Makala

Finya Kompyuta Upate Dola: Mambo ya kuelewa kuhusu mpango huu mpya wa serikali

February 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

HATUA ya serikali kuzindua mpango wa ‘Finya Kompyuta Upate Dola’ umezua maswali kuhusu ikiwa utafaulu, ikizingatiwa kuwa huu si mpango wa kwanza kuwakuza na kuwaendeleza vijana kidijitali kuzinduliwa.

Kulingana na tangazo la serikali, mpango huo unalenga kuwapa vijana ujuzi wa kidijitali, ili kuwawezesha kupata kazi mtandaoni.

Mpango huo unafuatia kauli ya Rais William Ruto kwa vijana nchini kukumbatia teknolojia ili kujiendeleza kimapato.

“Lengo kuu la mpango huu ni kuwapa vijana ujuzi wa kidijitali kufanya kazi mtandaoni ili kupata pesa za kujiendeleza kimaisha,” ikasema notisi iliyotolewa na Wizara ya Leba na Ulinzi wa Jamii mnamo Jumatatu.

Kulingana na notisi hiyo, mpango huo unalenga kujumuisha mafunzo tofauti ili kuhakikisha vijana wamepata ujuzi wa kutosha kujiendeleza kimaisha.’

Mpango huo umepangiwa kuanza Machi 4 hadi 8 mwaka huu, kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 11 jioni.

Katika siku za hivi karibuni, Rais Ruto amekuwa akiwarai vijana kukumbatia mtandao ili kujipatia mapato, ijapokuwa serikali yake imekuwa ikikosolewa kwa kutoweka miundomsingi ya kutosha kufanikisha mpango huo.

“Ningetaka kuwaambia vijana kufinya kompyuta ili kupata pesa [dola]. Lazima tukumbatie uwepo wa mtandao ili kuhakikisha tumejitengenezea ajira,” akasema Rais Ruto mwezi uliopita, alipohutubu katika Kauti ya Bungoma.

Hata hivyo, kauli yake imekuwa ikokosolewa na Wakenya kwenye mitandao ya kijamii, baadhi wakiitilia mzaha kuhusu ikiwa mpango huo utafaulu.

Baadhi ya wacheshi ambao wametoa video za kicheshi kuukejeli mpango huo ni Victor Naaman.

“Nataka kufinya kipakatalishi ili nipate dola…..,” anasema mcheshi huyo kwa njia ya kejeli.

Wakenya pia wamekuwa wakitoa jumbe za kejeli katika mitandao ya kijamii, wengine wakiutaja kuwa “mzaha wa serikali”.

Baadhi ya mipango kama hiyo iliyoanzishwa bila mafanikio ni Ajira Digital, ambapo vijana wengi wamekuwa wakisema haikufanikiwa kama ilivyotarajiwa.

Mpango huo, hata hivyo, ulianzishwa na serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.