FATAKI: Ukiachwa kubali yaishe, hii tabia ya kitoto ya kumpapura mwenzio mitandaoni ni ushenzi!
Na PAULINE ONGAJI
Siku kadha zilizopita tulitofautiana na kaka mmoja mtandaoni kufuatia hatua yake ya kuchapisha ujumbe kumtusi binti fulani.
Inasemekana kuwa kaka huyu alikuwa amemtema binti huyo ambaye alikuwa mpenzi wake wa zamani. “Mwanamume akikuacha nenda zako. Badala ya kumfuatafuata ishi maisha yako uache kuwa kama nzi wanavyofuata kinyesi,” aliandika chini ya picha ya msichana huyo.
Hayo hayakuishia hapo tu kwani baadaye dume hili lilichapisha picha yake wakibusiana na binti mwingine huku akidai kuwa alikuwa mpenzi wake mpya pengine kumfanya mshikaji wake wa zamani ahisi wivu.
Bila kuzingatia nini kilichosababisha uhasama baina ya wapenzi hawa wa zamani, suala dhahiri ni kuwa bwana huyu alionyesha tabia ya kipumbavu na kitoto.
Lakini ukichunguza zaidi utapata si yeye tu, wapo wengine. Ni mara ngapi umeshuhudia watu wakielekeza hasira zao mtandaoni baada ya uhusiano wao kuvunjika?
Picha
Au hata kuchapisha picha za wapenzi wao wa sasa ili kumtonesha kidonda wa zamani? Kuchapisha picha za wapenzi wao wapya kwenye kurasa zao za Facebook, kwenye WhatsApp miongoni mwa mambo mengine?
Kadhalika kunao wanaochapisha nukuu za matusi mtandaoni ili kuwaudhi wapenzi wao wa zamani.
Pengine unafanya hivi ili kumuudhi mwenzako mbali na maoni yako kupendwa na watu kadha, lakini mwishowe unapaswa kujiuliza ungehisi vipi ikiwa mwenzako angeutangazia umlimwengu wote kuwa amekutema?
Hiyo ni tabia ya kitoto na inasinya hata zaidi hasa ikiwa ni mwanamume aliyeota ndevu anayefanya hivi. Kwani unadhani penzi lako ni oksijeni? Wadhani bila wewe maisha yatamkatikia mwenzako?
Kiburi
Watu wanapaswa kukomesha hiki kiburi kinachowadanganya kuwa wana umuhimu sana maishani mwa watu wengine kiasi cha kuwa wakiondoka, basi dunia itafika mwisho.
Kabla ya hata kuingiwa na fikra za aina hii unapaswa kujiuliza mlikutana na mhusika akiwa na umri gani? Kabla ya kuja maishani mwake hakuwa na uwezo wa kupumua?
Je, wewe ni chakula au maji ya mhusika kiasi cha kwamba ukimtema, basi atakufa njaa au kwa kiu? Je, ni wewe pekee uliye stadi katika masuala ya mahaba?
Kwa kifupi acha kuonyesha upumbavu wako mtandaoni. Ukitema au kutemwa na mwenzio, nenda zako kwa amani. Penzi lako sio muhimu sana maishani mwa mwenzio kiasi cha kwamba ukiamuacha basi hakuna mwingine ambaye ataona uzuri wake.
Pindi utakapoelewa, basi pengine tabia za kitoto zitakuondoka.