Gharama ya juu ya mahari inavyozimia vijana ndoto ya ndoa
Na MWANGI MUIRURI
IKIWA kuna safu moja ya kimaisha ambayo inawalemea kuwapa imani na ndoa vijana wengi katika jamii, ni mahari.
Aliyekuwa mkuu wa kanisa katoliki katika Kaunti ya Nyeri, Askofu mstaafu Peter Kairo anasema kuwa “mahari imegeuzwa kuwa biashara ya kutajirisha wakwe kiasi kwamba vijana wengi hawana imani na ndoa.”
Anasema kuwa mahari iliwekwa katika tamaduni kama shukran kwa wazazi wa msichana anayepozwa, “lakini leo hii ni biashara ambayo hata inaweza ikasajiliwa katika soko la hisa.”
Anasema kuwa kunafaa kuwekwa mikakati ya kuwapa vijana hasa walio na pesa kidogo maishani kujiamini kwa kuwapa matumaini kuwa kesho yao wanaweza wakapata pesa za kulipa mahari.
“Lakini leo hii unapata kijana amesononeka kwa kuwa gharama za ndoa zimeenda juu lakini sio kwa kiwango kile cha kawaida bali ni kwa kusukumwa na wanaooza mabinti zao,” asema.
Mshirikishi wa Shirika la Wanawake waelimishaji Barani Afrika, Cecilia Wanjiku anasema kuwa katika jamii ya Agikuyu, vijana wengi hawaoi kwa kuwa gharama ya ndoa imetinga zaidi ya Sh moja Milioni.
“Ukienda kuomba harusi, utahesabiwa gharama nyingi na mashemeji hao watarajiwa. Ukishapita kigezo hicho, gharama za harusi ya hadhara zinakungoja, hali ambayo imewaelekeza hata wengi wa vijana kutekeleza ndoa zao kwa njia za kujificha,” asema.
Anasema kuwa ukifika ni wakati wa kuhesabiwa gharama za mahari, unapata kuwa kijana masikini amehesabiwa gharama ya msichana huyo kana kwamba ni dhahabu sokoni.
“Ndio sababu wengi wa vijana siku hizi wanatoroshana na wasichana na kuanza ndoa zao bila hata kuwafahamisha wazazi kwa kuhofia gharama,” ateta.
Anasema kuwa mahari ya Agikuyu kwa mfano huwa ni pamoja na pesa taslimu zisizopungua Sh100, 000 za kuwaandalia karamu marafiki wa kijiji cha msichana huyo, zawadi za Sh100, 000 kwa wakwe na pia pesazingine kiwango cha maelfu za kupishwa nyumbani kwa wakwe hao.
“Shida kubwa sasa hutokea katika gharama ya msichana ambayo husemwa ni mbuzi 100 na ambao kulingana na hadhi ya familia, mbuzi mmoja huwekewa thamani ya kati ya Sh5, 000 na Sh15, 000. Hii ina maana kuwa bei ya msichana huyo ni kati ya Sh500, 0000 na Sh1.5 Milioni bila kujumlisha zile gharama za mwanzo,” asema Bi Wanjiku.
Anasema kuwa ndiyo sababu vijana wengi katika jamii wamezama katika ulevi kwa kuwa “ukioleka kwa ulevi, gharama ni chache na kuna kule kuzimia kwa mawazo na unajipa imani ghushi ya kimaisha.”
Na huku pombe haramu ikilaumiwa kwa kudhoofisha nguvu za kiume sasa Bi Wanjiku anasema kuwa Fawe imezindua harakati za kuwatuza wanaume ambao watakoma tembo, kuoa na kisha kupachika wake zao mimba.
Mashujaa hao watatunukiwa vifaa vya nyumba na pia kupimwa suti huku pia wakipewa kitita cha pesa cha kugharamia manguo ya mtoto atakayezaliwa.
Anasema kuwa Fawe inalenga kuwapa vijana motisha ya kuoa na ambapo itawapa uhamasisho kuhusu njia zingine nyingi za kuzindua familia zao bila kujipa stresi za kuhesabiwa gharama za juu.
“Kuna harusi za afisi za kisheria na pia kwa makamishna wa Kaunti. Kuna ndoa za kienyeji na pia kuna ndoa zile za kuishi pamoja bila kujificha mkingoja mkusanye mali ya kupeleka kwa wakwe….Sio lazima tufuate ule utaratibu wa kuhesabiwa gharama hata kabla ya kujaribu kama mnaweza mkawiana katika ndoa,” asema.
Bi Wanjiku anasema kuwa mpango huo utawalenga wanaume ambao wamefikisha umri wa miaka 30 na ambao hawajawahi kuoa na ni walevi.
“Hii ni kwa sababu mpango huu unaweza tumiwa vibaya na wanaume ambao tayari wameoa kwa kuwapachika mimba mabibi zao kiholela ili watuzwe,” akasema Bi Wanjiku.
Mpango huu umewadia wakati makasisi wengi makanisani wamekuwa wakilalamika kuwa wafuasi wao wamekoma kuleta watoto wapya duniani kinyume na sheria za Mungu kuwa tujaze ulimwengu.
Mwenyekiti wa Kanisa la Presybeterian la Mbogo-ini Bw Titus Njuguna aliteta katika ibada kuwa “Vijana kutooa na walio oa kukosa kuzaa kumezua wasiwasi mkubwa katika maeneo mengi ya Mkoa huu. Nataka kuwashukuru wale ambao wameshikilia hadhi ya eneo letu kwa kuendelea kujizatiti na kutomboa kutuzalia watoto wengine ingawa idadi yao ni chache sana.”
Hali hii inahusishwa na gharama za juu katika ndoa na ambazo huchochewa na mtazamo wa kibiashara katika kuwaoza mabinti katika jamii.