Makala

DCI walivyorudi zero baada ya kukosa kuhusisha Wanigeria wawili na kifo cha Waeni

February 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

GIZA limegubika uchunguzi wa mauaji ya kinyama ya mwanafunzi wa chuo kikuu Rita Waeni baada ya washukiwa wawili kuachiliwa huku maafisa wa uchunguzi wakilazimika kuanza uchunguzi upya.

Katika kile kinachostaajabisha, ni kwamba polisi wamefichua hawajapata ushahidi wa kuwahusisha raia wa Nigeria William Opia na Johnbull Asbor na mauaji ya Waeni ambayo yaliyomshtua hata mpasuaji mkuu wa maiti wa Serikali Dkt Johansen Oduor.

Polisi wamedokeza huenda Waeni aliuawa na mwanafunzi mwenzake ambaye wanatumia nguvu zote kumsaka.

Hata hivyo, raia hao wa kigeni walioachiliwa wataendelea kusaidia polisi katika uchunguzi wa mauaji ya Waeni kwa sababu waliachiliwa kwa masharti wawe wakipiga ripoti mara moja kwa wiki katika afisi ya Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI).

Opia na Asbor walipatikana na silaha zinazofanana na zile zilizotumika kukatiza maisha ya mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

Mnamo Ijumaa, Opia na Asbor waliamriwa na hakimu mkazi wa mahakama ya Makadara Agnes Mwangi wawe wakijisalimisha katika afisi ya uchunguzi wa mauaji ya kutatanisha katika afisi ya DCI mara moja kwa wiki.

Afisa anayechunguza kesi hiyo alieleza Bi Mwangi kwamba ushahidi uliopatikana kufikia sasa kutoka kwa kitengo cha DCI cha kufichua mauaji tata almaarufu CRIB, hauhusishi Opia na Asbor na mauaji ya Waeni, ambaye kufikia kifo chake, alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa nne JKUAT.

“Polisi wangali wanamsaka mshukiwa katika mauaji haya na wanashuku ni mwanafunzi mwenza wa marehemu katika chuo hicho cha JKUAT,” Bi Mwangi alielezwa na afisa wa uchunguzi.

Walipotiwa nguvuni, Opia na Asbor walipatikana na silaha zinazofanana na zile zinazoaminika zilitumika kumtoa uhai Waeni.

“Uchunguzi katika kesi hii unaendelea na kufikia sasa zimetimia siku 21 na hatujapata ushahidi wowote wa kuhusisha Opia na Asbor na mauaji ya kinyama ya Waeni,” hakimu alifahamishwa.

Hata hivyo, mahakama ilijuzwa polisi wamejitosa kikamilifu katika uchunguzi wa mauaji hayo wakitumai kwamba hivi karibuni watamtia nguvuni muuaji wa Waeni.

Hakimu alifahamishwa kwamba washukiwa hao wawili walinunua silaha walizopatikana nazo kutoka kwa jukwaa sawa na pale aliyetekeleza mauaji hayo ya Waeni alinunua silaha zake.

Mnamo Januari 31, 2024, polisi walikubaliwa kuwazuilia washukiwa hao wawili kwa siku 21 kisha wapate sampuli za DNA kutoka kwa washukiwa kulinganisha na sampuli zilizotwaliwa kutoka pahala pa mauaji.

Walipokamatwa, muda wa cheti cha usafiri cha Opia ulikuwa umeisha ilhali Asbor aliwaeleza wachunguzi kwamba pasipoti yake ilipotea miaka miwili iliyopita.

Washukiwa hao walitiwa nguvuni kufuatia uchunguzi wa kina dhidi yao.

Afisa wa polisi Konstebo Benjamin Wangila kutoka afisi ya DCI Kasarani aliambia mahakama kwamba Opia na Asbor hawaishi mbali na bwawa ambapo kichwa cha Waeni kilipatikana.

Kichwa kilichoaminika kuwa ni cha Waeni kilipatikana kwenye bwawa lililoko Kiambu mnamo Januari 21, 2024.

Maiti ya Waeni ilikuwa imekatwa vipande na kutupwa katika pipa la taka.

Walipokamatwa, Opia na Asbor walikuwa na kijishoka, kisu cha bucha, kitambulisho cha kitaifa cha raia wa Kenya (jina limebanwa), simu sita za kiunga mbali na kadi 10 za simu.

Kadi hizo za simu zilikuwa za kampuni za Safaricom, Airtel, Telkom miongoni mwa kampuni nyingine za mawasiliano.