Familia ya watu 33 iliyofurushwa kijijini Kamora kwa kuhusishwa na ushirikina yaomba usaidizi
Na GAITANO PESSA
FAMILIA moja ya watu 33 kutoka kijiji cha Kamora, wilayani Teso Kusini inalilia usaidizi baada ya kufurushwa kutoka kijiji hicho kwa madai ya ushirikina.
Familia hiyo ambayo imepiga kambi karibu na hospitali ya wilaya ya Alupe tangu Juni 13, 2016, ilihusishwa na vifo vya wakazi zaidi ya watatu ambao wanakijiji walidai kuwa vilitokana na maswala ya uchawi.
Ikiongozwa na Simon Ong’amo, familia hii imeambia Taifa Leo kuwa wanakijiji waliwafurusha na baadaye wakateketeza nyumba yao; hatua ambayo iliwaacha bila makao.
“Tulifurushwa kwa madai ya ushirikina bila ushahidi wowote. Zaidi ya nyumba tano ziliteketezwa na kutuacha bila pa kwenda,” amedai Bw Ong’amo.
Baadaye serikali ya kitaifa iliwanusuru kwa kuwapa makao katika ghala moja kuu eneo la Alupe kujisitiri japo jumba hilo limewaongezea masaibu hata zaidi kutokana na baridi kali wanayokumbana nayo kila siku.
Paa la jumba hilo pia linavuja sana hasa msimu huu wa mvua ya masika katika eneo hilo.
“Hili Jumba linavuja sana. Milango na madirisha haina vioo na hivyo basi kutuanika kwa baridi na mbu. Tunahisi serikali imetutelekeza tangu itupe makao haya,” alisema.
Bw Ong’amo ameongeza kuwa wanalazimika kufanya kazi za sulubu kujikimu maishani kando na wanao kujihusisha na vibarua shambani na kuwaoshea wakazi nguo katika jitihada za kutafuta pesa za kununua chakula.
Ameongeza kuwa juhudi zao za kupata makao mapya ziligonga mwamba 2017 baada ya matapeli kutoweka na mabati zaidi 100 walizokabidhiwa na aliyekuwa mbunge wa Teso Kusini Mary Emaase.
“Bi Emaase alitueleza kuwa tutapokea mabati kutoka kwa afisi za uongozi wa mikoa mjini Busia lakini juhudi hizo zimegonga mwamba baada kupuuzwa na kila afisa tunayemweleza hitaji letu.”
Familia hiyo sasa imeitaka serikali kusikia kilio chao na kuwasaidia kurejea makwao ili kuepuka masaibu zaidi.
“Tangu mwaka wa 2016 tumekuwa tukipitia hali ngumu na la kustaajabisha ni kuwa wakazi wa Kamora wangali wanatutishia dhidi ya kurejea kijijini,” amesema Ong’amo.
Licha ya kuwashtaki wale wanaowatishia, familia hii inasema kuwa hatua zozote za kisheria hazijachukuliwa dhidi ya wahusika.
“Tutaishi hivi hadi lini? Mbona tuwe wakimbizi katika taifa letu. Serikali itusaidie turejee Kamora ili kuepukana na masaibu zaidi.”