DOMO KAYA: Koffi ashaomba radhi jamani, tuache unafiki
Na MWANAMIPASHO
WIKENDI iliyopita mfalme wa muziki wa rhumba Koffi Olomide alitua nchini baada ya marufuku yake ya kutokanyaga Kenya kufutiliwa mbali na serikali. Nataka kuamini ilifutiliwa mbali baada ya kuomba msamaha.
Lakini ni msamaha uliosubiriwa kwa miaka minne kukubaliwa. Koffi tofauti na zile mbwembwe zake, alitua katika uwnaja wa ndege wa JKIA kimya kimya. Uwanja ambao hana kumbukumbu nzuri nao. Ni katika uwanja huo wa ndege Julai 2016 alijiweka kwenye mashaka na serikali baada ya kunaswa kwenye kamera akimtandika teke dansa wake wa kike.
Ni kisanga kilichotafsiriwa kuwa udhalilishaji wa wanawake na kuwapelekea watu wengi kupiga kampeni kubwa mtandaoni ya kumtaka afurushwe nchini. Ndicho kilichotokea. Lakini licha ya kuomba msamaha hakuna aliyetaka kumsikiza na Koffi akaamua kuwatumia mawakili kumtetea na hatimaye alifaulu.
Jumapili iliyopita alipotua nchini, alikuja kupima hali tu kuona ikiwa kila kitu kipo sawa. Na hakika akapata kweli serikali imemwondolea marufuku hiyo. Alitua kwenye Siku ya Wanawake Duniani na pengine kwa kuhofia kutonesha kidonda, ndio sababu aliamua kuingia kimya kimya ijapokuwa sio mgeni Kenya. Kaja huku zaidi ya mara 25.
Siku tatu kabla ya kuabiri ndege kuja +254, Koffi aliposti ujumbe wa video kwenye Facebook akiwafahamisha mashabiki wake wa hapa Kenya kwamba atakuwa akirejea nchini baada ya serikali kumwondolea marufuku. Kila mtu alikuwa kimya na pengine walidhani anatania.
Ila Jumapili taarifa zilipoanza kuzangaa kwamba Koffi yupo nchini, ghafla kelele za kupinga kuondolea kwa marufuku hiyo zikaanza.
Mtandaoni watu wengi hasa jinsia ya kike walikesha wakikashifu kuruhusiwa kuingia kwake nchini wakiongozwa na mwanasiasa Martha Karua.
Kinachonichekesha ni jinsi Wakenya walivyo wanafiki. Hivi tulisubiri mpaka aje ndio tuanze kelele. Alipoposti video ile akisema anarejea mbona hatukunung’unika na kulalamika wakati huo? Kinachonichekesha hata zaidi ni hili, wengi wa hao wanaomchamba ni mashabiki wake wakubwa.
Nilipoposti picha yangu na Koffi mitandaoni, kila mmoja alianza kuni DM akiomba tiketi. Wengine ni watu ninaokumbuka kabisa wakimkashifu. Ila waliposikia shoo yake ipo Mei ghafla wakasahau kisanga kile.
Nisionekane namtetea jamani. Kosa lilitendeka, alichokifanya sio kitu cha kusifia. Mamangu ameniambia mara mia mwanamke hapigwi, bora hata umfukuze bila ya kumwekelea mkono. Itakuwa Koffi hakufunzwa na kama alifunzwa basi kasahau. Kilichonivutia mimi zaidi ni ule msamaha ambao kautoa zaidi ya mara mia na, lakini bado tunakausha.
Hivi ni nani asiyekosea. Hata Papa Francis namkumbuka akimpiga mtu mkono alipomvuta amsalimie. Baadaye aliomba msamaha. Makosa ni sehemu ya maisha yetu, hivyo tunapojigeuza wanafiki kwa dizaini hii, inakuwa sio vizuri. Koffi kaomba msamaha jamani, tumsameheni na kama akirudia basi tutajua la kufanya. Naamini marufuku ya miaka minne ilikuwa funzo kwake.