• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 5:50 AM
David Sankok: Sindano ndio ilinigeuza mlemavu ingawa sasa umegeuka kuwa baraka kubwa!

David Sankok: Sindano ndio ilinigeuza mlemavu ingawa sasa umegeuka kuwa baraka kubwa!

NA LABAAN SHABAAN

MBUNGE wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) David Sankok, 46, alizaliwa bila ulemavu mwaka wa 1978 kijijini Entoltol katika Kaunti ya Narok.

Ulemavu wa miguu uliomkuta akiwa shuleni hapo mwanzoni ulimpiga mshipa asijue la kusema wala la kufanya.

Je, ni nini kilimfanyikia mvulana mchangamfu aliyezaliwa mzima kuwa mlemavu?

Ilikuaje mvulana mchungaji mifugo aliyefana katika mchezo wa mpira wa miguu na mbio fupi akagandishwa baina ya magongo milele?

“Nilibebwa hadi hospitalini Naivasha kutibiwa ugonjwa wa kichomi (pneumonia).

Daktari alinidunga sijui kama alisahau kutumia sindano ya binadamu ama ya ng’ombe lakini nilipona,” alisema katika podkasti ya Dau la Maisha.

“Nilipoamka kutoka kitandani niliangukaanguka kasha nikamwarifu mama yangu. Ilibidi nipelekwa katika Hospitali ya Kijabe.

Daktari alinitathmini akaingia chumbani ambamo alitoka akiwa ameshika jozi ya magongo.

Akaniambia, ‘Shika ujifunze kutumia kwa sababu utatumia katika maisha yako yote,’” alikumbuka.

Nilikuwa na Changamoto Kujikubali Nimelemaa

Bw Sankok aliona kiza katika maisha yake baada ya kugundua kuwa ataishi katika hali ya ulemavu.

Alifikiria sana jinsi ya kuishi katika jamii ya Kimaasai anayosema inategemea nguvu za kimwili kujimudu kupitia ufugaji wa kuhamahama.

“Ili uweze kuchunga ng’ombe, kufanya biashara na kutafuta maji na malisho, lazima uwe na nguvu za kimwili,” alikiri.

“Ilibidi nijikubali na kukumbatia masomo ambayo niliona yalikuwa tegemeo langu la kipekee,” aliongeza.

Mujibu wa mbunge huyu, baada ya kukabiliwa na hali hii, mtazamo wake wa maisha ulibadilika.

Awali hakuwa anafanya vizuri katika masomo ila ulemavu ulimpa dira mpya na akaanza kufana shuleni.

“Unaweza kupitia changamoto nyingi. Ukifanya uamuzi, maisha yako yatabadilika,” aligundua.

Kadhalika, Bw Sankok anaeleza kuwa huenda angeuliwa katika wizi wa mifugo msituni kama asingekuwa mlemavu.

Vile vile, anaongeza kuwa hali hiyo imemletea baraka ya kuwa mbunge na mwakilishi wa watu wanaoishi na ulemavu.

“Nimekuwa mbunge mteule kwa miaka mitano Kenya na pia mjumbe wa EALA sasa sababu ya ulemavu,” alisema.

Ulemavu Ulimchochea Kuwa Daktari

Japo anasimulia masaibu yake kwa uchangamfu, haikuwa rahisi kwake kukubali kuwa daktari aliyefaa kumtibu alimgeuza mlemavu.

Ulemavu alioupata uliwasha moto wa njaa ya elimu hasaa ya kuwa daktari.

Alitaka kuwa tabibu agangue chanzo cha ulemavu wake.

Na hapo ndipo alitia fora masomoni akaishia kusoma udaktari katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

“Niligundua daktari alinidunga neva isiyofaa hadi ikafa na nikakuwa mlemavu,” alieleza.

Anaendelea kufafanua kuwa aliwahi kumchumbia msichana ili amuoe lakini akatemwa kama kiazi moto.

“Hata kama alinikataa kwa sababu ya ulemavu na umaskini, najua sasa ananitamani kwani nimefaulu maishani kama familia yao aliyoringa nayo,” alifunguka.

Akiri Amefanikiwa Maishani Licha ya Ulemavu

Sasa Bw Sankok ni mjumbe wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kuteuliwa na serikali ya Kenya Kwanza 2022.

Aliwahi kuwa mbunge maalum kati ya mwaka wa 2017 – 2022 akiwakilisha masuala ya wanaoishi na ulemavu katika bunge la kitaifa.

Kabla ya kuwa mbunge, Sankok alihudumu wadhifa wa mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Watu Wanaoishi na Ulemavu (NCPWD) kati ya mwaka wa 2014 – 2017.

Mbali na kazi ya siasa, Bw Sankok anaendesha biashara ya kufuga ng’ombe wa maziwa, nyama na Hoteli ya Osim Country Lodge.

  • Tags

You can share this post!

Iko wapi gesi ya Sh500? Kilio mtungi wa kilo 13 ukiongezeka...

Mkulima Nakuru aliyeacha majirani vinywa wazi kwa kung’oa...

T L