Eugene Wamalwa: Nitakuwa debeni 2027 kuwania urais
NA WANDERI KAMAU
KIONGOZI wa Democratic Action Party of Kenya (DAP-K), Bw Eugene Wamalwa, ametangaza nia yake kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa ujao, 2027.
Mnamo Jumamosi, Januari 13, 2023 Bw Wamalwa alisema kuwa nafasi za pekee ambazo hajashikilia tangu ajitose kwenye ulingo wa siasa nchini ni ya Naibu Rais na Rais.
Kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha NTV, Bw Wamalwa alisema kuwa kulingana na umri wake, bado ana nafasi ya kuhudumu katika nyadhifa hizo mbili.
“Ninaamini kwamba nimejitayarisha vilivyo na nina tajriba ya kutosha kuliongoza taifa hili. Tayari, nishaidhinishwa na chama changu kuwania urais.
Niko kwenye mchakato wa kujitayarisha kuwania urais,” akasema Bw Wamalwa.
Bw Wamalwa, aliyehudumu kama Waziri wa Ulinzi katika serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, alisema kuwa chama hicho kiko kwenye mchakato wa kuandaa shughuli za kuwasajili wanachama wake kote nchini.
Alisema kuwa hivi karibuni, kitafanya chaguzi za mashinani na baadaye kuandaa kongamano la kitaifa la wajumbe ili kuidhinisha rasmi nia yake ya kuwania urais.
Mbunge huyo wa zamani Saboti, alisema amekuwa akiahirisha nia yake ya kuwania urais tangu 2013, ingawa amekuwa akihudumu kwenye nyadhifa tofauti.
Kiongozi huyo alisema kwamba ikiwa Bw Kenyatta na Rais William Ruto walifaulu kushinda urais na kuingia katika Ikulu, basi hata yeye anaamini ana uwezo kutimiza ndoto hiyo.
“Ninaamini kuwa kuna siku itafika wakati pia mimi nitaingia huko (Ikulu),” akasema.
Mnamo 2013, iliibuka kuwa Bw Kenyatta alikuwa amemteua Bw Wamalwa kama mgombea-mwenza wake, lakini akalazimika kumteua Rais Ruto ili kuboresha nafasi yake kuwania urais.
Wawili hao—Bw Kenyatta na Dkt Ruto—waliwashinda Bw Raila Odinga na kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, kwa zaidi ya kura 800,000 kwenye uchaguzi huo, uliokuwa wenye ushindani mkali.
Bw Wamalwa pia aliudumu kama Waziri wa Haki na Masuala ya Kikatiba kwenye serikali ya Rais Mstaafu (marehemu) Mwai Kibaki hadi 2013.
Alikuwa akihudumu kama wakili hadi 2003, alipowania ubunge katika eneo la Saboti, baada ya kifo cha kakake, Michael Kijana Wamalwa, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Mzee Kibaki.