• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
DAU LA MAISHA: Ametetea haki za wanyonge miaka tisa

DAU LA MAISHA: Ametetea haki za wanyonge miaka tisa

Na PAULINE ONGAJI

AMEJITWIKA jukumu la kutetea haki za kibinadamu, shughuli ambayo ameitekeleza kwa miaka tisa sasa.

Huku akiendesha shughuli zake katika Kaunti ya Taita Taveta, Bi Flora Ali amejizatiti katika shughuli za uanaharakati huku akihudumia mashirika kadhaa.

“Nimekuwa nahudumu katika mashirika mbali mbali ikiwa ni pamoja na Taita Teen Pregnancy, Women for Change na shirika la Kiislamu la kutetea hakiza kibinadamu, MUHURI ambapo nimehudumu kwa miaka miwili,” aeleza.

Kwa sasa anafanya kazi na shirika la MUHURI kama mwelimishaji wa kijamii na mratibu katika kaunti hiyo.

“Hapa majukumu yangu ni pamoja na kuelimisha jamii kuhusu masuala kama vile ya uongozi,” aeleza.

Mbali na hayo, pia anafanya kazi na shirika la Women for Change, lenye makao yake eneo la Mwatate ambapo anahusika na kuwapa wanawake na vijana nguvu kupitia shughuli za mafunzo na uhamasishaji.

“Kupitia elimu kwa jamii, nataka kuhakikisha kwamba jamii inaweza kuelewa majukumu yake na kushiriki katika shughuli zinazoathiri jamii hasa katika uongozi.”

Mbali na hayo, yeye ni mtetezi wa haki za kibinadamu na mwanaharakati dhidi ya dhuluma za kijinsia eneo la Taita Taveta.

Katika masuala ya dhuluma za kijinsia, anapigania jinsi ya kukabiliana na visa vya dhuluma dhidi ya wanawake na watoto hasa katika viwango vya mashinani.

“Nahakikisha kwamba kupitia mafunzo kuhusiana na dhuluma za kijinsia, nawasaidia kufikia haki vilivyo. Kwa hivyo nashirikiana na washikadau wengine kama vile polisi, wahisani na jamii kuwaokoa kutokana na dhuluma,” asema.

Pia, amekuwa akifanya kazi na mashirika mengine ya kijamii ambapo amekuwa akipigania haki za watoto, vijana na wanawake kuanzisa kiwango cha mashinani. “Najiita ajenti wa mabadiliko na hivyo nahusika sana katika mafunzo na shughuli za kuhamasisha jamii.”

Mafunzo yake mengi pia yamekuwa yakihusisha ushiriki wa umma katika siasa, kusaidia watu wa jamii kubadilisha mtazamo wao kuhusiana na mambo tofauti.

“Hii ni sehemu ambayo imeathirika kutokana na baadhi ya mila na itikadi zinazoirudisha nyuma. Hapa, jukumu langu ni kuelimisha wakazi kuhusu jinsi mila hizi zinazuia maendeleo, na hivyo kutumai kwamba watabadili mitazamo kimaisha,” asema.

Pia, amekuwa akifunza ujuzi wa kimaisha huku akizuru shule mbali mbali. “Nimefunza walimu kuhusu ujuzi wa kimaisha, mafunzo ambayo yametupeleka katika taasisi mbali mbali mjini Mombasa,” aelesa.

Hii ni mbali na kufunza jamii kuhusu jinsi ya kuhakikisha kwamba viongozi wao wanawajibika.

Kitu tosha

Licha ya kwamba hajawahi tambuliwa kutokana na jitihada zake, anasema kwamba mabadiliko anayoleta katika jamii ni tosha.

Tayari bidii yake imeanza kuvuna matunda kwani nimeshuhudia mabadiliko ya kitabia miongoni mwa vijana.

Vita vyake dhidi ya dhuluma za kijinsia vimesaidia waathiriwa hasa wa ubakaji kufikia haki.

“Tumekuwa tukifuatilia kesi kuhakikisha kwamba wahalifu wanapelekwa mahakamani,” aeleza.

Aidha, kumekuwa na mabadiliko kuhusu ushiriki wa umma katika shughuli za kimaendeleo, mabadiliko kimtazamo kuhusiana na mambo tofauti, suala ambalo limechangia pakubwa katika kusaidia watu kufikia uamuzi wa busara katika maisha yao ya kila siku.

Hata hivyo, haijakuwa rahisi huku akikumbana na changamoto mbali mbali katika shughuli zake za kila siku.

“Kwa mfano kwa visa vya dhuluma za kijinsia unapata kwamba tunalazimika kuwapa waathiriwa makao hasa kesi inapoendelea, jambo linalohitaji pesa.”

Kwa sasa ndoto yake ni kuhakikisha kwamba visa vya dhuluma za kijinsia, vinapungua, vilevile wananchi kutoka kila pembe nchini wanapata ufahamu kuhusu masuala ya uongozi na hivyo kuwashinikiza viongozi wao kuwajibika.

  • Tags

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Alinitoroka nikiwa mjamzito sasa anataka...

UMBEA: Usihangaike bure; furaha yako unayo kiganjani mwako

adminleo