Familia yakwama na maiti miaka minne kaunti ikidai kumiliki ardhi wanamoishi
FAMILIA mmoja kutoka Kaunti ya Vihiga imeshindwa kuzika mpendwa wao aliyefariki miaka minne iliyopita baada ya serikali ya Kaunti kuelekea mahakamani kupinga kuzikwa kwake ikidai kumiliki shamba la marehemu.
Hezekiah Mavisi Ondego, 83, alifariki Novemba 11, 2020 kabla ya kukata rufaa ya kupinga uamuzi wa mahakama ya Kakamega iliyoamua kuwa familia yake inamiliki shamba hilo kinyume na sheria.
Bw Ondego alitarajiwa kuzikwa Novemba 21, 2020 katika shamba alilodai kuwa lake, lakini serikali ya Kaunti ikaelekea mahakamani Novemba 20, saa tano asubuhi kuomba kusitishwa kuzikwa kwake.
Mwanawe marehemu, Philip Odari anasema pingamizi la kumiliki shamba lao – South Maragoli/Bugonda/2097 lilijitokeza upya wakati serikali ya ugatuzi ilianza nchini.
Hii ni baada ya aliyekuwa gavana mwaka 2013-2017 Bw Moses Akaranga kuwataka wahamie hadi eneo la Lugari ili kutoa nafasi ya kujenzi wa afisi za kaunti.
Familia ya marehemu inadai shamba lililotolewa na manisipaa mwaka 1988 katika eneo la Lugari-Mautumu Central settlement scheme/1397 tayari linamilikiwa na familia nyingine.
“Hatujakataa kuhama. Mzee alitembelea shamba ambalo alipewa na manisipaa ikaonekana kuwa linamilikiwa na mtu mwingine,” alieleza Bw Odari.
“Hata alipotembelea shamba hilo alipigwa na mmliki wa shamba hilo hadi akapoteza uwezo wa kusikia, mwenzake akivunjwa mguu,” alisema Bw Odari huku Taifa Leo ikionyeshwa barua ya daktari mwaka 2014.
Mzozo huo ulipelekea Bw Hezekiah Mavisi Ondego (Marehemu) kuelekea mahakamani kutafuta haki.
Hata hivyo, alipata pigo baada ya Jaji wa Mahakama ya Kakamega Nelly Matheka Awori kuamuru kuwa anamiliki ardhi hiyo kinyume na sheria.
“Uamuzi ulitolewa mwaka 2019 kuwa tunamiliki shamba la babu yetu kinyume na sheria. Baba hakuwa amekubali kuhama kwa kuwa alifanya uchunguzi wake akaona tukihamia Lugari au Mau Forest tutakuwa wakimbizi,” aliongeza Bw Odari.
Jaji Matheka aliyetoa uamuzi huo, alisema kuwa hati inayomilikiwa na familia hiyo ilipatikana kwa njia ya ulaghai.
“Naona mlalamishi wa kwanza alilipwa fidia ipasavyo kwa kukubali ardhi mbadala na akahama. Pia, mlalamshi wa kwanza aligawanya ardhi na hati miliki husika zote zilitolewa mwezi Desemba 2013…na kukabidhiwa watu watatu, alikuwa akijihusisha na udanganyifu…” aliamuru Jaji Matheka.
Familia hiyo kwa sasa inaomba serikali ya kaunti kufanya nao mkutano wa maelewano wa kumpumzisha mpendwa wao.
Bw Odari anasema mamake Bi Grace Imali Masivi amepatwa na msongo wa mawazo kwa kushindwa kumzika mumewe. Aliongeza kuwa Bi Masivi analazimika kutembelea hifadhi ya maiti ya hospitali ya Rufaa ya Vihiga kila mwezi kuona mwili wa mumewe.
Taifa Leo ilizungumza na Waziri wa Mipango, Ardhi na Nyumba Kaunti ya Vihiga Victor Kivaya Cheye ambaye alisisitiza kuwa ardhi hiyo inamilikiwa na serikali ya kaunti.
Akiegemea uamuzi uliotolewa na mahakama mwaka 2019, alisema kuwa kaunti inapangia kujenga afisi zaidi katika ardhi hiyo.
“Ndio, familia haijamzika na hakuna mzozo hapo. Korti ilitoa uamuzi na hatuwezi kuruhusu marehemu azikwe,” alisema Bw Cheye.