuwa mmoja wa waliofanikisha muungano kati ya Kanu na NDP ya Raila Odinga mwaka 2002.Baada ya kupoteza uchaguzi wa 2002, alirejea 2007 kwa tiketi ya ODM na kuungwa mkono na Raila.

Lakini 2014 alishtumiwa tena kwa kushirikiana na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na kutajwa kuwa ‘msaliti’. Alijaribu kuanzisha vuguvugu la Kalausi kupinga ushawishi wa Raila Nyanza, lakini lilifeli.Mwaka 2017, alishindwa katika kura ya mchujo ya ODM na baadaye kama mgombea huru.

Mwaka 2018, aliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC), tume aliyosaidia kuanzisha.Katika historia ya serikali ya mageuzi ya Rais Kibaki, Dalmas Otieno atakumbukwa kama mmoja wa mawaziri waliobobea, waliotoa mchango mkubwa kwa taifa.