Makala

DINI: Watu wanaangamia kwa kukosa maono, yakujuzu upange maisha

July 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na FAUSTIN KAMUGISHA

KUTEKELEZA maono ni mtihani.

Maono ni kuona ambacho hakionekani. Maono ni ndoto kujumlisha na uhalisia.

Biblia yasema, “Pasipo maono watu huangamia” (Mithali 29: 18). Biblia haisemi, pasipo pesa au fedha watu huangamia.

Biblia haisemi, pasipo chakula watu huangamia, bali pasipo maono watu huangamia.

Kuna aliyesema, “Mtu bila maono ni mtu bila wakati ujao. Mtu bila wakati ujao atageukia wakati uliopita.” Atausifia wakati uliopita. Kuna wajenzi watatu waliokuwa wanajenga ukuta. Mpita-njia alimuuliza wa kwanza, mnafanya nini? Alijibu, “tunapanga tofari.”

Alimuuliza wa pili, mnafanya nini? Alijibu, tunajenga ukuta. Alimuuliza wa tatu, wa tatu akasema, “mnafanya nini.” Akajibu, “tunajenga benki.”

Wa kwanza hakuwa na maono. Kuna watu wanafanya shughuli ni kama wanapanga tofari.

Hawana maono. Hawajui lengo la shughuli ni lipi. Wa pili naye hakuwa na maono, alifikiria ukuta badala ya benki. Wa tatu alikuwa na maono. Maono ni mtihani.

Kuna hatua tano za kutekeleza maono yawe ya kuanzisha shirika, kampuni, taasisi, au ya maendeleo ya mtu binafsi.

Hatua hizi zimetumiwa na baadhi ya makampuni ya kutengeneza magari ya Japan.

Kwanza ni kuchambua. Simba akizidiwa hula nyasi, lakini anachambua asile miiba. Hii ni hatua ya kuchambua watu sahihi unaowahitaji.

Usipochukua mtu sahihi, rasilimali sahihi, vitendea-kazi sahihi, vifaa sahihi, utanoa.

Hata kwenye ndoa mtu asipochukua mtu sahihi atonoa badala ya kuoa au atazolewa badala ya kuolewa.

Kama ni kutengeneza gari, yanachambuliwa madini yanayohitajika na vifaa vinavyohitajika.

Ukitaka kuvua kama maono yako unahitaji kuchambua unavyohitaji: mtumbwi, nyavu, chambo, kutaja machache tu.

Ukitaka kuelemisha watu kama maono yako, utahitaji majengo (madarasa), walimu, wanafunzi, vitabu. Na hapa utachambua. Si kila kitabu utakihitaji.

Hatua ya pili ni kuweka miundo-mbinu na kujenga. Ni hatua ya kuweka mazingira sawa.

Ni hatua ya kuandaa jukwaa na kujenga.

Katika hatua hii unatumia busara ya fundi cherehani; pima mara mbili kata mara moja.

Hapa unajenga msingi mzuri. Ni hatua ya kujenga na kupanda. Hapa unaunganisha pointi. Unatumia vizuri nguvu ulizo nazo. Ni hatua ya kupanda mbegu ya maono, ikaota na kukua.

Hatua ya tatu ni hatua ya kung’aa. Sasa maono yanaonekana. Kampuni inakuwepo, taasisi imeanzishwa, ndoa imefungwa, shule imejengwa, nyumba imejengwa, gari toleo jipya liko barabarani.

Usione vyaelea vimeundwa. Hapa sifa zinatolewa kwa hatua iliyofikiwa. Mchumia juani hulia kivulini. Baada ya dhiki faraja.

Hapa kuna mafanikio. Katika hatua hii mtume Paulo alisema, “Nimevipiga vita vilivyo vizuri…” (2 Timotheo 4: 6-8).

Hatua ya nne ni ya kuweka viwango na masharti. Ni kuweka utambulisho sawa. Kwa mshangao na kutoa sifa watu watahitaji kujifunza kutoka kwako. Lazima kuweka viwango, kanuni, masharti.

Lazima kuwafundisha watu kutokana na uzoefu wako. Dunia ni kijiji, tunajifunza kutoka kwa watu wengine.

Ni rahisi kujifunza kitu kutoka kwa mwingine kikiwa na viwango. Jungu kuu halikosi ukoko.

Hatua ya tano ni hatua ya kuendeleza. Hii ni hatua ya uthabiti.

Hiki ni kipimo cha uaminifu kwa maono. Juu ya uthabiti, Mtume Paulo anatushauri, “Tupige mbio kwa uthabiti katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu,” (Waebrania 12:1).

Kipimo

Maono lazima yapitie kipimo sahihi kabisa, kile cha muda wote.

Hivyo, hatua ya tano ya kutekeleza maono ni kutobadilika (uthabiti).

Ni rahisi kuwa thabiti kwa siku moja au mbili.

Ni vigumu kuchukua wembe ule ule kwa maisha yako yote.

Ni rahisi kuwa na uthabiti katika wakati wa shauku, si vigumu kuwa hivyo wakati wa taabu.

Ni kufanya maono yaliyotekelezwa yadumu.

Ni hatua ya mwendelezo wa chema. Chema chajiuza, kibaya chajitembeza.