Dume wa kilo 690 aliyeuzwa Sh1 milioni ASK Nairobi
DUME mkubwa, wa rangi ya hudhurungi na madoadoa meupe anaondoka kwa madaha kutoka mnada wa uwanja wa maonyesho wa Jamhuri, Nairobi asijue sababu ya watu kumshangilia.
Fahali huyo aina ya Boran, alilelewa na kufugwa na Elgon Downs Farm na aliibuka kidedea katika Maonyesho ya Kimataifa ya Kibiashara Nairobi mwaka huu, 2024, yaliyoandaliwa na Chama cha Kilimo cha Kenya (ASK).
Elgon Downs Farm, ni mradi wa ufugaji katika Gatuzi la Trans Nzoia unaomilikiwa na Kampuni ya Mbegu ya Kenya, maarufu kama Kenya Seed Company (KSC), na dume huyo aliongoza orodha ya mafahali walionadiwa mithili ya dhahabu katika maonyesho hayo ya Makala ya 123.
“Fahali huyu aina ya Boran ndiye ameibuka mshindi kimauzo katika maonyesho ya ASK 2024 Nairobi,” Leonard Kipkosgei, Msimamizi wa Uzalishaji katika mradi huo akaambia Akilimali Dijitali.
Akiwa na uzani wa kilo 690, aliingiza kima cha Sh1 milioni ambapo alinunuliwa na mwanasiasa mashuhuri anayeshikilia wadhifa mkuu serikalini.
Maonyesho hayo yaliyofanyika kati ya Septemba 23 hadi 29, yalivutia watu kutoka ndani na nje ya nchi, wakubwa kwa wadogo wakifurika.
Dume huyo, kulingana na Kipkosgei ana umri wa miaka miwili na nusu.
Amepewa jina ‘Ngirici’, utambulisho wa aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Kike Kirinyaga, Purity Wangui Ngirici ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Kenya Seed.
Huku mafahali wa chotara (cross breed) wakitawala ushindi wa maonyesho ya ASK ya miaka ya awali, Boran huyo halisi alitwaa jukwaa la mwaka huu.
Mwaka 2018, chotara wa Boran na bridi ya Simmental mwenye uzani wa kilo 650 pia kutoka Elgon Downs Farm, aliibuka kidedea akiingiza kima cha Sh650, 000.
Fahali wa pili bora katika ASK 2024 Nairobi ana uzito wa kilo 600, kwa mujibu wa maelezo ya Kipkosgei.
Hata ingawa Kampuni ya Kenya Seed ni maarufu katika uzalishaji wa mbegu, kupitia Elgon Downs Farm inafuga ng’ombe wa nyama (madume) na wale wa maziwa.
Mradi huo unaendelezwa kwenye shamba la ukubwa wa ekari 4,500, Kitale, Trans Nzoia.
Siri ya fahali Ngirici kuibuka mshindi katika utandawazi unaotawaliwa na madume ya chotara ni ipi?
Kipkosgei anafichua kwamba siri ipo kwenye malezi, na zaidi ya yote hatua za kuwafanya wawe wanene.
“Steji za mwishomwisho katika malezi ya ng’ombe wa nyama ni muhimu sana,” anasisitiza.
Anasema malisho bora ya kutamatisha yanasaidia ng’ombe asambaze mafuta yake yawiane au yaingiane sawasawa na nyama.
Elgon Downs Farm imejikita kwenye uzalishaji wa ng’ombe chotara wa bridi asilia na ya kisasa, malisho yakipewa kipau mbele.
Chakula wanachopewa kinajumuisha nyasi za Boma Rhodes, matawi ya mahindi, mtama, hay, desmodium, na malisho yaliyosheheni Protini kama vile mbegu za alizeti, pamba, canola, maharagwe ya soya, kati ya mengine.
“Hujikuzia malisho yetu, kisha tunayapiga jeki kwa virutubisho na madini faafu kwa mifugo,” Kipkosgei anadokeza.
Afisa huyu pia anasisitiza haja ya kusawazisha virutubisho vya Protini na Wanga (carbohydrates) kwa minajili ya ukuaji bora.
Isitoshe, Elgon Downs Farm huhakisha mifugo wanapata maji safi.
Aidha, mradi huo una zaidi ya ng’ombe 600, na katika maonyesho ya ASK 2024 Nairobi mafahali wapatao 40 walinadiwa, wote wakiingiza mapato ya kuridhisha.
Haron Kimutai, vetinari wa mradi huo anafafanua Boran kama spishi na bridi inayostahili maeneo kame na kiwango chake cha malisho ni nafuu.
“Wanahimili mikumbo ya kiangazi na ukame, muradi tu wanapata chakula kiasi na maji,” anaelezea mtaalamu huyo.
Hii inaashiria kuwa wanaishi na kudumu katika maeneo kame (ASAL), bila kujali mazingira.
Boran, anasifiwa kutokana na hulka yake kugeuza chakula upesi kuwa nyama hivyo basi kuwa bridi bora kwa minajili ya ufugaji wa biashara ya nyama.
Kipkosgei anafichua kwamba Elgon Downs Farm ina soko tayari katika mikahawa na hoteli kadhaa Nairobi.
Kilo moja ya mfugohai, inachezea Sh250 hadi Sh400, huku aliyechinjwa akiwa kati ya Sh1, 000 na Sh1, 500 kwa kilo.