Makala

Eneo la Tusitiri latajwa kuwa ngome ya mapepo katika Bahari Hindi

March 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 4

NA KALUME KAZUNGU

TUSITIRI ni eneo maarufu ambalo wengi wanalifahamu Lamu.

Liko kwenye Bahari Hindi, karibu na ufukwe wa Wiyoni katikati ya Kisiwa cha Lamu na Jeti ya Mokowe.

Eneo hilo lilibandikwa jina ‘Tusitiri’ karibu miaka 20 iliyopita kutokana na kwamba mtalii au mzungu mmoja aliyemiliki mashua kubwa ifahamikayo kwa jina ‘Tusitiri’ alikuwa akiitumia eneo hilo la ufukwe kupakisha chombo chake.

Vyombo vingine vya baharini, yakiwemo maboti madogo pia ya mekuwa yakiegeshwa eneo hilo.

Licha ya jina ‘Tusitiri’ kuwa zuri kwani kwa maelezo ya kimsingi ni sawa na dua ya kumwelekea Mwenyezi Mungu kuwakinga, kuwaficha au kuwafunika waja kutokana na hatari, mambo au kitu cha aibu, hali katika eneo hilo la Tusitiri hata hivyo ni kinyume kabisa.

Eneo hilo limekuwa likitajwa na wengi, hasa mabaharia wakiwemo manahodha wa mashua, wakidai kuwa ni ngome ya mapepo.

Madai yao yanatokana na matukio ya kiajabuajabu, hasa ajali za mashua au maboti baharini ambazo zimekuwa zikiripotiwa eneo hilo la Tusitiri.

Hali hiyo mara nyingi imewaacha wasafiri wakiaga dunia huku nayo mizigo ya mamilioni ya fedha ikizama baharini.

Isitoshe, eneo la Tusitiri pia limeandikisha vituko vya watoto wanaocheza au kuogelea ufukweni kutoweka ghafla katika hali isiyoeleweka na kisha miili yao kupatikana baadaye wakiwa tayari wamefariki.

Kuna nyakati ambapo pia watu hujipata pabaya wakisafiri baharini kwani punde wanapofika katika eneo hilo la Tusitiri huhusika kwa ajali zisizotarajiwa na ambazo kwa wengi waliohojiwa walizihusisha na imani au nguvu za giza.

Mnamo Februari 2020, mwanamke mmoja aliaga dunia baada ya kupigwa na kukatwakatwa na kisahani cha kuzungushia propela ya injini ya mashua walimokuwa wakisafiria eneo hilo la Tusitiri.

Mashua hayo yalikuwa yametoka Jeti ya Mokowe kuelekea kisiwani Lamu yakiwa yamebeba abiria sita pamoja na nahodha.

Punde walipofika Tusitiri, kisahani cha propela ya injini kilichomoka ghafla na kuzunguka hewani huku kikikatakata, kuchinja na kujeruhi vibaya wasafiri.

Mwanamke huyo aliaga dunia alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali kuu ya King Fahad mjini Lamu kwani kisahani hicho cha injini ya mashua kilikuwa kimemsababishia majeraha mbavuni na kifuani.

Wengine wawili, akiwemo nahodha, pia walijeruhiwa vibaya kwenye mkasa huo uliotajwa na wengi kuwa wa nguvu za giza au wa nguvu za pepo.

Mnamo Aprili 2021, mtu mmoja aliaga dunia huku wengine wawili wakiokolewa baada ya boti walimokuwa wakisafiria kuzama katika hali isiyoeleweka eneo lilo hilo la Tusitiri.

Mnamo Februari 10, 2024, maboti mawili yalizama kiajabu eneo hilo la Tusitiri lakini kwa bahati nzuri abiria wote wakaokolewa na maafisa wa Kenya Coast Guard Services (KCGS) waliokuwa wakipiga doria kwenye Bahari Hindi kwa wakati huo eneo hilo.

Kati ya 2015 hadi sasa, makumi ya ajali za mashua na maafa yamerekodiwa eneo hilo la Tusitiri.

Manahodha na wasafiri waliohojiwa na Taifa Jumapili kuhusu hali halisi ya Tusitiri hawakuficha kushangazwa kwao na vimbwanga vya eneo hilo la Bahari Hindi, ambalo wengi wanaliona kuwa la nuksi wanazoamini kuchangiwa na mapepo au majini.

Bw Musa Athman, ambaye ni nahodha, anashikilia kuwa lazima kuna nguvu za giza eneo hilo la Tusitiri.

Alitoa wito kwa viongozi wa kidini kuja pamoja na kufanya sala, swala na dua ya kufukuza nuksi na kisirani.

Sehemu mojawapo ya eneo la Tusitiri lililoko karibu na ufukwe wa Wiyoni, katikati ya kisiwa cha Lamu na Jeti ya Mokowe. Eneo hilo limevuma kwa kushuhudia ajali za ajabuajabu ambazo wengi wanazihusisha na nguvu za giza au mapepo. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Athman anasema yeye binafsi amewahi kujipata kwenye ajali ya boti lake kugongana na jingine katika hali anayodai hadi leo hajaifahamu.

“Mimi huwa makini sana ninapoendesha chombo changu lakini hiyo siku hadi leo imenichanganya. Nakumbuka nikiendesha boti langu kwa upole na utaratibu. Mbele hakukuwa na chochote. Cha ajabu ni kwamba nilijipata tu nikigongana na mwenzangu, hivyo boti langu liikaanza kuweweseka hadi likazama. Cha kushangaza yule niliyekuwa nikimkwepa hakuonekana tena baada ya sisi kuzama baharini,” akasema Bw Athman.

Bw Athman alikuwa na msaidizi wake botini wakati ajali ilipotokea ambapo wote walifaulu kuogelea hadi nchi kavu lakini boti lao na mizigo, vyote vikizama baharini.

“Tulikuwa wawili botini na magunia ya viazi. Nashukuru kwamba sote tuliogelea na kujinusuru japo tulikuwa na majeraha madogomadogo. Mali yetu yote ndio ilizama baharini. Watu wasitazame vitimbi vya Tusitiri kwa jicho la nje au hali ya kawaida tu. Lazima kuna kitu pale,” akadai.

Bw Abdalla Baishe, mkazi wa Lamu, anasema matukio yenyewe yanayorekodiwa Tusitiri, likiwemo la watoto kufa wakiogelea au kucheza baharini ni ya kutiliwa shaka.

“Ipo siku kijana ambaye ni polisi aliumwa na yeda (stingray) wakati akiogelea eneo hilo la Wiyoni-Tusitiri. Hilo tayari ni jambo lililoshangaza wengi kwani hapo kamwe hakujaonekana yeda miaka yote. Yaani si ngome ya mnyama huyo wa baharini kabisa,” akaeleza Bw Baishe.

Jamaa mwenyewe ilibidi aokolewe dakika za mwisho mwisho akiwa karibu kufa maji.

“Pia kuna kisa ambapo baadhi ya watoto walikuwa wakiogelea pale huku wengine wakicheza ambapo mmoja wao ghafla alikosekana. Wapiga mbizi walikita kambi pale kumsaka mtoto huyo mchana mzima. Baadaye alipatikana akiwa amefariki eneo hilo hilo la Tusitiri. Hapa panatisha,” akasema Bw Baishe.

Harrison Kahindi, nahodha, pia anaamini kuwepo kwa mapepo eneo hilo la Tusitiri.

Anasema manahodha wengi wamejipata wakichanganyikiwa na hata kuishia kuzamisha maboti yao wakati wakipita eneo hilo.

Bw Kahindi anasema huenda roho za wengi zilizoangamia Tusitiri zikawa ndizo zinazochangia mikosi eneo hilo.

“Kuna ajali nyingi zimetokea hapa miaka yote. Maafa yameripitiwa hapa, wengi wakiaga dunia kwa hasira, iwe ni kupitia ajali za maboti, mashua au wanapoogelea baharini. Huenda hasira hizo za kuzimu zikawa ndizo zinadai na hata kuchangia mikosi zaidi kuendelea kushuhudiwa Tusitiri,” akasema Bw Kahindi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Majanga ya Dharura katika Kaunti ya Lamu, Shee Kupi, alisema kuwepo au kutokuwepo kwa mapepo au majini eneo hilo la Tusitiri ni suala ambalo hawezi kulithibitisha bayana, akisisitiza kuwa hizo ni imani tu ambazo zimejengwa na watu.

Bw Kupi anaeleza kuwa msingi au kichocheo cha ajali nyingi zinazoripotiwa Tusitiri ni kutokana na kuwepo kwa mkondo mkali au njia ya maji mengi baharini aliyoitaja kudumu eneo hilo kwa karibu miaka 70 sasa.

Alikiri kuwa vyombo vingi vya baharini, yakiwemo mashua, majahazi, maboti na vyombo vinginevyo vimezama Tusitiri, hali iliyoacha mali ya mamilioni ya fedha ikiangamia.

Alisema vifo vingi pia vimeshuhudiwa Tusitiri.

“Kwa upande wangu mimi ninaamini sababu kuu ya ajali za Tusitiri ni kuwepo kwa huo mkondo mkali. Wale wanaoweka dhana ya kuwepo kwa nguvu za giza au mapepo mahali pale ni imani zao tu walizojenga. Mimi kwa upande wangu siwezi kuzithibitisha bayana imani hizo,” akasema Bw Kupi.

Mkurugenzi wa Idara ya Majanga ya Dharura na Uokozi, Kaunti ya Lamu Bw Shee Kupi. Anasema sababu kuu ya ajali za kila mara eneo hilo la Tusitiri ni kutokana na kuwepo kwa mkondo wa maji makali ya Bahari Hindi eneo hilo. PICHA | KALUME KAZUNGU

Afisa huyo alisema tayari wamepokea maonyo kutoka kwa idara ya hali ya anga kwamba mabaharia wawe waangalifu, hasa wanaposafiri kupitia mahali kama Tusitiri na maeneo mengine mengi hatari katika Bahari Hindi eneo la Lamu.

“Kwa jumla, bahari inashuhudia dhoruba na mawimbi makali kwa sasa, hivyo mabaharia wawe makini. Mahali kama pale kwenye mkondo wa Tusitiri maji yake yamejikusanya na kujipinda pale, hivyo kuhatarisha mabaharia na vyombo vyao. Watu wawe waangalifu,” akasema Bw Kupi.

Mbali na Tusitiri, mikondo au vivuko vingine vinavyotambulika kuwa hatari kwa usafiri baharini ni Mlango wa Tanu ulioko Mkokoni, Mlango wa Bomani, Mlango wa Alii, Mlango wa Shela, Mlango wa Kipungani, Kivuko cha Mkanda na Manda Bruno.

Kwa wale ambao imani zao ni dhabiti, aidha, huu ni wakati wa kupiga dua zaidi kwa Mola kuondoa mikosi ya Tusitiri ili badala ya eneo hilo kuendelea kuonekana kuwa la maafa, mikosi na masaibu mengine mengi, ligeuzwe au kubadilishwa kuwa mahali salama pa watu kujisitiri kwelikweli sawa na lilivyo jina lake.