Makala

Dawa ya kitamaduni ya China inayoangamiza punda Kenya na Afrika

Na CALVIN SOLOMON ONYANGO December 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

PUNDA wako katika hatari ya kutoweka. Barani Afrika na hapa Kenya, biashara kubwa na isiyodhibitiwa ya ngozi za punda, inayochochewa na mahitaji ya dawa ya jadi ya China ijulikanayo kama ejiao, inaangamiza idadi ya punda na jamii zinazowategemea katika shughuli zao za kijamii, kiuchumi na kitamaduni.

Utafiti wa hivi karibuni hapa Kenya umeonyesha kuwa asilimia hadi 97 ya wamiliki wa punda wamewahi kuibiwa punda wao. Biashara hii katili haishinikizi tu kutoweka kwa punda; inaangamiza kabisa maisha ya watu wanaowategemea kuishi.

Kwa vizazi vingi, punda wamekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa vijijini. Wanyama hawa wapole na werevu hubeba bidhaa kwenda sokoni, kubeba maji na kuni, na kupatia familia nafasi ya kupata kipato na kuwasomesha watoto wao.

Kwa wanawake wengi, punda ni mkombozi, mshirika anayewasaidia kukabiliana na changamoto za kila siku. Punda wana hisia, wana akili na hujenga uhusiano wa karibu na binadamu wanaofanya nao kazi.

Hata hivyo, biashara ya kimataifa inayohitaji ngozi za punda milioni 5.9 kila mwaka kwa utengenezaji wa ejiao inawachukulia kama bidhaa tu, hivyo kuwaacha wakikabiliwa na wizi, ukatili na kuchinjwa kinyama.

Biashara ya ngozi za punda ni janga la ustawi wa wanyama. Punda huondolewa kwao, hulazimishwa kutembea umbali mrefu au kusafirishwa katika mazingira mabaya kuvuka mipaka, na hatimaye kuchinjwa kinyama.

Wale wachache wanaosalia hubebeshwa mizigo kupita kiasi. Madhara hayawapati punda pekee, yanawaathiri wanadamu vilevile.

Punda anapoibwa, hatima ya familia pia huibwa, kwani wengi hawawezi kurudishwa. Madhara yake ni makubwa: watoto, hasa wasichana, huacha shule ili kufanya kazi ambazo punda angefanya. Bila msaidizi wao, wanawake hubeba mzigo wa kazi, kimwili na kihisia.

Mwaka huu, The Donkey Sanctuary ilichapisha matokeo ya utafiti huru uliofanywa na Chuo Kikuu cha Maasai Mara kuhusu athari za biashara ya ngozi.

Matokeo hayo yanaonyesha ukubwa wa janga hili katika jamii za vijijini, yakionyesha familia zilizokwama katika umaskini na mustakabali wao kuangamizwa.

Kuna mwamko mpya wa kukomesha mateso haya na kuwalinda punda na jamii zinazowategemea, kakini hatuwezi kufanya peke yetu. Tunahitaji washirika na wadau kuungana nasi kupinga biashara hii katili.

Kuna hatua zinazopigwa. Mwaka 2024, Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika walikubali kusimamisha kwa bara lote uchinjaji wa punda kwa ajili ya ngozi.

Tunatoa wito kwa serikali, watunga sera na vyombo vya usalama kutekeleza kikamilifu uamuzi huu. Kenya tayari imeonyesha uongozi kwa kupiga marufuku uchinjaji wa kibiashara wa punda na kuanzisha Kikosi Maalum cha Dharura (RRI) ambacho kilidhibiti kwa kiasi kikubwa uchinjaji haramu uliokuwa ukiendelea.

Wiki hii, Bunge la Afrika Mashariki litapiga kura kuhusu kupiga marufuku uchinjaji wa punda kwa ngozi katika nchi wanachama. Huu utakuwa uwekezaji katika mustakabali wa bara ikiwa watapitisha sheria hiyo, kwa kulinda mojawapo ya rasilimali muhimu za Afrika.

Kila mmoja wetu ana jukumu. Lazima tuelimishane kuhusu umuhimu wa ustawi wa punda, kuunga mkono jamii katika kuwalinda, na kuwasemea wasio na sauti.

Punda ametutumikia kwa uaminifu kwa vizazi. Sasa ni wakati wetu kusimama na kuwatetea.