• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Eneo ambalo hakuna bucha hata moja, nyama huchinjwa na kuuzwa chini ya mti msituni

Eneo ambalo hakuna bucha hata moja, nyama huchinjwa na kuuzwa chini ya mti msituni

NA OSCAR KAKAI

NI saa nne asubuhi, Jumamosi ndani ya msitu, nyama ya mbuzi inaning’inia juu ya mti huku vijana watatu wenye nguvu wakiikata kwenye vipande kutumia visu vikali.

Hapo, wanaume na wanawake wako tayari kupata nyama. Upande mwingine, vijana wengine wawili wanachoma nyama kwenye meko tayari kuwauzia wateja.

Kwingineko, wazee wakongwe wameketi kwenye viti vya jamii ya Pokot kwa jina (Apolong) wakinusa tumbaku. Mbele yao kuna matawi ya mti wa kienyeji yametandazwa chini kama sahani ambayo nyama itawekwa.

Mkono wa kulia, vijana wengine wameketi wakijitayarisha kula nyama choma.

Eneo hilo hakuna dalili ya nyumba. Kijiji hicho cha eneo la kuchinja na kuuza nyama kwenye msitu ni eneo la Kotulupogh, wadi ya Masol, kaunti ndogo ya Pokot ya kati.

Wadi ya Masol iko kwenye mpaka wa kaunti ya Pokot Magharibi na Turkana umbali wa kilomita mia moja ndani ya Pokot kutoka makao makuu ya kaunti mjini Kapenguria imetelekezwa pakubwa.

Pia, eneo la Kotulupogh liko kilomita 30 kutoka kwenye barabara kuu ya Kitale –Lodwar ambalo halijawahi kuwa na duka la kuuza nyama ama kichinjio. Hii ni kutokana na kiwango cha juu cha umaskini na ukosefu wa maendeleo katika eneo hilo katika eneo hilo ambalo ni vigumu kufikika.

Hata hivo, nyama kutoka kwa mifugo wa eneo hilo ni tamu sana. Haihitaji chumvi sababu ya kuwa na madini ya kiasili.

Athari za wizi wa mifugo na ujangili bado zinaathiri maendeleo na uchumi wa eneo hilo.

Zaidi ya miaka 60 ya uhuru na miaka 12 ya ugatuzi, watu wengi kwenye vijiji vya mashinani katika Kaunti ya Pokot Magharibi hawana maduka ya kisasa ya kuuza nyama ama vichinjio. Wakazi katika eneo hilo bado wanaishi maisha ya kale ya uchochole ambapo nyama huchinjiwa chini ya mti.

Licha ya changamoto hizo zote, eneo hilo la kuuza nyama huvutia watu wengi ambao humiminika kununua nyama.

Baada ya kununua, wengine kubeba bila hata kufunga ama kuweka kwenye mfuko.

Raymond Lotudoreng, mkazi anasema kuwa eneo hilo halina mambo muhimu ya kimsingi.

“Eneo hili halijakuwa na duka la kuuza nyama hata moja. Sisi huchinjia ng’ombe ama mbuzi chini ya mti,”anasema.

Anasema kuwa wakazi hutegemea nyama kama chakula chao cha kila siku, maziwa na damu.

“Nyama huwekwa kwenye matawi ama sufuria baada ya kukatwakatwa. Wakazi hupashwa habari kupitia kwa ujumbe wa mdono ama kupigiwa simu,” anasema.

Anasema kuwa nyama hupimwa na mkono bila kukaguliwa na daktari.

Nyama kukaguliwa

“Hatujui kitu kama nyama kukaguliwa. Sisi hula hivyo. Maisha hapa ni rahisi tena ya chini. Hatujali sana. Mungu hutulinda tu,”anasema.

Mkurugenzi wa matibabu ya mifugo katika Kaunti ya Pokot Magharibi Dkt Samuel Chelimo anaeleza kuwa nyama ya eneo hilo haihitaji chumvi.

“Nyama ya Pokot ni tamu na hutuweki chumvi. Iko na madini ya kiasili na virutubishi,” anasema.

Dkt Chelimo anasema kuwa nyama hiyo ni safi tena ya kuvutia.

“Ni tamu sababu mifugo hula mimea ya kiasili na udongo wa huku ni mwekundu na hufanya nyama kuwa tamu. Haiwezi kulinganishwa na kwingineko. Mbuzi hula miti shamba,”anaeleza.

Muuzaji nyama Lokwakado Lomada anasema kuwa wao huuza nyama ya zaidi ya mbuzi tano kila siku.

“Tuko na ujuzi wa kupima nyama kutumia mikono zetu na macho. Sisi huuza nyama kwa kiwango chochote kulingana na fedha kuanza Sh20. Sisi pia tumebobea kwa kuchoma nyama,” anasema Bw Lokwakado.

Hata hivyo, mkazi Mary Loitangole anasema kuwa kushika nyama ambayo huchinjwa chini ya mti sio salama kwa afya na huchangia magonjwa.

Anasema kuwa changamoto huwa wakati wa kubeba nyama.

“Sijawahi kununua nyama kwenye duka la nyama tangu nizaliwe,” anasema.

Wakazi wa eneo la Masol wanalalamikia kutengwa kwa elimu na hata masuala mengine ya kijamii.

Wanasema kuwa wamesahaulika kwa maendeleo kutokana na visa vya wizi wa mifugo na mizozo na majirani wao.

Mizozo ya mara kwa mara ilipelekea eneo la Masol kusalia nyuma hadi miaka mitano iliyopita ambapo lilianza kufunguliwa baada ya amani kurejea eneo hilo.

Wakazi sasa wanataka maendeleo kufanyika eneo hilo.

Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong anasema kuwa kuna haja ya mpango maalumu wa maendeleo katika eneo hilo sababu ujangili huogofya waekezaji.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mshukiwa wa mauaji alivyotia wakazi hofu kwa kutoa...

Mcheshi Butita atishia kuuza gari kwa kusengenywa eti...

T L