• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 2:24 PM
DOMO KAYA: Mageuzi au twapotoka?

DOMO KAYA: Mageuzi au twapotoka?

Na MWANAMIPASHO

“HAO madem wasimame au wainamee…aaah wee wainame…hao mangoes wasimame au wainamee..aah wee wainame…”

Usidhani nimepagawa, hapana, kichwa changu ni kizima kabisa.

Huo ni mshororo tu kwenye ‘hook’ ya wimbo mpya wao Sailors uitwao Wainame.Hawa Sailors ndio waliokuletea ule Wamlambez. Na ndio tu wahusika walioibuka na Pekejeng.

Mpaka hapo sijui umegundua nini ila nitakuambia kitu. Hii ndio staili mpya ya muziki uliovuma ndani ya +254. Tayari staili hii ishapewa jina na sasa inafahamika kama ‘Gengetone’.

Kikweli nafurahia kuona mageuzi yaliyoletwa na muziki wa Gengetone ambao sasa ndio unashabikiwa sana. Wasanii wanaofanya staili hii kama vile Ethic watunzi wa Lamba Lolo, Ochunglo Family waliokutungia Krimino, ukiniuliza umri wao utakuwa kati ya miaka 20 hadi 25. Hiki ndicho kizazi cha Gengetone.

Mojawapo ya mageuzi makubwa yaliyonikosha mimi kutokana na ujio wao ni kwamba wamefanikiwa kuangamiza kabisa utawala wa muziki wa Nigeria na Bongo Flava katika mawimbi yetu na chati zetu. Siku hizi utakatiza mjini bila kusikia muziki wa Bongo Flava au Nigeria ukirindima. Kama hutasikia Wamlambez, basi itakuwa ni Pekejeng.

Hata hivyo masikitiko yangu makubwa yapo kwenye staili hii ya Gengetone. Ni staili ya muziki mchafu, usio na maudhui, usioelimisha, unaoendekeza uasherati, ngono na matumizi ya dawa za kulevya. Gengetone sio muziki unaoweza ukasikiza na mamako au mwanao. Hebu jichoree picha pale ukiwa umetulia sebuleni na mamako mzazi mkitia stori za kimaisha kisha video ya Wainame ichezwe. Itakuwa ni aibu tupu.

Kinachonipasua moyo hata zaidi ni kuwa, utunzi huu unafanywa na wasanii wadogo kiumri ambao hawana ukomavu wa kimaisha.

Akili zao haziwazii maendeleo, zinawazia tu ngono. Nyongo yangu hukorogeka hata zaidi unapozitizama video zile.

Zinaweza kukutia kichefuchefu hasa kama wewe ni mzazi wa wana hasa mabinti. Wanaotumiwa kwenye video zile ni mabinti wachanga mno. Kazi yao kwenye video zile ni kutingisha misambwanda yao ambayo kutokana na umri wao mdogo bado haijaimarika na kuwa kama ile ya Vera pengine.

Huwa naumia sana kuona vijana wachanga wanavyoshabikia nyimbo hizi. Akilini huwa namwaza mwanangu anayekuwa. Kwa nyimbo hizi itakuweje?

Ni hapa ndipo mara nyingi najikuta nikikubaliana na misimamo mikali yake Dkt Ezekiel Mutua katika kuzipinga. Tatizo langu naye ni kuwa, anazungumza sana kuliko utendaji. Hawa madogo wanastahili kutiwa adabu. Waruhusiwe kukuza vipaji vyao ila kwa tungo zenye heshima.

Wakati mwingine huwa natamani tungelikuwa na BASATA Kenya, hizi tungo za ngono zingepata taabu sana. Ila kwa kuwa Wakenya ni wastaarabu sana, tunaishia kuruhusu mmomonyoko wa maadili. Wainame tayari umevutia ‘views’ zaidi ya laki tatu ndani ya siku mbili toka ulipoachiwa. Hii inakuambia nini?

Hakika Mutua anacho kibarua kikubwa cha kufanya kuusafisha huu muziki mchafu wa Gengetone. Na kama kazi inamlemea, basi ukiniuliza mimi, ningependekeza tumpe Pasta Ng’ang’a awafunge ‘huto tuvitu twao’.

  • Tags

You can share this post!

UFUGAJI: Usagaji wa majani unaepushia mifugo athari za...

KASHESHE: Burna Boy amwaga povu kali

adminleo