Faida za kiafya unapokula kwa ‘mfungo’
KILA mmoja anataka kuimarisha afya ya mwili ili kuwa na afya njema.
Utafiti umeonyesha kuwa moja ya mbinu za kutimiza hilo ni kula kwa saa chache na kisha ‘kufunga’ kwa saa nyingi – kwa Kimombo intermittent fasting.
Mbinu hii ina manufaa sio tu katika kupunguza uzito wa kilo mwilini bali pia hatari ya kupatwa na maradhi yanayotokana na ulaji vyakula duni, kama vile maradhi ya moyo na kisukari.
Hususan kisukari cha aina ya Type 2 diabetes kwa sababu unapofunga kiwango cha sukari kwa damu hupungua na hivyo kupunguza hitaji la mwili kuunda kimeng’enya cha insulini.
Mwisho, mtindo huu husaidia kukarabati na kuhuisha seli za mwili.
Jinsi ya kushiriki mfungo huu
Maryanne Wanza ni mtaalamu wa mauala ya afya. Katika mahojiano na Afya jamii anasema wanaoshiriki wanapaswa kufuata urari wa 16:8 — unafunga saa 16 na kula saa nane zilizosalia kwa siku moja.
Mfano halisia ni kula kati ya saa sita mchana na saa mbili usiku.
“Mbinu hii imeibuka kupendwa sana sana kwa sababu watu wengi hukosa kula kiamsha kinywa wanaporaukia shughuli za siku. Nayo saa saba au saa nane usiku huwa ni wakati wa kulala,” anatanguliza Wanza.
Mbinu nyingine ni kula siku tano mfululizo ila unahakikisha lishe yako ina kalori 500-600. Kisha unafunga kula siku mbili zitakazofuata (urari wa 5:2).
Pia, Wanza anasema watu wengine huamua kula siku moja kisha kufunga siku inayofuata. Au wanakula vyakula vilivyo na kiwango cha chini cha kalori wakati wa mfungo.
“Mbinu ya mwisho ni wale wanaofunga kula na kunywa kwa saa 24 za siku. Hii huwa mara moja au mbili kwa wiki,” aeleza mtaalamu huyu wa lishe bora.
Mtindo huu wa kula kwa kipindi fulani pekee na kufunga saa zilizosalia husaidia mtu kudhibiti hamu ya kula kiholela pindi tu unapohisi njaa.
Pia, unasaidia mtu kuchagua mlo mahususi usio na kalori nyingi. Vile vile, unakufunza kuwa na ustahimilivu wa muda mrefu bila chakula.
Wanza, hata hivyo, anatahadharisha kwamba mfungo huu sio wa kila mtu.
“Akina mama wajawazito au wanaonyonyesha watoto, watu wenye historia ya kufakamia mlo kwa sababu ya msongo wa mawazo (eating disorder), watoto, wagonjwa au wanaopata nafuu baada ya ugonjwa, watu wanaougua kisukari, watu wanaofanya mazoezi ya mwili, na watu wanaofanya kazi zinazotumia nguvu nyingi hawafai kushiriki mfungo huu,” anaeleza.
Aina za chakula utakazotumia
Chakula utakachokula baada ya kufunga kitalingana na muda ambao ulikuwa umefunga.
Wanza asema ni vyema kula vyakula vyenye lishe bora kama mchele wa kahawia, njugu, samaki, kuku, na karoti.
Pia, mboga mbalimbali kama spinachi, sukumawiki, na managu. Kisha matunda kama chungwa au embe.
“Protini itakusaidia kujenga misuli ya mwili. Vyakula vyenye mafuta asilia kama njugu kukupa nguvu. Vyakula vilivyochachushwa (kwa Kimombo fermented) na vile vyenye nyuzinyuzi vitaimarisha bakteria salama mwilini. Pia kunywa maji wakati umefunga ili mwili usikauke,” anahoji mtaalamu huyo.
Vinywaji vingine unavyoweza kutumia wakati wa mfungo ni chai asili isiyo na sukari, au hata kahawa ilmradi si kwa wingi usije kujipata na matatizo ya moyo yanayoletwa na kafeini.
Kwa upande mwingine, Wanza anasema hufai kula vyakula vilivyo na sukari au chumvi nyingi, vilivyopikwa kwa mafuta mengi, na vile vya kusindikwa (kwa kimombo processed food).
“Jiepushe na vinywaji kama juisi na pombe kwani vitapandisha insulini kwa damu,” aeleza.
Ili kupata manufaa zaidi kutokana na mbinu hii ya kula kwa mfungo Wanza anakushauri kufanya mazoezi, lakini kwanza uwe umekula. Wakati umefunga unaweza kutembea kwa haraka au kukimbia polepole, ila ni vyema utie kitu tumboni baadaye.
“Baada ya mazoezi kula protini kama kuku au samaki na nafaka isiyokobolewa kama mahindi, mchele, ngano, mtama, mawele na mbegu za chia,” ashauri.
Yapo madhara ya mbinu hii?
Unaweza kupata maumivu ya kichwa au kuhisi kisunzi ukikosa kula kwa muda mrefu kwa sababu sukari imepungua katika damu.
Pili, mtaalamu Wanza anatahadhari kwamba unaweza kujipata umefakamia mlo kupita kiasi wakati ule wa kula, eti unafidia saa za mfungo, na hivyo kuongeza kilo badala ya kupunguza.
“Unaweza kuhisi uchovu, hasira au hata njaa na ukakosa kutekeleza majukumu yako ya siku,” aeleza.
Watu wengine pia huripoti kutoweza kulala vizuri.