Makala

DOMO KAYA: Zari, mbona hivi?

October 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANAMIPASHO

KUNA ‘kataarifa’ ambako kamenichekesha kidogo.

Eti yule soshiolaiti wa Uganda aliyeachiwa mali kama yote kule Sauzi na aliyekuwa mumewe marehemu Ivan Ssemwanga, kaamua kuitoa rangi Google.

Sasa kosa la Google eti ni kuchapisha taarifa zisizo za kweli kuhusiana na utajiri wake.

Kulingana na meneja wake Galston Anthony, ni kuwa makadirio yaliyochapishwa na Google ni kidogo sana.

Meneja wake anadai utajiri wa bosi wake ni zaidi ya Sh912 milioni zilizochapishwa na Google.

Anthony kadai eti utajiri huo uliochapishwa wa Sh912 milioni haufikii hela alizoingiza Zari 2019.

Kinachonichekesha ni hichi, mwanzo hata mwaka haujaisha, hesabu zake hizo mzee baba kidogo zina mashaka. Lakini hata tukiamua kumwamini, anataka kutuambia eti utajiri wa Zari utakuwa zaidi ya bilioni na senti juu.

Au labda kwa hela za Uganda, hapo sitapingana. Kama mama huyo ni bilionea kweli, basi haiwezekani akawa anakesha mitandaoni kuturingishia nyumba alizonunuliwa na machali wengine. Si bilionea, kuna kitu kinachoweza kumshinda kumiliki?

Sikatai mama wa watu ana utajiri wa kutosha na lazima nisisitize kuwa ni utajiri wa kurithi. Aisee, kuzaa na watu wanaojiweza wakati mwingine ni raha sana manzee. Ila hatua hii ya kutaka kushindana na Google ni sawa na kushindana na tembo kunya. Nani ataweza? Hata Eliud Kipchoge na kauli zake za ‘No human is limited’ hapa hawezani!

Google hadi wanachapisha taarifa kama hizi huwa wamejitahidi sana kuthibitisha hesabu zao kwa stakabadhi zilizopo. Hawafanyi kwa kukisia au kuparamia tu. Lakini ni nani asiyemjua mama huyo mpenda kiki, ukimpa fursa tu, anakunyoosha. Baada ya meneja wake kutema yake, naye Zari akajiongeza akimsifia sana kwa kazi kubwa aliyofanya ya kuwaweka Google sawa.

Mtazamo wangu katika hili ni kwamba kama kweli meneja wa Zari anapania kufanya hivyo kwa niaba ya bosi wake, basi itakuwa ni kusaka kiki tu hakuna lingine.

Huyu mama bwana anapenda kiki si mchezo. Kwa kuzungumziwa tu, yaani bora mkeshe kumchamba, anapenda sana. Ila nilikuja kugundua kuwa mitusi pia humuumiza na hapo ndipo najua kaguswa pabaya hasa ukweli unapoanikwa wakati akiwa amejitahidi kuuficha. Siwezi kumwamini Zari mimi. Mwanamke wa umri wake anayepiga picha zake mpaka akiwa kwenye pool, maji yanapinda kutokana na ‘photoshop’, nitaanzaje kumwamini?

Tena kwa umri wake huo mkubwa wa miaka 38 akiwa anakaribia ‘fourth floor’, huwa nashindwa kumwelea kabisa.Kumfuatilia Zari kwenye Instagram ni raha sana. Mama wa watu anajua kuishi, anaweza akakufanya ukayachukia maisha yako bure kwa jinsi anavyovuruga. Lakini kwa wanaume, unaweza ukayasahau yote anapokuanikia mapacha yake meupe aliyojichubua juu chini, kama tu shogake Vera Sidika.

Ishi kwa amani

Kikweli kwa umri wa Zari, kuna mambo mengine sio ya kushindania, kama Mungu kakuneemesha na kukujalia, basi ishi maisha yako ya starehe kwa amani.

Mashabiki wako wameshakuzoea na kukubali kwamba una hela sasa haja gani kulazimishia sana mengine kama haya ya Google? Mbona asingeliwaandikia barua pepe kina Google kuwataarifu kwamba wamekosea, lazima angelipayuka mitandaoni tu? Mbona akili ndogo? Smh! Haya yote ni kwa faida gani?

Matajiri wengi huishi kwa ukimya ila kwa Zari na utajiri wake huo mdogo wa kutishatisha, ndio hatupumui, sasa mnamwona anataka kuwavembea pia Google. Yule shabiki aliyewahi kumuuliza ni wakati gani yeye hufanya kazi sababu muda mwingi kazi yake ni kuposti picha, nafikiri alishatambua Bi mkubwa ana matatizo. Naogopa kuzeeka kwa staili hii jamani!