Makala

Fahamu mataifa yanayoendelea kutekeleza hukumu ya kifo duniani

March 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA WANDERI KAMAU

BAADA ya Mahakama Kuu kumpa Joseph ‘Jowie’ Irungu hukumu ya kifo kutokana na mauaji ya mfanyabiashara Monicah Kimani mnamo 2018, Taifa Leo imeamua kuelekeza darubini yake, kuangazia nchi ambazo bado zinatekeleza hukumu ya kifo kote duniani.

Ijapokuwa hukumu hiyo imekuwa ikitolewa na mahakama tofauti nchini, ilisimamishwa na Katiba ya sasa, iliyopitishwa mnamo 2010.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya sheria, mara nyingi hukumu hiyo huwa inageuzwa kuwa kifungo cha maisha.

Mtu wa mwisho kunyongwa nchini alikuwa mwanajeshi wa ngazi ya juu Hezekiah Ochuka, aliyenyongwa mnamo 1987, baada ya kupatikana na hatia ya uhaini.

Alikuwa miongoni mwa wanajeshi waasi walioongoza jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Mstaafu (marehemu) Daniel Moi mnamo 1982.

Kufikia sasa, nchi 55 kote duniani huwa zinaendesha hukumu ya kifo kwa kuwanyonga wale wanaopatikana na hatia tofauti.

Mataifa tisa kati ya hayo huwa yanatekeleza adhabu hiyo kwa makosa yenye uzito, kama vile mauaji ya halaiki.

Mataifa 23 hayajakuwa yakitumia adhabu hiyo kwa karibu miaka kumi.

Kulingana na shirika la Amnesty International (AI), mataifa 20 ndiyo yamekuwa yakitekeleza adhabu hiyo kwa kiwango kikubwa.

Baadhi ya mataifa ambayo bado yanaendesha hukumu hiyo kwa kuwanyonga watu ni China, Iran, Saudi Arabia, Misri, Amerika, Singapore, Iraq, Kuwait, Somalia na Sudan Kusini.

Mataifa yaliyonyonga idadi kubwa ya watu mnamo 2023 ni China, Misri, Iran, Iraq, Saudi Arabia, Amerika, Vietnam na Yemen.

Korea Kaskazini pia inaorodheshwa kuwa miongoni mwa mataifa yanayonyonga idadi kubwa ya watu.

Shirika hilo limekuwa likiendesha harakati za kuyataka mataifa hayo kuondoa adhabu hiyo, likiitaja kuwa ukiukaji wa haki za binadamu.

Hata hivyo, baadhi ya mataifa hayo yamekuwa yakishikilia kuwa adhabu hiyo inalingana na sheria na tamaduni zake, hivyo hayawezi kuiondoa.

Mfahamu kwa undani Jowie

Jowie ambaye Jumatano alihukumiwa kunyongwa, alizaliwa katika eneo la Gucha, Kaunti ya Nakuru.

Ndiye kitindamimba wa Bw Julius Irungu Mwangi na Bi Anastasia Thama.

Alikulia katika Kaunti ya Nakuru. Babake ni mtaalamu wa mashine aliyestaafu, aliyekuwa akifanya kazi katika Serikali ya Kaunti ya Nakuru. Mamake ni mfugaji kuku nyumbani kwao katika eneo la Nguta, karibu na kambi za kijeshi za Lanet.

Kwenye mahojiano na maafisa wa mahakama kuhusu mienendo ya mwanawe, Bw Irungu alimtaja Jowie kama mtoto aliyekulia katika mazingira ya kawaida. Hakuwa na matatizo yoyote ya kiafya, isipokuwa maradhi ya ugonjwa wa kupumua (yaani asthama) kwa kiwango kidogo.

“Ni mtoto aliyependa kuingiliana na watu, aliyekuwa na hekima kwa kila mtu na taasisi zilizopo. Alikuwa Mkristo, aliyecheza gitaa kwenye kanisa,” akasema babake.

Jowie amehudumu katika nyadhifa za juu kwenye makanisa ya Victoria na Agape jijini Nakuru. Kwa muda mrefu, alikuwa amehudumu kama mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya makanisa hayo.

Dadake Jowie, Bi Nellius Wanjiru, anahudumu katika benki moja jijini Nairobi. Amekuwa karibu na kakake tangu kesi dhidi yake ilipoanza. Amekuwa akisisitiza kwamba hana hatia yoyote; kauli ambayo pia imekuwa ikitolewa na mamake Jowie.

Jowie ana ndugu wengine wawili—kakake, anayehudumu kama mpigapicha katika eneo la Kahawa Sukari, Kaunti ya Kiambu na mwingine ambaye hufanya kazi Dubai, Milki ya Kiarabu (UAE). Taifa Leo haitawataja kwa sababu za kiusalama.

Jowie alisomea katika Shule ya Msingi ya Freehold, Nakuru kati ya Darasa la Kwanza hadi la Nne. Baadaye, alielekea katika shule ya kibinafsi ya Carol Academy, alikofanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE).

Baadaye, alijiunga na shule tatu za upili ambazo ni; Langalanga, St Gabrielle na St Luke, alikofanyia mtihani wake wa Kidato cha Nne (KCSE) mnamo 2010 na kuzoa alama ya D+.

Baada ya kufanya mtihani wa KCSE, alijiunga na Kenya Polytechnic, alikosomea diploma katika masuala ya chakula na kumaliza masomo yake mnamo 2011.

Baada ya hapo, alielekea Dubai, alikopata kazi ya ulinzi. Alipata mafunzo ya kijeshi kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Polisi ya Dubai na kampuni ya usalama ya Ogara Group, ambayo wakati huo ilikuwa na matawi Dubai, Uingereza na mataifa mengine barani Ulaya.