Makala

GATHONI WA MUCHOMBA: Simba jike wa malumbano Mlima Kenya

June 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na MWANGI MUIRURI

IKIWA kuna mwanasiasa wa kike wa Mlima Kenya ambaye amejipa sifa ya malumbano na wenzake, muite Gathoni wa Muchomba ambaye ni Mwakilishi Mwanawake wa Kaunti ya Kiambu.

Bi Wa Muchomba amekuwa akikejeliwa na wengi kama “aliyejaliwa ulimi ulio na mbio ya kubingirika na ambao huenda ukamponza kisiasa.”

Hata hivyo, anasisitiza kuwa yeye ni mtetezi wa mtu mnyonge wa kawaida wa Kiambu na Kenya kwa ujumla, akisema kuwa wanaomsuta aidha wanasombwa na wivu wa ufanisi wake maishani au hawana la manufaa la kujihusisha nalo.

Ni hivi majuzi ambapo alijitokeza hadharani akiwasema wenzake wengi wa Mlima Kenya ambao wanampigia debe naibu wa rais William Ruto kutwaa urais baada ya 2013 kuwa walikuwa na njama ya kumtimua rais Uhuru Kenyatta mamlakani kupitia hoja ya kutokuwa na imani naye.

‘Mdaku sokoni’

Madai hayo yalimkera mwenzake wa Murang’a, Sabina Chege ambaye alimjibu hadharani akimtaka “athibiti huo ulimi wake ulio na mazoea ya kudaidai kiholela kiasi cha kujiangazia kama mdaku wa kawaida sokoni.”

Wawili hawa walikuwa katika taaluma moja ya utangazaji katika vituo vya redio vya kupeperusha matangazo kwa lugha ya Gikuyu.

Wamekuwa katika kituo cha Kameme, Wamuchomba pia akiwa katika vituo vya Bahaca FM na pia Inooro FM huku Bi Chege akiwa katika kituo cha Coro FM.

Kabla ya kujitosa katika ulingo wa kisiasa mwaka wa 2017 wa Muchomba alikuwa mwandalizi wa kipindi cha maridhiano cha “Muiguithania” lakini hali yake ya sasa inasemwa kukiuka mada mhiyo ya kuwaleta watu pamoja.

“Alijipa sifa hadi tukamchagua kwa kuwa alikuwa ametupa imani kuwa yeye ni wa kuridhiana mirengo katika familia. Tulidhani yeye angeishia kuwa sawa na mpaliliaji amani sugu kiwango cha Koffi Annan lakini aligeuka na kwa sasa ndiye wa kupalilia utengano na uhasama katika siasa za Kiambu na pia katika siasa za Mlima Kenya,” ateta Bi Jane Mwangi, msaidizi wa gavana Ferdinand Waititu.

Kuna mwaandishi wa habari wa Mlima Kenya ambaye anaripoti jinsi Wa Muchomba alialika kikao na wanahabari katika Kaunti hiyo lakini akachelewa kujitokeza.

“Alifika na akapata nimetoka kwa kikao hicho ili kushughulikia kazi nyingine… yeye alichukua simu yake na akapigia mkubwa wangu afisini akidai kuwa nilifika katika kikao hicho nikiwa mlevi kupindukia na ndio sababu amenifukuza kutoka hafla yake,” asema.

‘Mwongo’

Anaongeza kuwa “Bi Wa Muchomba alijiangazia tena kama aliyekuwa na mazoea ya kunena uongo kwa kuwa huyo mkubwa wangu ndiye alimwelezea kuwa huwa sibugii pombe.”

Alianza punde tu baada ya kuchaguliwa kwa kura 922, 989 kwa kutangaza kuwa mshahara wa wabunge ulifaa uongezwe.

Kilio kilichozuka kutoka kwa Wakenya, wengi katika mitandao ya kijamii na pia makala katika vyombo vya habari, kilikuwa kingi ajabu na kilichomshtua na akaomba msamaha.

Muda mfupi baadaye akanaswa na kamera za vyombo vya habari akiwa amevalia minisketi iliyosemwa kuwa fupi zaidi ya ufupi, urefu ukiwa saizi ya koti la suti ya mwanamume, na pia akaomba msamaha alipoona kuwa hakukuwa na nafasi ya kuwahimiza Wakenya wamkubali na vazi hilo lake.

Wanaume waoe wake wengi 

Muda mfupi baadaye akawarai wanaume kutoka jamii yake wawe wakioa zaidi ya bibi mmoja ili idadi ya watoto iongezeke na kuihakikishia ubabe wa kisiasa katika kura zijazo.

Akasema kuwa mpango huo wa ndoa utahakikishia wanawake wengi kupata mabwana na pia watoto wawe na uhakika wa kuwa na baba mzazi au baba mlezi.

Alishangaa ni kwanini jamii ya Wasomalia hapa nchini inazaana kwa kasi kuliko Agikuyu, akisema kuwa hilo ni hatari.

Mjadala ukatanda huku akiungwa mkono na wanaojiita wawakilishi wa jamii ya Agikuyu ambao huhubiri itikadi za mamabu ziendelee kudumishwa na Agikuyu hasa za ndoa kwa wake wengi na upande mwingine viongozi wa kanisa za Kikiristo wakimpinga kwa dhati.

Wanawake walio katika ndoa wakawa ndio hao wanapinga, wale ambao hawako katika ndoa na hujipa riziki kupitia kuchumbiana na waume za watu wakiunga, nao vijana wakigeuza mjadala huo kuwa sarakasi.

Ndiye tena alikuwa katika vichwa vya habari akisema kuwa alikuwa na ushahidi wa wabunge kupewa hongo ndani ya vyoo vya bunge ili waangushe ripoti ya sukari ya sumu iliyokuwa ikidaiwa kuingizwa hapa nchini kimagendo.

Wa Muchomba alizaliwa katika kijiji cha Komothai kilichoko katika Kaunti ya Kiambu, mamake akiwa na watoto wanne lakini familia yao ya ndoa ya mitaara ikiwa na wengine 11.

Utata kwa familia

Haijulikani ni wapi historia ya Wa Muchomba ilihitilafiana na hali kwamba mamake huishi katika Kaunti ya Murang’a na ambapo hivi majuzi kuliandaliwa mazishi ya nduguye ambaye baada ya kuonekana katika baa moja ya eneo hilo akilewa, mwili wake ndio uliishia kufika katika lango la boma lao na ambapo mamake Wa Muchomba ndiye alihutubia waandishi wa habari akielezea kuhuzunishwa na utata wa mauti hayo.

Aliyekuwa Mbunge wa Maragua, Elias Mbau anakumbuka akishindana na Wa Muchomba kutwaa wadhifa huo katika uchaguzi mkuu wa 2007, wakati huo mwanadada huyu akiwa katika mrengo wa uwaniaji wa urais wa Raila Odinga.

Katika mahojiano yake na vyombo vya habari, Wa Muchomba hukemea babake mzazi kama “aliyekuwa mlevi kiholela na aliyekosa maarifa ya malezi” huku akiachia mzigo wa malezi mamake Wa Muchomba.

Anasema kuwa kero hilo la babake lilimuadhiri maishani kiasi kwamba aliamua kuwa kamwe hatawahi kuolewa, na ndiye huyo akiwataka sasa wanaume waoe wanawake wengi.

Licha ya masaibu yake ya malezi, aliishia katika shule ya upili ya Precious Blood Riruta, na nusura aondoke shuleni kufuatia ukosefu wa karo lakini akapata ufadhili wa mhisani.

Akiwa wa miaka inayoelekea 47 kwa sasa, Wa Muchomba alipata kazi ya ualimu katika Shule ya karibu na kwao nyumbani na ambayo ni Makuyu iliyoko Kaunti ya Murang’a.

Alisomea shahada ya ualimu katika chuo kikuu cha Nairobi na ambapo pia alikuwa akichuuza huduma za ususi nywele na pia bidhaa za urembo ili kujipa mapeni mfukoni.

Katika makala ya hivi karibuni na vyombo vya habari, Wa Muchomba alikemea ulevi kiholela, akiongeza kuwa “hakuna anayekukataza kunywa pombe kujiburudisha. Hata mimi hutumia pombe lakini haifai kukugeuza kuwa mtumwa.”