Dau la Gachagua, Kalonzo linavyopigwa na dhoruba kali kuelekea 2027
MIPANGO ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuungana kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 sasa inaonekana kukumbwa na dhoruba kutokana na uasi dhidi yao katika ngome zao za kisiasa.
Hii ni kufuatia hatua ya wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya kujitenga na Bw Gachagua, siku chache baada ya Kiongozi wa Narc Charity Ngilu kuonekana kugura kambi ya Bw Musyoka ndani ya muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.
Mnamo Alhamisi jumla ya wabunge 48 kutoka Mlima Kenya Magharibi walimuasi Gachagua na kuelekeza uaminifu wao kwa Waziri wa Usalama Kithure Kindiki.
Viongozi hao walitoa kauli hiyo siku mbili baada ya wenzao 14 kutoka Mlima Kenya Mashariki kujitenga na Naibu Rais wakishikilia kuwa Profesa Kindiki ndiye msemaji wao.
Na mnamo Jumamosi, Septemba 6, Bi Ngilu aliwahimiza viongozi na watu wa jami ya Wakamba kuunga mkono serikali ya Rais William Ruto ili eneo hilo lifaidi kimaendeleo.
Hii ni kinyume na msimamo wa Bw Musyoka ambaye amedinda kushirikiana na serikali hii akishikilia kuwa ataendelea kuikosoa huku akijiandaa kumwondoa mamlakani Rais Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Itakumbukwa kuwa mnamo Juni 21, mwaka huu, Mbw Musyoka na Gachagua walishiriki jukwaa moja katika kaunti ya Kiambu ambapo waliahidi kushirikiana kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Kiongozi huyo wa Wiper alimtaja Naibu Rais kuwa “kiongozi jasiri” na kuahidi kumtetea kutokana na masaibu ya kisiasa yanayomzonga ndani ya chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA).
“Hii ndio mara yangu ya kwanza kuketi kando ya Rigathi Gachagua. Navutiwa na uwezo wako wa kupambana na wale wanaojaribu kukupiga vita,” Bw Musyoka akasema katika eneo la Ruiru wakati wa hafla moja ya kanisa.
Alikuwa akiwarejelea baadhi ya wabunge wa UDA ambao walikuwa wakimpiga Bw Gachagua vita kisiasa na hata kutisha kuwasilisha hoja ya kumtimua afisini.
“Nakuhakikishia kuwa nitakuunga mkono katika vita hivi. Na Mungu akipenda tutafanya tutashirikiana pamoja kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027,” Bw Musyoka akaeleza.
Kwa upande wake, Bw Gachagua alisema yu tayari kushirikiano na viongozi “wote hata majirani zetu wa Ukambani kwa manufaa ya watu wetu.”
Wadadisi wa masuala ya kisiasa walifasiri mkutano wa wawili hao kama mwanzo wa mpango mpana wa wao kushirikiana kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
“Sio sadfa kwa wanasiasa wa mirengo hasimu kushiriki jukwaa moja walivyofanya Mbw Gachagua na Kalonzo. Kuna dalili kwamba wanapania kubuni ushirikiano wa kisiasa,” mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Gitile Naituli alinukuliwa akisema wakati huo.
Lakini sasa juhudi za wawili hao kudumisha usemi wa kisiasa katika ngome zao zinakumbwa na pingamizi, hali ambayo inaweza kuzima mipango yao ya kushirikiana kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Siku chache baada ya kuibuka kwa misukosuko ndani ya Azimio baada ya Rais Ruto kufaulu kuvutia chama cha ODM upande wake, Bi Ngilu ambaye awali aliamua kuegemea mrengo wa Musyoka katika Azimio, amepiga abautani.
“Naomba Wakamba wajipange na kuunga mkono utawala wa Rais Ruto ndani ya kipindi hiki cha miaka mitatu. Lazima tuwe sehemu ya utawala wa sasa ili tunufaike kimaendeleo,” akasema alipohudhuria hafla moja ya mazishi katika eneo bunge la Kitui ya Kati.
Bw Odinga alipoamua kushirikiana na serikali na kuruhusu kuteuliwa kwa wandani wake watano katika baraza la mawaziri, Bi Ngilu ni miongozi mwa vinara wa Azimio waliopinga hatua hiyo wakiongozwa na Bw Musyoka.