Makala

DINI: Ni vyema kufanya mambo kwa vipimo, usipunguze na usizidishe

December 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

KUNA methali za kiafrika zinazogusia kuwa usizidishe: Wamekusifu kuwa wewe ni mkimbiaji mzuri umepita kwenu.

Wamekusifia kuwa wewe ni mpishi mzuri umelamba kijiko. Katika maisha ya kiroho usizidishe, usiongeze.

Tunapojiandalia Krismasi, tunasoma katika Biblia.“Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake. Kila bonde litafukiwa, na kila mlima na kilima vitasawazishwa. Njia zilizopotoka zitanyoshwa, na njia za kukwaruza zitalainishwa, na kila kiumbe kitauona wokovu wa Mungu” (Luka 3: 4-5).”

Ukipunguza ukarimu unakuwa uchoyo. Ukizidisha ukarimu unakuwa kutapanya ovyo. Ukipunguza unyenyekevu unakuwa majivuno, ukizidisha unyenyekevu unakuwa kujidhalilisha.

Juu ya kifungu cha Biblia Baba wa Kanisa Gregori alikuwa na haya ya kusema, “Anaamrisha mabonde yafukiwe, vilima na milima kusawazishwa, kuonesha kuwa kanuni ya fadhila haipungukiwi uzuri na wala haivuki na kupita kiasi.”

Bonde na milima vinaonyesha kuzidisha na kuharibu fadhila ama kupunguza na kuharibu fadhila. Kiasi ni tambarare. Ulevi ni bonde. Ulevi ni kupunguza upande wa kiasi. Ukizidisha kiasi ni kuharibu afya.

Usipunguze unyenyekevu, usizidishe unyenyekevu. Somo la unyenyekevu tunalipata toka mahali pengi. Nyota hazilifuniki jua. Nyota hazishindani na mwanga wa jua. Nyota zinatupa somo la unyenyekevu.

“Unyenyekevu unamaanisha mambo mawili. Kwanza, ni uwezo wa kujikosoa. Sifa ya pili ni kuwaruhusu wengine wang’ae, kuwakubali wengine, kuwawezesha na kuwafanya wawe na uwezo,” alisema Cornel West mwanafalsafa wa Amerika aliyezaliwa 1953.

Kama ambavyo huwezi kuzuia nyota zising’ae hauwezi kuzuiwa using’ae ingawa unaweza kucheleweshwa.

Usipunguze unyenyekevu, usizidishe unyenyekevu. Juu ya ujasiri Nelson Mandela alikuwa na haya ya kusema: “Nimejifunza maishani kwamba ujasiri maana yake si ukosefu wa woga; bali ni ushindi dhidi ya woga, na kwamba shujaa si yule ambaye hana woga; bali ni yule anayeushinda woga.”

Kwa shujaa huenda kilio, kwa mwoga huenda kicheko. Usipunguze, usiongeze.

Usipunguze ukarimu, usizidishe.Unaweza kutoa bila kupenda lakini hauwezi kupenda bila kutoa,” alisema, Robert Louis Stevenson.

Kusema kweli maneno kwenye kanga au leso za wanawake yanasema, yote. Kula unibakizie. Ni ukarimu kuwabakizia wengine. Uchoyo ni chanzo cha kuzika haki. Uchoyo hauna malipo.

Usipunguze busara wala usizidishe busara. Ukipunguza busara unapata upumbavu. Ukizidisha busara unapata ulaghai.

Tunapotengeneza njia ya Bwana tumuombe Mungu atujalie neema ya kutokuwa kama gari la caterpillar ambalo hutengeneza barabara na halitumii kamwe barabara hiyo. Likifika mwishoni wakati wa kurudi linabebwa kwenye gari jingine.

Tujue kuwa Kristu ni Njia: Njia ya Kristu ni ndefu, nyembamba na yenye vikwazo. Njia ya shetani ni fupi, pana na ya mteremko haina vikwazo. Tuachane na visingizio.

Visingizio havisaidii katika kukuwepa kutenda mema. Kuna mtu ambaye alikuwa haogi kwa muda wa miezi sita alitoa visingizio kumi. Moja, nililazimishwa kuoga nikiwa mtoto.

Mbili, watu wanaoga ni wanafiki wanafikiri wao ni wasafi kuzidi wengine. Tatu, kuna aina nyingi za sabuni, sikuweza kamwe kuamua ni ipi nitumie. Nne, Nilizoea kuoga lakini ilinichosha.

Tano, naoga wakati wa Krismasi na Pasaka tu.

Sita, Hakuna rafiki yangu anayeoga. Saba, nitaanza kuoga nitakapozeeka. Nane, sina muda. Tisa, chumba cha kuoga ni baridi. Kumi, naweza kuteleza nikavunja uti wa mgongo bafuni.

Katika kutengeneza njia ya Bwana Yesu visingizio havisaidii ni kukwepa ukweli.

Visingizio kama hakuna pesa ya kufunga ndoa. Watoto wako shule za Kiingereza hawawezi kujifunza katekisimu ili kuweza kukomunika.