DINI: Ukitaka kufanikiwa katika hatua zako maishani, lazima uweke maombi mbele
NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA
Sala haimbadili Mungu, inakubadilisha wewe. Mungu atabaki kuitwa Mungu. Kwa binadamu, kila anapotaka kufanya mbadiliko maishani, lazima asali.
Mtoto wa miaka minne aliona picha ya Yesu akisali, akauliza kuhusu alichokuwa anafanya Yesu katika picha hiyo.
Aliambiwa kuwa Yesu Kristo alikuwa anasali. Mtoto alizidi kuuliza, “Anasali kwa nani?” Alijibiwa, “Anasali kwa Mungu Baba”.
Mtakatifu Cypriani alisema, “Kama alisali yeye ambaye hakuwa na dhambi, basi mwenye dhambi hana budi kusali zaidi.”
Tunasoma katika Biblia, “Yesu aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu” (Luka 6:12).
Mwinjilisti Luka anaeleza kwamba Yesu alikuwa akisali katika matukio muhimu au kabla ya kufanya maamuzi mazito.
Uteuzi wa mitume kumi na wawili ulifanyika baada ya Yesu kusali usiku kucha. Musa pia alitumia mtindo kama huu.
Alisali mlimani akipokea maelekezo kuhusu wasaidizi (Kutuko 19: 24) na warithi (Hesabu 27: 15-23) wake. “Kanuni ya sala ni kanuni ya mavuno. Ukipanda haba katika sala, utavuna haba. Ukipanda kwa wingi katika sala utavuna kwa wingi.
“Tatizo ni kuwa, tunajikaza sana kupata kuvuna kutoka juhudi zetu kitu ambacho hatukupanda,” alisema Leonard Ravenhill.
Yeye ambaye amejifunza kusali amejifunza siri ya mafanikio. Ukiona mafanikio yoyote maishani mwa Mkristo, kuna magoti yaliyopigwa.
“Sala inapanua moyo wazi na kukuwezesha kubeba zawadi ya Mungu mwenyewe,” alisema Mt. Mama Teresa Calcutta. Tumuige Bwana wetu Yesu Kristo katika kusali. Tunahitaji kupata nguvu kutoka kwa Mungu kwa ajili ya maisha yetu ya kila siku.
Nguvu hizo zinakuja tu kupitia maombi. Kila hatua iwepo dua.Unapotaka kufanikiwa, kwenda kanisani iwe desturi.
Ombi hili lilionekana katika gazeti la parokia ya Kanisa la Mt. Charles, Uingereza: “Ulipozaliwa, wazazi wako walikuleta kanisani. Ulipooa, mwenzi wako alikuleta Kanisani. Ukiaga dunia, jamaa zako watakuleta kanisani. Huwezi kujaribu kujileta sasa?” Tendo la kwenda kanisani liwe kama kawaida.
Yesu alikuwa na desturi ya kwenda kanisani. Tunasoma hivi katika Biblia, “Yesu alienda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya Sabato akaingia katika Sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake” (Luka 4: 16).
Kawaida ni kama sheria. Ukizoea si rahisi kuacha. Desturi ya Yesu ya kwenda kuabudu kila mara ndiyo siri yake ya mafanikio na mfano kwetu sisi wanafunzi wake.
“Mahali pa kila Mkristo ni kanisa…kushiriki katika ibada, ushirika wake na ushuhuda,” alisema John R. W. Stott.Yesu alipopotea wazazi wake walimtafuta Hekaluni.
Tunaambiwa: “walimkuta hekaluni” (Luka 2:46). Naye aliwaambia: “Kwa nini mmenitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?” (Luka 2: 49).
Mara nyingi Yesu alitumia neno “imenipasa.” Inatupasa kuwa katika nyumba ya Baba. Tuwe tunapatikana katika nyumba ya Baba.
Tusimfanye padre arejelee mstari huu kila mara: “Walipo wawili au watatu, nipo kati yao.” Usikose kuhudhuria ibada kanisani kwa sababu wewe ni maskini. Hakuna kiingilio.
Usikose kwenda kanisani kwa sababu mvua inanyesha. Mbona wakati mwingine unaenda kupanda basi kwenda kazini wakati kunanyesha, wala hutoi vijisababu.
Usikose kwenda kanisani kwa sababu nguo zako si za gharama. Kanisani si mahali pa kuonyeshea mitindo ya mavazi.
Usikose kwenda kwa ibada ya kanisa kwa sababu hujaalikwa. Mbona watu huenda kwa mazishi ilhali huwa hawajaalikwa.
Kama unataka kufanikiwa, basi kwenda kanisani iwe kama kawaida. Kuna ambaye alikuwa anasema kuwa haendi kanisani kila siku kwa sababu ibada ni ndefu.
Ibada sio ndefu bali ni uvumilivu wake ulikuwa mfupi. Kabla kila hatua ya maisha piga dua kwanza. Unataka kuanza shule, piga dua.
Unataka kuchumbia, piga dua. Ungependa kufunga ndoa, piga dua.