Gachagua: Sisi ni wa nani?
NA MWANGI MUIRURI
NAIBU Rais Rigathi Gachagua mnamo Jumatano alisema kwamba wakulima wa kahawa wa Mlima Kenya wanafaa pia kusamehewa madeni, sawa na wenzao wa miwa kutoka eneo la Magharibi.
Mwezi Februari, Rais William Ruto alisamehea wakulima wa miwa wa Nzoia deni la Sh50 bilioni na akaapa kuwafanyia hivyo wenzao wa viwanda vya Muhoroni, Chemelil, SoNy na Miwani ambapo madeni ni Sh117 bilioni.
Akiongea kwa lugha ya Gikuyu akiwa katika Kaunti ya Murang’a, Bw Gachagua alisema kwamba hakuna mtoto wa kubebwa kwa upande wa tumbo na mwingine abebwe kwa mgongo. Ikiwa wengine wanasamehewa madeni kwani sisi ni wa nani?”.
Alisema kwamba Wizara ya Ushirika na Wizara ya Fedha kwa sasa ziko katika harakati za kuandaa mikakati ya kutangaza msamaha huo wa madeni ya kahawa.
Bw Gachagua alikuwa ametembea katika Kaunti ya Murang’a kufungua kiwanda cha kusaga kahawa cha Ikundu ambacho kilizinduliwa na gavana wa kwanza wa Murang’a Bw Mwangi wa Iria kwa bajeti ya Sh180 milioni.
Ni hafla ambayo Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, Seneta wa Murang’a Joe Nyutu na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a Betty Maina hawakufika.
Kaunti hiyo katika siku za hivi majuzi imekuwa ya miereka ya kisiasa kati ya kambi ya Bw Gachagua na ya Bw Nyoro licha ya Rais Ruto kusemekana kuwaonya dhidi ya kugawanya wenyeji.
Wiki iliyopita, Bi Maina aliteta kwamba “kuna wanasiasa ambao kazi yao ni kujitafutia umaarufu kwa kushinda wakifuatana na Naibu Rais na kukesha wakitangaza kwamba wako nyuma yake”.
“Hata Bw Gachagua naye anafaa kupanua mikakati yake na kujiangazia kama kiongozi wa kitaifa,” akasema Bi Maina.
Bw Nyoro amekuwa akitua maeneo kadha ya nchi akionekana waziwazi kujipa sura ya kitaifa katika siasa zake na kuunda miungano na wanasiasa wa kimaeneo.
Bw Gachagua kisha alifululiza hadi chuo kikuu cha Murang’a kilichoko katika eneo bunge la Kiharu kutoa hotuba ya hadhara na Bw Nyoro kama mwenyeji hakufika na hakutoa pole ya kutofika.
Ni hali ambayo iliwaacha wadadisi wa masuala ya kisiasa wakizua gumzo kuhusu kivumbi cha 2027 ambapo Bw Gachagua na Bw Nyoro wanaonekana wazi kuwa na kambi kinzani zinazobishania uthibiti wasiasa za Mlima Kenya.
Licha ya Bw Nyoro kukana kwamba yuko katika upinzani na Bw Gachagua, mikakati yake katika siku za hivi karibuni imekuwa ikimwangazia kama aliye katika harakati za kujikarabati kwa makuu ya siasa za baadaye.
Bw Nyutu ambaye tayari ashatangaza kwamba anamuunga Bw Nyoro kuteuliwa kuwa Naibu Rais baada ya uchaguzi wa 2027 na hatimaye aibuke kuwa rais baada ya uchaguzi mkuu wa 2032 aliambia Taifa Leo kwamba “mimi niko tu lakini nilionelea nisifike na nikatuma udhuru wangu kupitia Mbunge wa Maragua Mary wa Maua”.
“Kuna taswira ambayo sitaki ijitokeze katika mikutano na ndio maana nimeona nihudumie wakazi na wenyeji wa Murang’a kwa mazingira mengine mbali na hapo,” akasema Bw Nyutu.
Bw Gachagua alitembelea Chuo Kikuu cha Murang’a siku moja baada ya Bw Nyoro kutoa hotuba ya mhadhara kwa umma sawa na hiyo katika Chuo Kikuu cha Tom Mboya kilichoko Kaunti ya Homa Bay.
Bw Gachagua akizunguka Murang’a, naye Bw Nyoro alikuwa katika mitandao ya kijamii akikumbusha wafuasi wake kwamba alikuwa katika Chuo Kikuu cha Tom Mboya na ambapo aliwashajiisha wanafunzi watie bidii ili kupata mafanikio maishani.
“Vijana walioko katika safu ya uongozi ni lazima wawe wa kuibuka na mabadiliko ya faida na wala sio kukimbizana hapa na pale na kung’ang’ania mamlaka,” akaandika Bw Nyoro katika ukurasa wa akaunti yake ya Facebook.
Aidha, Bw Nyoro alipachika ujumbe wa kiuchumi akisema kwamba soko la hisa la Kenya limekuwa thabiti “kiasi kwamba kabla ya Desemba 2024 litakuwa bora zaidi barani Afrika”.