• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
DINI: Krismasi ni somo la kupanga ya kesho

DINI: Krismasi ni somo la kupanga ya kesho

Na FAUSTIN KAMUGISHA

MATUMIZI ya Krismasi huacha mifuko ya pesa ya watu imesinyaa kila mwaka.

Lakini ukweli ni kuwa Krismasi ni somo la mpango mkakati. Krismasi haitokei kama dharura.

Inajulikana kuwa kila tarehe 25 Desemba ni Sherehe ya Kuzaliwa Bwana Wetu Yesu Kristo.

Krismasi inatufundisha kuwa Mungu wetu ni Mungu wa mipango. Hakurupuki, habahatishi na hachezi bahati nasibu.

Alipanga juu ya kuzaliwa mkombozi. Alipanga juu ya siku na saa ya kuzaliwa mkombozi.

Ulikuwa ni mpango wa muda mrefu na mpango mkakati wa kumkomboa mwanadamu.

Maishani usipofikiria juu ya kesho, huwezi kuwa nayo.Maisha ni kupanga.

Isaya alitabiri, “Tazama, bikira atachakua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli” (Isaya 7:14).

Katika maneno hayo mapokeo ya Kanisa yanaona tangazo la fumbo juu ya uzazi wa Yesu Kristo.

Utabiiri huu ulitolewa 736-700 K.K. K.K. ni ufupisho wa Kabla ya Kristo. Kuna aliyesema, “Mungu kila mara ana kitu kwa ajili yako, ufunguo wa kila tatizo, mwanga kwa kila kivuli, faraja kwa kila huzuni na mpango kwa kila kesho,” Ndugu msomaji kuwa na mpango wa kila kesho.

Kuwa na mpango wa kila mwaka. Kuna kampuni yenye mpango wa miaka 100 kwa nini usiwe na mpango walau wa miaka kumi.

“Usifanye mipango midogo; haina ‘uchawi’ wa kusisimua damu ya watu,” alisema Daniel Burnham.

Mpango wa ukombozi wa mwanadamu ni mpango mkubwa sana.

Ulisisimua damu ya Yesu. Ulisisimua damu ya mitume wake. Mipango uliyo nayo je, inasisimua damu yako?

Mkakati ni chaguo zuri sana. Mungu alijifanya mtu. Kuna mkristo mmoja haliacha kusali na halikuwa haelewi ni namna gani Mungu anaweza kujifanya mtu.

Siku ya Krismasi hakwenda kanisani kusali.

Mvua ilinyesha sana. Kuku wake walikuwa nje lakini walinyeshewa mvua sana.

Alitaka kuwapeleka bandani hawakuelewa.

Alijiambia, “Ningekuwa na uwezo wa kuwa kama kuku nikaongea lugha yao wangenielewa. Ningewasaidia.” Tafakari hiyo ikampeleka Krismasi na akatafakari kwa nini Mungu alipata mwili akazaliwa na kukaa na sisi ili kutukomboa.

Somo linguine la Krismasi ni kuwa popote ng’aa. Hata kama umezungukwa na wabezaji ng’aa. Yesu alizaliwa horini. Yesu alizaliwa pangoni amezungukwa na wanyama kama ng’ombe na punda.

“Mtoto Yesu anapata joto toka kwa ng’ombe na punda; ng’ombe ni alama ya bidii katika kazi; kukubali kubezwa hata pale tunapofanya kazi njema, kunawakilishwa na huyu punda ambaye hufanya kazi lakini hakuna anayemjali” (Mt. Gaspari del Bufalo).

Kuna methali ya Tanzania isemayo, “asiyeweza naye hudharau.”

Hata kama unadharauliwa na wasioweza endelea kung’aa.

“Mbezaji ni mtu anayejua njia lakini hawezi kuendesha gari,” alisema Kenneth Tynan.

Hata kama uko horini ng’aa. Shimoni ng’aa. Kwenye makazi mabaya ng’aa. Dhahabu inang’aa shimoni. Kuna methali ya Tanzania isemayo, “Jiwe dogo walilitupa majini likasema, Yote makazi.” Yesu alizaliwa horini lakini aling’aa.

“Anafungiwa mahali padogo pa hori baya, ambaye kiti chake kilikuwa mbinguni, ili atupe chumba cha kutosha katika furaha za ufalme wa mbinguni. Yeye ambaye ni mkate wa mbinguni analazwa horini, ili atushibishe kama wanyama walivyokuwa wanashibishwa,” alisema Baba wa Kanisa Bede.

“Pasingekuwepo na msalaba, pansingekuwepo na hori; pasingekuwepo na misumari, pasingekuwepo na nyasi” (Askofu Fulton Sheen).

Lakini baada ya dhiki faraja, penye msalaba kuna utukufu, penye misumari kuna neema.

You can share this post!

Tuju aonya viongozi fisadi ndani ya Jubilee

Ipo njama ya kuzima Ruto 2022

adminleo