Dondoo

Ndoto ya kuogofya yafanya soja amwage unga Kiambu

Na SAMUEL MUIGAI March 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MLINZI wa usiku katika boma moja Kamiti Corner mjini Kiambu alijipata bila ajira baada ya nduru alizopiga akiwa kwemye ndoto kumwamsha bosi wake.

Soja huyo amekuwa mtiifu na mwaminifu na hivyo amefanya kazi katika boma hilo kwa muda mrefu.

Kutokana na hali ngumu ya uchumi nchini, soja alipiga hesabu na kuona ni vyema kuwa anasaka vibarua mchana, kisha kuingia kwa kazi yake ya usoja kila jioni ili aweze kukimu mahitaji yake.

Kutokana na haya, mara nyingi alikuwa anajipata akisinzia kazini juu ya uchovu. Siku ya tukio,soja alifika kazini kama kawaida na alipoona taa zimezimwa kwa nyumba ya mdosi wake, akajilaza kwenye chumba chake karibu na geti.

Haikuchukua muda bila soja kujipata kwenye usingizi mzito. Muda si muda, polo alijipata kwenye ndoto ya kuogofya iliyomfanya apige nduru akijaribu kujinusuru.

Zile nduru zikamwamsha mdosi aliyenyanyuka na kuchungulia nje. Mdosi alipokosa kuona chochote cha kutisha, akaamua kucheza kanda ya CCTV ili ajue kilichotokea.

CCTV pia haikuonyesha tishio lolote ila tu jinsi soja alikuwa anajilaza. Mdosi alikasirika na kwenda kwa soja wake.

“Toka Hapa!! Sikukuajili hapa uje kulala!” bosi alimwambia soja huku akimfukuza usiku wa manane.