Fahamu faida ya makundi ya wakulima na wafanyabiashara wadogo
NA BENSON MATHEKA
UKIWA mfanyabiashara au mkulima mdogo, ungana na wengine kwa manufaa yako.
Wataalamu wa biahara na masuala ya fedha wanashauri kuwa wakulima na wafanyabiashara wadogo wakiungana kwa vikundi huwa katika nafasi nzuri ya kunufaika kwa mafunzo na misaada kutoka kwa serikali na mashirika wafadhili.
Miungano inajumuisha makundi au vyama vya ushurika (Sacco).
Wataalamu wanasema kwa kuungana, wakulima wanaweza kupigania bei ya mazao yao na hivyo basi kuongeza mapato yao kuliko mtu anavyofanya binafsi.
“Kila wakati wakulima na wafanyabiashara wakiungana huwa ni kwa manufaa yao. Umoja huwezesha watu kupiga hatua na kupata soko la bidhaa zao lenye ushindani mkuu,” asema Cyrus Kamau, wa shirika la Hope Capital linalofadhili makundi ya wakulima.
Mtaalamu huyu anasema wakiungana, wakulima huweza kubadilishana mawazo ya kuimarisha kilimo. Vile vile, huwa katika nafasi nzuri ya kupata mafunzo kutoka kwa maafisa wa serikali na mashirika mengine.
“Ninajua makundi ya wakulima ambayo baada ya kuungana walipata misaada ya mbegu, kifedha na ushauri kutoka kwa mashirika na sasa wameanzisha miradi mikubwa. Baadhi ya makundi hayo yanauza mazao yao nchi za nje na mengine yamebadilika kuwa kampuni kubwa,” asema.
Anasema japo kila kundi huundwa kutimiza malengo yake, lililo muhimu ni kupata faida.
“Ni muhimu pia kwa wakulima, wawe katika makundi au binafsi wakumbatie teknolojia ili waweze kufaulu shambani na masokoni. Tuko katika enzi za utandawazi na kila anayebaki nyuma atajuta,” anatahadharisha.
Anasema kwa sababu vijana wamebobea katika teknolojia, wanapasa kujiunga na kilimo.
“Suluhu ya uhaba wa chakula Kenya ni vijana kushiriki kilimo. Hata hivyo, serikali inapasa kuwapa motisha unaofaa kwa kupunguza gharama ya pembejeo na kuwapa mikopo nafuu,” aeleza Bw Kamau.
Kulingana na mtaalamu huyu wakulima wengi hupata hasara kwa sababu ya kutotumia mbegu halisi.
“Hakikisha kwamba umepata na kupanda mbegu halisi ili kuepuka hasara. Kuna watu wanaochukia kilimo baada ya kupata hasara bila kujua wao ndio chanzo cha hasara hiyo,” aeleza.
Anasema wauzaji wa mbegu halisi huwa wanafahamu zinazofaa kwa kila eneo.
“Wakiungana kwa vikundi ni rahisi kupata mafunzo kutoka kwa mashirika yanayoshiriki mtandao wa kilimo au biashara,” asema na kuongeza kuwa walio katika vikundi pia huwa wanahimizana wenyewe kwa wenyewe.
“Wanajadiliana na kupata fursa zaidi za hata kuwekeza. Huwa katika nafasi nzuri ya kupata mkopo kupanua biashara au shughuli zao za kilimo,” asema Kamau.
Hata hivyo, anasema ni sharti wanaoungana waweke mifumo ya kisheria inayohitajika kabla ya kunufaika kutoka kwa mashirika ya kutoa mikopo na hata kupokea mafunzo.
“Kimsingi, ni lazima wasajiliwe kisheria chini ya mwavuli mmoja na wadumishe kiwango cha juu cha nidhamu na uaminifu,” anasema.