Familia yadai polisi wanajua aliko MCA aliyetoweka mahakama ikimsakama IG Kanja
NI siku 16 tangu Diwani Yussuf Hussein Ahmed wa Wadi ya Della Kaunti ya Wajir atekwe nyara na watu wanaotuhumiwa kuwa maafisa wa polisi.
Hali ya suitafahamu na wasiwasi imekumba familia yake – Haijui aliko lakini wana mashaka.
Ili kutegua kitendawili hiki cha Bw Ahmed, Jaji Alexander Muteti, mnamo Ijumaa (Septemba 27,2024) alimpa Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Douglas Kanja siku saba (7) kufanya juu chini kutambua aliko diwani huyo.
Mawakili Shadrack Wambui, Sam Nyaberi, Danstan Omari na Hosea Manwa walimweleza Jaji Muteti kwamba familia ya diwani huyo inaamini kwamba alitekwa nyara na maafisa wa polisi.
“Mahakama hii imempa siku saba (7) IG kuwasilisha ripoti kamili mahakamani kuhusu aliko Bw Ahmed,”Jaji Muteti aliamuru baada ya kupokea ripoti kutoka kwa Naibu wa Mkuu wa Uchunguzi wa Jinai (DRCIO) Msimamizi Mkuu (SSP) Justus Imaana.
SSP Imaana alieleza mahakama kwamba polisi katika kituo cha polisi cha Industrial Area walipokea ripoti ya utekwaji nyara wa Bw Ahmed na dereva wa teksi Wambua Kioko mnamo Septemba 13,2024 saa tatu usiku.
Mahakama ilielezwa Bw Ahmed alikuwa anatoka mtaani South C kuelekea Pangani.
Alikuwa ameabiri teksi
Kwenye barabara ya Enterprise Road, Nairobi, Jaji Muteti alielezwa na Bw Imaana kwamba, magari mawili muundo wa Prado (ya rangi nyeupe na nyeusi) walimwandama Bw Kioko na kumzuia mbele.
“Mmoja wa wanaume watano waliokuwa wamejihami kwa bunduki na bastola alifungua gari langu baada ya kuziba barabara na kumvuruta Bw Ahmed kutoka kwa gari. Walimwingiza ndani ya Prado nyeusi na kutoroka naye,” Bw Imaana alimweleza Jaji Muteti.
Afisa huyo alifika kortini kutoa taarifa ya Bw Ahmed kufuatia agizo la Jaji Muteti.
Wakimhoji Bw Imana, mawakili Nyaberi, Wambui, Omari na Manwa walimweleza Jaji Muteti kwamba familia inaamini diwani huyo angali anazuiliwa na polisi.
Kwa mujibu wa familia hiyo Bw Ahmed alikuwa ameagizwa na kamati ya usalama afike mbele yake Agosti 8,2024 kuhojiwa kuhusu usalama katika Wadi ya Della.
Msemaji wa familia hiyo amedokeza kwamba “Bw Ahmed alifika mbele ya kamati hiyo lakini alichohojiwa hakufichua.”
Akimhoji Bw Imana kortini Bw Wambui alieleza Jaji Muteti “familia ya diwani huyo aliye naibu wa waliowengi katika Bunge la Kaunti ya Wajir inaamini alitekwa nyara na polisi.”
Bw Imana alishindwa kueleza nambari za usajili za magari hayo ya Prado yaliyomwandama Bw Ahmed usiku wa Septemba 13,2024.
Uchunguzi wa CCTV
Mahakama ilielezewa kwamba video za kamera za CCTV katika majengo na kituo cha mafuta ya Petrol cha Ola zimepelekwa katika maabara ya idara ya uchunguzi wa jinai (DCI) kukaguliwa.
Mahakama ilijuzwa na Bw Imaana kwamba simu ya Bw Ahmed iliyopatikana ndani ya gari la teksi aliyokuwa ameabiri imepelekwa kuchunguzwa na maafisa wa DCI.
“Je, kulingana na muda uliopita tangu Bw Kioko awasilishe ripoti ya kisa hicho ni wazi idara ya polisi imekuwa na uzembe wa kumsaka aliko Ahmed,” Bw Omari alimwuliza Bw Imaana.
“Tangu ripoti iwasilishwe mengi yamefanywa na polisi wanaendelea na uchunguzi. Diwani huyu angelikuwa mikononi mwa polisi ningeliambia hii mahakama,” Bw Imaana alijibu.
Katika mawasilisho yao mawakili hao waliambia mahakama kwamba polisi hawajaonyesha pupa kumsaka aliko Bw Ahmed.
“Maisha ya binadamu ni kitu cha thamani kuu.Familia ya diwani huyo imegumbikwa na hali ya suinto fahamu kwa vile siku inapopita bila ya yeye kurudi inaongezea wasi wasi kuhusu usalama wake,” Bw Omari alimweleza Jaji Muteti.
Jaji huyo alikubaliana na msimamo wa familia hiyo na kusema “suala la haki na maisha ya mmoja ni jambo la kuchukuliwa kwa uzito na asasi zote za serikali.”
Jaji Muteti aliamuru polisi wafanye kila juhudi kutambua aliko diwani huyo.
Kwa mujibu wa msemaji wa familia ya Bw Ahmed aliitwa na kamati ya usalama ya kaunti ya Wajir.
Familia yake iliambia Taifa Leo kwamba, alihudhuria mkutano na wakuu wa usalama katika afisi ya kamishna wa Kaunti ya Wajir mnamo Agosti 8 saa nne asubuhi.
Baada ya kurejea nyumbani hakuzugumza na yeyote kuhusu mjadala wake na wakuu wa usalama.
Usiku wa kutekwa nyara
Usiku aliotekwa nyara Septemba 13,2024, watu wasiojulikana walizuia teksi iliyokuwa imembeba mwanasiasa huyo.
Mmoja wa watekaji nyara hao alimwekea Kioko bunduki kichwani na kutisha kumtwanga risasi.
Watekaji nyara hao walimnyaka na kutoroka naye.
Familia yake, marafiki, wafanyakazi wenzake na jamii sasa wanasalia katika hali ya kutatanishana kujawa na hofu huku polisi wakisisitiza kuwa hawakumkamata na hawamzuilii.
‘Kabla ya kutekwa nyara, hakuwa ameonyesha hofu yoyote kuhusu maisha yake au kuwa na makabiliano na polisi,” msemaji wa familia aliambia Taifa Leo.
Lakini mnamo Agosti 6,2024, Bw Ahmed alipokea barua kutoka kwa kamati ya usalama ya Wajir ikimtaka ahudhurie mkutano Agosti 8,2024. Alihudhuria mkutano na wakuu wa usalama katika afisi ya kamishna wa Kaunti ya Wajir mnamo Agosti 8 saa nne asubuhi.
Alisema barua ya kumwalika katika mkutano huo wa usalama ilitaja, ajenda ilikuwa masuala ya usalama katika eneo la Dela-Anole na Riara kaunti ya Wajir.
“Hakutoa maelezo kuhusu waliyozungumza katika mkutano huo,” familia iliambia Taifa Leo.
Bw Ahmed, aliyezaliwa katika kijiji cha Anole eneo bunge la Eldas mnamo Januari 25, 1994, alilelewa kama mtoto mwingine yeyote katika jamii yake ambapo alisomea Shule ya Msingi ya Eldas na baadaye Shule ya Sekondari ya Griftu.
Baada ya kumaliza diploma ya usimamizi wa biashara katika Frontier Institute of Professional Studies, aliibuka kuwa mfanyabiashara tajika, akiendesha maduka ya Mpesa na kuuza bidhaa kwa jumla.
Ahmed ameoa wake wanne na ana watoto.
Jaji Muteti aliamuru kesi hiyo itajwe Oktoba 7,2024 DCI awasilishe ripoti aliko diwani huyo.