Makala

Dili mpya kati ya Ruto na Raila itakayonusuru Wetang’ula ghadhabu za Azimio

Na SAMWEL OWINO February 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANDANI wa aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua wamefukuzwa kwenye uongozi wa kamati mbalimbali za Bunge huku Rais William Ruto na Kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga wakiafikiana kuhusu washikilizi wa nafasi hizo.

Hatua hiyo imemnusuru Spika Moses Wetang’ula ambaye alikuwa akikodolewa macho na kura ya kutokuwa na imani na uongozi wake. Bw Wetang’ula wiki jana alipuuza amri ya korti na kutangaza kuwa Kenya Kwanza itasalia Mrengo wa Wengi.

Mahakama ilikuwa imetoa uamuzi kuwa alikosea mnamo Agosti 2022 kwa kuwa mrengo wa Azimio ndio ulistahili kuchukua nafasi ya upande wa Wengi.

Katika mkutano uliofanyika katika Ikulu Jumatatu kati ya viongozi wa Wengi na wale Wachache, Rais Ruto alikubali kuruhusu Azimio ichukue uenyekiti wa kamati muhimu

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu wa Rais Prof Kithure Kindiki, Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen, Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot na mwenzake wa Wachache Steward Madzayo.

Wengine walikuwa Kiongozi wa Wengi Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah na mwenzake wa Wachache Junet Mohamed pamoja na Kiranja wa Wachache Millie Odhiambo.

Kati ya kamati ambazo Azimio itaongoza ni ile ya Bajeti, Afya, Biashara na Viwanda, Leba na Utangamano wa Kieneo. Kamati ya Bajeti ilikuwa ikisimamiwa na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

Mbunge wa Endebes Robert Pukose na mwenzake wa Runyenjes Karemba Muchangi nao walikuwa wakiongoza kamati za Afya na Leba mtawalia.

Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia na mwenzake wa Embakasi Kaskazini James Gakuya walikuwa wakiongoza kamati za Utangamano wa Kieneo na Biashara. Azimio inatarajiwa kuwasilisha majina ya wanachama wa kamati hiyo leo.

“Ndiyo kama Azimio, tuna mkataba na Kenya Kwanza kuhusu nyadhifa za uongozi. Maelezo zaidi yatatolewa leo,” akasema mmoja wa viongozi wakuu wa Azimio bungeni.

Katika Seneti wandani wa Bw Gachagua waliotimuliwa wiki jana kwenye kamati mbalimbali ni Joe Nyutu (Murang’a), Karungo wa Thang’wa (Kiambu), James Murango (Kirinyaga), John Methu (Nyandarua) na Kanar Seki (Kajiado).

Wiki jana Bw Mohamed alisema wataanza mchakato wa kumbandua Bw Wetangúla kwa kukiuka amri ya korti lakini mkutano wa Jumatatu ulizima tofauti hizo.

Mnamo Jumatatu Karani wa Bunge la Kitaifa Samuel Njoroge Vuguvugu la Grassroot Oversight ambalo liliwasilisha ombi la kutaka Bw Wetangúla abanduliwe, halikufuata sheria.

Alisema ombi kama hilo linastahili kuwasilishwa kama hoja na mbunge kwa sababu sheria haliruhusu asasi hiyo kujadili mienendo ya spika bila hoja hiyo.