DIMBA: Kinda Jesus hana kifani, aenda mbali
Na GEOFFREY ANENE
Unapowahesabu makinda wanaotoa kila ishara ya siku moja hivi karibuni kuondokea kuwa majabali katika kandanda, basi huwezi, wala hufai, kumsahau raia huyu wa Brazil.
Hakika upevu wake kwenye safu za mbele za Manchester City na Brazil hauna kifani na ndiyo maana miaka miwili iliyopita, ama alishindania namba au alishirikiana na masogora Neymar Jr, Roberto Firmino na Philippe Coutinho kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi.
Mwaka mmoja awali, kocha wa Manchester City Pep Guardiola alikuwa ameyaona ma na kumleta Etihad angali mbichi japo mpevu ajabu.
Gabriel Fernando de Jesus ni mshambuliaji matata wa klabu ya Manchester City inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uingereza.
Kinda huyu, ambaye anasema anachochewa zaidi kisoka na talanta ya jagina Ronaldo Luis Nazario de Lima, alizaliwa Aprili 3 mwaka 1997 katika mji wa Sao Paolo alikoanzia soka yake ya malipo katika klabu ya Palmeiras.
Kifungamimba huyu alikuza kipaji chake kupitia soka ya mitaani akianza kufanya hivyo akiwa na umri wa miaka mitano. Tangu utotoni, alipenda soka ya kasi ambayo anafahamika nayo zaidi.
Alianza soka kama kiungo wa kati, ingawa alivutiwa zaidi na ushambuliaji baada ya Kombe la Dunia 2002 alipotambua na kupendezwa sana na Ronaldo anayekumbukwa kuwa mchana-nyavu matata enzi zake.
Ronaldo alisaidia Brazil kushinda kombe hilo akichangia mabao manane yakliwemo mawili katika fainali dhidi ya Ujerumani.
Baada ya kutetemesha katika timu kadhaa za machipukizi, Jesus alianza kuvutia timu kubwa mjini Sao Paulo alipofuma wavuni magoli 29 akicheza soka isiyo ya malipo katika klabu ya Anhanguera Associacao Paulista katika mashindano ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 15.
Alinyakuliwa na miamba wa Palmeiras kuchezea timu yao ya makinda baada ya kufanyiwa majaribio na kupita.
Jesus hakupoteza muda kujitokeza kuwa tegemeo kwa timu hiyo kiasi cha mashabiki kuitisha apewe nafasi katika timu ya watu wazima ya Palmeiras. Alipata nafasi hiyo na hakusikitisha. Alichangia mabao 12 na kusaidia Palmeiras kutoka maeneo ya kushushwa ngazi na kuwa mabingwa mwaka 2016.
Aling’ara sana msimu huo. Alitawazwa mchezaji bora wa msimu baada ya kusaidia Palmeiras kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 22.
Kila mechi aliyoshiriki, ilivutia maskauti wa timu nyingi duniani.
Licha ya kufahamu kuwa macho yote yalikuwa kwake, Jesus hakuingiwa na kiburi wala kupoteza kumakinikia soka yake.
Baadhi ya mashabiki walimbandika jina Little Neymar kutokana na talanta ya hali ya juu aliyoonyesha sawa na mshambuliaji mwingine matata wa Brazil Neymar anayevumisha katika klabu ya Paris Saint-Germain.
Kwa haraka, Jesus, ambaye alilelewa na mamaye Vera Lucia baada ya babaye Diniz kutelekeza familia yake, alijitokeza kuwa mmoja wa wachezaji shupavu katika historia ya Palmeiras.
Talanta yake ilikosesha klabu nyingi usingizi. Ilisukuma mabwanyenye wa Uingereza Manchester City kumnyakua
Aliandamana na mamaye pamoja na kakaye na marafiki wawili alipowasili nchini Uingereza mwaka 2017.
City ililipa ada ya uhamisho ya Sh4.0 bilioni kupata huduma za Jesus, ambaye alipata mafanikio makubwa katika misimu yake miwili ya kwanza.
Nyota huyu, ambaye hula mshahara wa Sh1.1 bilioni kwa mwaka uwanjani Etihad (Sh23.2 milioni kila wiki), alishinda Ligi Kuu ya Uingereza msimu 2017-2018 alipochangia mabao 13 akiwa mfungaji wa tatu bora katika klabu yake nyuma ya Sergio Aguero (21) na Raheem Sterling (18).
Alikuwa katika kikosi cha City kilichohifadhi ubingwa wa ligi msimu 2018-2019.
Jesus ni mchezaji stadi na hodari katika ushambuliaji.
Anafahamika kwa kasi ya kutisha na uwezo wa kuchana nyavu.
Msimu huu pekee, Jesus amesakata mechi 34 ligini akitikisa nyavu mara 14 na kuchangia pasi nane zilizozalisha magoli.
Mchezaji huyu ana kandarasi na City hadi mwaka 2023.
Ameshiriki mechi saba za Klabu Bingwa Ulaya msimu huu na kufuma wavuni mabao sita.
Yumo mbioni kushinda Klabu Bingwa Ulaya baada ya kuchangia bao la ushindi dhidi ya Real Madrid mnamo Agosti 7 wakati miamba hao wa Uhispania walibanduliwa nje katika raundi ya 16-bora.
Akiwa na umri wa miaka 23 pekee, Jesus tayari ameshachezea Brazil mechi 39 zikiwemo tano kwenye Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi alikotafuta mabao bila mafanikio.