Makala

DAU: Awapa kipazasauti waathiriwa wa ubakaji

May 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KAMA vitongoji duni vingine, Kibra hakijasazwa kutokana na visa vya dhuluma za kimapenzi hasa dhidi ya wasichana na wanawake.

Hii ndiyo sababu kuu iliyomsukuma Editar Adhiambo, 30, kuhakikisha kwamba waathiriwa wa unyama huu wanapata haki.

Anaendeleza vita hivi katika kijisehemu cha Kisumu Ndogo kupitia mradi alioanzisha wa Feminist for Peace, Rights and Justice Center.

“Madhumuni ya mradi huu sio tu dhidi ya dhuluma za kimapenzi, bali pia za kinyumbani,” anaeleza Adhiambo.

Baadhi ya mambo ambayo wamekuwa wakijihusisha nayo ni kufuatilia wahanga wa ubakaji na ulawiti.

“Baada ya kuwafuatilia, tunahakikisha kwamba visa hivi vinaripotiwa katika kituo cha polisi. Pia, tunawapeleka hospitalini kuhakikisha kwamba mbali na kupata matibabu na dawa za kuzuia maambukizi ya HIV (Pre-exposure prophylaxis) PrEP, ushahidi haupotei. Isitoshe, pia huwatafutia washauri nasaha,” anasema huku akiongeza kuwa haya ni mbali na kufuatilia kesi mahakamani kuhakikisha kwamba haki inatendeka.

Kulingana naye, kwa siku wanapokea visa viwili vya dhuluma za kimapenzi ambapo tangu mwaka jana amefuatilia kesi tatu ambazo zilifikia tamati mahakamani huku washtakiwa wakifungwa.

“Kufikia sasa zaidi ya wasichana na wanawake 100 wamenufaika kutokana na mradi huu,” anaeleza.

Licha ya jitihada hizi, anasema kwamba visa vya ubakaji bado viko juu.

“Tatizo ni kwamba watu wengi hukaa kimya, suala linalofanya iwe vigumu kufuatilia kesi hizi,” anaeleza.

Hii sio changamoto ya pekee anayokumbana nayo.

“Visa vingi haviripotiwi. Kulingana na majirani na duru zetu, tunasikia tu vimefanyika na hivyo siwezi kufuatilia ikiwa hakuna nia ya kuwafichua wahalifu hawa,” anaeleza.

Asema kwamba sababu kuu ni kuwa kuna baadhi ya wakazi ambao hawako tayari kujitokeza na kutoa taarifa uhalifu wa aina hii unapotendeka.

“Hii ni kutokana na kuwa visa vingi vya ubakaji, ulawiti na dhuluma zingine za kimapenzi hutekelezwa na watu wanaotambulika,” anasema.

Aidha, kizingiti kingine ni kwamba mara kwa mara amepokea vitisho.

“Nimepokea vitisho hasa kutoka kwa watu wasiotaka nifuatilie kesi fulani. Aidha, kumekuwa na jaribio la kunihonga ili niache kufuatilia baadhi ya kesi,” anaongeza.

Kutolegeza kamba

Licha ya changamoto hizi, anaahidi kutolegeza kamba katika juhudi hizi.

Katika masuala ya kupiga vita dhuluma za kinyumbani hasa wao hujadili jinsi ya kusaidia wahanga huku wakiwapa nguvu kiuchumi na kijamii katika harakati za kuwaandaa kuwa viongozi wa siku zijazo.

Juhudi zake zilianza akiwa msichana mdogo. Hata hivyo alipata ujasiri wa kuzungumzia masuala haya alipokomaa kiumri.

“Wakati huo nilikuwa na miaka 21 ambapo nilikuwa mwanachana mwanachama wa kikundi cha Sita Kimya, kilichokuwa kikiwasaidia wahanga wa dhuluma za kimapenzi kwa kuwapa jukwaa la kuzungumzia wazi waliyokumbana nayo,” anaeleza.

Akiwa hapa, aligundua kuwa kulikuwa na idadi kubwa ya wasichana zaidi ya miaka 18 na hata wanawake waliokomaa kiumri ambao bado walikuwa wanaogopa kuzungumzia wazi masaibu yao.

“Hii ilinifanya niingiwe na hofu kwani nilijiuliza ikiwa hawa wanawake waliokomaa hivi wanaogopa kuzungumzia matatizo haya, je, watoto wasichana watapata wapi sauti?”

Kwa sasa juhudi zake zimemtambulisha sio tu mtaani anakoishi, bali pia katika vyombo vya habari na baadhi ya viongozi mtaani Kibra.

Ni suala lililomfanya kuwa mmojawapo wa wanawake waliochaguliwa kushiriki katika shindano la Miss President na kumaliza miongoni mwa 40 bora.

Mbali na hayo amepokea tuzo mbalimbali ambazo anasema kwamba hatozitaja kwani kwake hilo sio muhimu.

“Ari yangu ni kuona kazi ninayofanya inawafaidi watu ninaopigania,” anaongeza.