• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 4:55 PM
Gachagua aahidi kuponda wafufuaji wa ‘Mungiki’

Gachagua aahidi kuponda wafufuaji wa ‘Mungiki’

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ameapa kutumia mikakati na nguvu zote kukabiliana na kuchipuka upya kwa kundi haramu la ‘Mungiki’ eneo la Mlima Kenya, akisema ataiga mfano wa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, marehemu John Michuki.

Michuki alikuwa waziri katika afisi hiyo ya kiusalama kati ya 2005 hadi 2008 ambapo genge la ‘Mungiki’ lilikuwa limezindua misururu ya dhuluma za kijamii na kiuchumi eneo hilo.

Aliaga dunia mnamo Februari 21, 2012, akiwa na umri wa miaka 79 na huenziwa sana eneo la Mlima Kenya hasa katika Kaunti ya Murang’a ambako pia ndiko alikozaliwa.

Kundi hilo la ‘Mungiki’ lilifahamika kupitia dhuluma za kukeketa wanawake, kuwabaka, kutoza ushuru sekta za ujenzi na uchukuzi huku waliokaidi wakiuawa kupitia kukatwa vichwa.

Vijana wadogo waliingizwa katika kundi hilo kwa lazima huku wakilishwa viapo vya utiifu na kuamrishwa wakikusanya pesa wawe wakituma hadi Nairobi katika makao makuu ya genge hilo.

Miezi mitano taifa likielekea uchaguzi mkuu wa 2007, Michuki alitangaza vita dhidi ya ‘serikali ya Mungiki’ akisema kwamba hata ikiwa hilo lingemaanisha yeye kupoteza wadhifa wake kama mbunge wa Kangema naye mwaniaji wa Urais Mwai Kibaki akose awamu ya pili, haikujalisha.

“Hatuwezi tukabadilishana  maisha ya watu na kura zenu ikiwa mmekuwa watundu hivi ndio tuwavumilie tukiwaomba hizo kura zenu, kaeni nazo na kuanzia sasa, hawa Mungiki wasipobadili mienendo yao basi mtakuwa mnasikia tu kuhusu mazishi yao,” akatangaza Michuki.

Kulizuka harakati za mauaji ya washukiwa huku wengine hadi sasa wakitoweka, Michuki akashinda kiti hicho cha Kangema licha ya operesheni hiyo dhidi ya Mungiki kunoga katika eneo hilo na Bw Kibaki pia akajipa awamu ya pili mamlakani, ishara kwamba wenyeji waliunga mkono kikamilifu mikakati ya kudhalilisha kundi hilo.

Marehemu John Michuki. PICHA | MAKTABA

Akionekana kuiga mwelekeo huo wa Michuki, Naibu Rais akiongea katika Kaunti ya Nyandarua mnamo Jumanne alikohudhuria mazishi ya babake Seneta John Methu, marehemu Michael Maigo Waweru, alisema “ikiwa nitapoteza kura kupitia harakati za kupambana na Mungiki na iwe hivyo”.

Alisema kwamba kundi hilo linafufuliwa kwa msingi wa kisiasa.

“Kkamwe hakuna vile tutakubali kurejea kwa ukeketaji wa wanawake, utozaji ushuru kwa biashara za wenyewe… kuua watu kiholela… hilo kamwe halitarejea hapa,” akaapa Bw Gachagua.

Bw Gachagua alipuuzilia mbali tetesi za baadhi ya wenyeji ambao wamekuwa wakimshutumu kwa kutangaza vita na vijana wa Mlima Kenya ambao ndio sanasana huingia katika kundi hilo.

“Sasa wakora wakiwa ni wa jamii hii yetu tunyamaze eti ni watoto wetu? Wakianza kuua huwa wanaua watu wa wapi? Huwa wanatoza ushuru biashara za wapi? Huwa wanakeketa wanawake wa wapi? Acha hapa tu kwetu, hakuna mahali popote pale katika taifa hili watakubaliwa kujiunda,” akasema.

Mnamo Januari 1, 2024, mwenyekiti wa baraza la Agikuyu Bw Wachira Kiago aliteta kwamba “Gachagua amezindua njama ya kupigana na vijana wetu ambao wanashiriki hafla za kitamaduni katika makavazi yetu ya kimila kama Mukurwe wa Nyagathanga na ambapo wazazi wa jamii yetu walikuwa wakiishi”.

Alikuwa akiteta kunyakwa kwa vijana 25 mnamo Desemba 31, 2023, katika makavazi hayo na kutuhumiwa kuwa wafuasi wa Mungiki.

Lakini akimjibu, Bw Gachagua alihoji hali ambapo miongoni mwa washukiwa hao, alikuwepo kijana wa umri wa miaka 11 na ambaye alipatikana na mafuta spesheli ya mbuzi, visu, pembe za ng’ombe, ugoro na pombe ya kitamaduni inayojulikana kama Muratina.

“Sasa huo ndio utamaduni mnaotuambia kuuhusu? Kijana wa umri wa miaka 11 ambaye hata hajaenda shule ya sekondari alikuwa akishiriki utamaduni gani wa pombe, ugoro na vifaa vya kiapo? Tukome kubebana ujinga,” akasema.

Bw Gachagua alisema kwamba “nawataka viongozi wa Mlima Kenya wakome kuwahurumia hawa watu na wasitishwe… waendelee kupinga urejeo wa Mungiki katika jamii”.

Alisema kuwa “tuko na wajibu wa kuzuia vijana hawa wetu kutumiwa vibaya na mtu mmoja ambaye akishaokotewa pesa mashinani na kutumiwa zikiwa kwa bahasha, anaendelea kujitajirisha kwa kujijengea majumba ya kifahari huku nao vijana hao wakizidi kuwa maskini”.

  • Tags

You can share this post!

Raila ataka Ruto ‘ashuke’ naye akiwekewa presha

Wito busara itumike kufanikisha mradi wa kawi ya nyuklia

T L