Faini ya Sh10.5 milioni ni kunionea; naadhibiwa kwa kuongea – Orwoba
ALIYEKUWA Seneta Maalum Gloria Orwoba amesema anaheshimu uamuzi wa mahakama uliomwamuru kumlipa Karani wa Seneti Jeremiah Nyegenye Sh10.5 milioni kwa kumharibia (karani huyo) jina, lakini hakubaliani nao.
Kwenye kikao na wanahabari Jumanne, saa chache baada ya Hakimu wa Mahakama ya Milimani Ruguru Ngotho kutoa uamuzi huo, Bi Orwoba alisema amewasilisha notisi ya rufaa.
“Ningependa kuweka wazi kwamba naheshimu uamuzi huo uliotolewa na mahakamani. Lakini sikubaliani nao na ndio maana mawakili wangu wamewasilisha ilani ya rufaa kwani ni haki yangu,” akaeleza.
“Mungu ataaibika ikiwa nitakufa roho na kukubali uamuzi huu japo naheshimu idara ya mahakama. Mungu aliniwezesha kuingia Bunge kwa sababu maalum. Niko tayari kulipia gharama zote,” Bi Orwoba akaongeza.
Mwanasiasa huyo alisema ataendelea kutetea haki zake kama mwanamke sawa na haki za wanawake wengine wanaopitia aina mbalimbali za dhuluma katika jamii.

Picha|Charles Wasonga
Katika uamuzi wake, Hakimu Ngotho alibaini kuwa jumbe ambazo Bi Orwoba aliweka katika mitandao ya kijamii alikidai Bw Nyegenye alimdhulumu zilimharibia jina, “kusababishia msongo wa kiakili na kumwaibisha karani huyo wa Seneti.”
Aidha, hakimu huyo alimwagiza Orwoba kumwomba masamaha Bw Nyegenye hadharani ndani ya muda wa siku 30 la sivyo alipe Sh1 milioni zaidi.
Isitoshe, Hakimu Ngotho alimzima Bi Orwoba au washirika wake kuchapisha taarifa zozote za kumharibia jina karani huyo wa Seneti.
Mnamo Mei 19, 205 chama cha United Democratic Alliance (UDA), kilichomteua kama Seneta, kilimvua uanachama.
Chama hicho kilisema kilimpata Orwoba na hatia ya kuvunja kanuni na sheria zake kwa kushirikiana na mrengo hasimu wa kisiasa.
Bi Orwoba ni miongoni mwa wanasiasa kutoka jamii ya Kisii ambao mnamo Aprili 24, 2025 walimlaki aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i aliporejea nchini kutoka Amerika.