DIMBA MASHINANI: Ndoto yao ya kubeba taji la Maulid yatimia
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
KWA miaka mingi, klabu ya Flamingo FC ya kisiwani Lamu imekuwa na hamu kubwa ya kushinda mashindano maarufu ya kila mwaka ya Maulid Cup.
Miaka saba tangu kuundwa kwa klabu hiyo, imewahi kushinda mashindano mengine karibu yote lakini siyo yale ya Maulid Cup ambayo hufanyika nyakati za kuadhimishwa kwa sherehe kubwa zinazofanyika kisiwani humo za kuzaliwa kwa Mtume Muhammad.
Ni hamu sawa na ile ambayo imekuwa kwa klabu na mashabiki wa Liverpool kushinda mataji yote isipokuwa lile la Ligi Kuu ya Uingereza kwa kipindi cha miaka 30.
Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Ali Katana amesema kuwa wamekuwa na hamu mwaka nenda mwaka rudi kushinda taji hilo la Maulid hadi mwaka huu ndipo wamefanikiwa kuibuka washindi.
“Tumewahi kushinda mataji ya mashindano kadhaa, lakini hamu yetu kubwa ilikuwa nasi tuwemo kwenye kitabu cha kumbukumbu cha timu zilizowahi kubeba kombe la Maulid Cup sababu linashindaniwa wakati muhimu wa sherehe za kuzaliwa kwa Mtume Muhammad.
“Tumekuwa na hamu hiyo sababu wakati huo waumini kutoka pande zote duniani hufika kisiwani kuhudhuria sherehe hizo. Tunashukuru mwaka huu tumeibuka washindi na nina imani kubwa tutaweza kulihifadhi taji mwaka ujao,” akasema Katana.
Alisema yeye pamoja na naibu wake Kahindi Pillo na meneja wa timu Pascal Yeri watajitahidi kuisimamia timu kuhakikisha taji hilo haliwatoki tena kwani kwa miaka saba wamekuwa wakibanduliwa nje.
Katana alisema wanasoka wake walipania kuhakikisha taji hilo wamelibeba kwani walijitayarisha mapema kwa mazoezi na akawapongeza kwa juhudi za kuweka historia ya klabu yao.
Alikitaja kikosi kilichofanikiwa kushinda kombe hilo la Maulid kikiongozwa na nahodha wake Henry Shukrani kuwa na Omar Chengo, Brian Karisa, Josphat Ziro, Adam Abdalla, Deche Sonje na Joseph Marui.
Wengine ni Michael Yanga, Hamza Barofa, Mwandeje Kalama, Willy Tsuma, Gideon Randu, Bongo Kaingu, Daniel Mangi, Omari Amira, Okiri Owino, Afro Charo, Baraka Chengo, Julius Kalume, Kadenge Shariff na Said Lewa.
Nahodha Shukrani anasema wana nia kubwa kuhakikisha wanashiriki Ligi ya Kaunti ya Lamu lakini wanahitaji udhamini utakaowawezesha kugharamia safari na mahitaji mengine muhimu.