DINI: Mazoea mabaya yakipata mizizi si rahisi kuyang’oa, dawa ni kuyazuia
NA FAUSTIN KAMUGISHA
MAZOEA ni mtihani.
Mwanzoni mazoea ni kama utando wa buibui baadaye ni kama nyaya ngumu.
Mwanzoni mazoea ni kama shati la pamba baadaye ni kama shati lililotengenezwa kwa chuma.
Shati la namna hiyo si rahisi kuchanika. Jambo unalolitenda kila mara na daima lilikuwa mazoea. Kutii sheria linakuwa jambo zuri la mazoea. “Nami nitaitii sharia yako siku zote, daima na milele” (Zaburi 119:44). Kuwa na mazoea ya kutii. Lakini kuna mazoea hasi kama kutosikia. “Ilikuwa desturi yako tangu ujana wako kutosikia sauti yangu” (Yeremia 22: 21).
Mazoea hasi yakishasimika mizizi si rahisi kuing’oa. Ukweli huu ulibainishwa na Samuel Johnson kwa maneno mengine, “Minyororo ya mazoea ni hafifu kuweza kuhisi mpaka inapokuwa na nguvu sana kiasi cha kutovunjwa.”
Dawa ya mazoea mabaya ni kuyazuia kabla hayajashika kasi na kuwa na nguvu. “Mazoea yasipozuiliwa, muda mfupi yanakuwa ya lazima,” alisema Mt. Augustino wa Hippo Afrika ya Kaskazini. “Jambo ambalo ni bahati mbaya katika dunia hii ni kwamba mazoea mazuri ni rahisi zaidi kuyaacha kuliko mazoea mabaya,” alisema W. Somerset Maugham. Mazoea ni jambo linalofanywa kila mara kiasi cha kujenga mwenendo uliozoeleka. Mazoea ni kawaida. Mazoea ni desturi.
Mazoea ni mlango wa sita wa fahamu unaotawala mingine mitano (Methali ya Uarabuni). Mazoea yatatawala kuona kwako. Unachoona huenda si kizuri, kitaonekana kizuri kwa sababu umekizoea. Mbwa akicheza sana na mfupa baadaye anaula. Kwa kila kitu kuna mara ya kwanza. Mara ya kwanza ikirudiwa rudiwa, inakuwa mara ya pili, mara ya tatu na kuendelea, mazoea yanazaliwa.
Kuna baadhi ya watu wakisikia neno mazoea wanakuwa na mtazamo hasi wa mambo kama uvivu, ulevi, umbeya. Lakini kuna mazoea mazuri kama ya uchapakazi, huruma, mafanikio kutaja machache. Mazoea mazuri ni siri ya mafanikio.
“Mazoea ni watumishi wazuri au ni mabwana wabaya,” alisema Nathaniel Emmons.
Mazoea yasikutawale. Njia nzuri ya kuwa na mazoea mazuri ni kuanza na kuyarudiarudia. Mfano, kurudiarudia ni mama wa kusoma. Mwanafunzi akirudia jambo mara nyingi linaingia vizuri akilini. Akitembelea vitabu vyake na daftari zake mara nyingi, kilichomo kitaingia vizuri akilini. Ni kama ukitembelea jiji la Dar es salaam mara mia moja, unakuwa na picha ya jiji akilini.
Anayeshiriki mashindano ya kukimbia mbio lazima kufanya kila mara mazoezi ya kukimbia mpaka kukimbia kuwe mazoea au desturi. Anayejifunza lugha ngeni lazima kuzungumza lugha hiyo kira mara, vinginevyo atasahau msamiati.
“Tunakuwa kile ambacho tunakifanya kila mara. Hivyo ubora si tendo bali mazoea,” allisema mwanafalsafa Aristotle ( 384-322KK). Jiulize, jambo gani nalifanya kila mara? Kwenye mashindano ya michezo, nia njema haitoshi kabla ya mashindano lazima uwe na nia ya kufanya mazoezi. Mchezaji kinanda anatakiwa kufanya mazoezi kila siku walau saa zaidi ya nne kila siku.
Kuanza
Mazoea mabaya yanaanza kama ugonjwa usioumiza.
“Mazoea mabaya ni kama vitanda vizuri- rahisi kulala kwenye vitanda hivyo lakini vigumu kuamka,” alisema Watson C. Black.
Mwalimu mzee na mwanafunzi walikuwa wanatembea kwenye msitu. Mwalimu alisimama na kumwonyesha mwanafunzi miti minne. Wa kwanza ulikuwa unaanza kuchipuka. Wa pili ulikuwa umeanza kuzamisha mizizi ndani ya ardhi.
Wa tatu ulikuwa mti mdogo. Wan ne ulikuwa mti mkubwa. Mwalimu alimwambia mwanafunzi kuing’oa miti hiyo. Mwanafunzi alijaribu. Wa kwanza ulikuwa rahisi kuong’olewa.
Wa pili ulikuwa ni kazi kuuong’oa. Wa tatu ulihitajika kazi ya ziada. Wa nne haukuwa rahisi kuung’oa. Mwalimu alimwambia mwanafunzi, “Hayo ni kama matokeo ya mazoea yetu mabaya. Yakiwa bado yanaanza ni rahisi kuyafutilia mbali, lakini yakishakomaa ni vigumu sana kuyafutilia mbali.” Heri kuzuia kuliko kuponya.
“Chunga mawazo yako; yanageuka maneno. Chunga maneno yako; yanageuka matendo. Chunga matendo; yanageuka mazoea. Chunga mazoea; yanageuka tabia. Chunga tabia yako inageuka hatima yako,” alishauri Frank Outlaw.