Makala

Gharama ya maisha ilifanya maelfu kupoteza ajira 2024

Na BENSON MATHEKA December 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

MWAKA huu notisi za kufuta wafanyakazi zilisheheni huku waajiri wakilalamikia ongezeko la gharama za uendeshaji biashara.

Waajiri wengi walitaja ushuru wa juu na mazingira magumu ya kiuchumi katika notisi za kufunga kampuni au kupunguza wafanyakazi.

“Kufuatia kupungua kwa biashara kutokana na changamoto kubwa za kiuchumi, ambazo zimefanya gharama ya kuendesha biashara zetu kuwa kubwa mno na hivyo kupunguza mapato, tunasikitika kushauri Wizara ya Leba kuhusu nia ya kampuni kusitisha nyadhifa ambazo hazihitajika,” ilisema barua kutoka kampuni ya ulinzi ya G4S mnamo Novemba 4, 2024, kwa Wizara.

Barua hiyo ilifafanua kuwa hatua ya kusitisha nyadhifa ingefanya kampuni kufuta zaidi ya wafanyakazi 400.Notisi kutoka kwa kampuni nyingine, Tile & Carpet, pia ilitoa sababu sawa na hizo.

changamoto za kiuchumi

“Kufuatia kupungua kwa mahitaji ya uzalishaji, changamoto za kiuchumi na mabadiliko ya kimkakati, imekuwa muhimu kupunguza shughuli katika kiwanda chetu cha uzalishaji ili kudumisha uwezo wa muda mrefu wa kampuni,” ilieleza taarifa ya kampuni ya Tile & Carpet ambayo huunda vigae na bidhaa zingine za kubandikia ukutani na sakafuni.

Kampuni ya kutengeneza magari Mobius pia ilitangaza mipango ya kufungwa mwezi Agosti, kabla ya mwekezaji kuingilia kati kuokoa kampuni hiyo, ambayo imekuwa ikihangaika kwa miaka mingi, isizame.Matukio haya yanasimulia taswira tofauti kabisa na kauli za Rais William Ruto kwamba “Kenya iko wazi kwa biashara” kila anapokutana na wawekezaji.

Inatarajiwa uchumi wa Kenya umekua kwa asilimia 5.2 mwaka huu wa 2024 – juu ya asilimia 2.6 ya wastani wa kimataifa kulingana na Benki ya Dunia.Lakini wafanyabiashara hawafurahii ukuaji huu kwa vile wanakabiliana na riba ya juu na ongezeko la gharama ya uzalishaji kutokana na ushuru mwingi.

Katika sherehe za hivi majuzi za Muungano wa Sekta ya Kibinafsi ya Kenya za kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa, Rais Ruto alisema, Kenya inavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, inachochea ukuaji wa uchumi na kuunda nafasi za kazi.Alisema lengo ni kukuza uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni hadi kufikia dola bilioni 10 (Sh1.3 trilioni) kila mwaka ifikapo 2027.

Mageuzi ya biashara

“Juhudi hizi tayari zinazaa matunda, na zaidi ya Sh230 bilioni za uwekezaji zimepatikana kupitia uboreshaji wa mageuzi ya biashara.Kenya sasa imejiweka katika nafasi nzuri kama kitovu cha uwekezaji katika kanda, ikitumia eneo lake la kimkakati, mfumo thabiti wa uvumbuzi, na ushirikiano thabiti wa sekta ya umma na binafsi ili kufungua fursa na kuendeleza ustawi wa pamoja,” alisema Rais.

Hata hivyo hatua ya kampuni kubwa za humu nchini kutangaza mpango wa kufuta mamia ya wafanyakazi imezidi kufichua hali duni ya kiuchumi inayokumba maelfu ya biashara, kutokana na kupanda kwa ushuru na mauzo kushuka.

Mbali na G4s na Tile & Carpet, kampuni ya kimataifa ya Procter & Gamble (P&G), ilitoa ilani za kufuta wafanyakazi zikilaumu ughali wa kufanya biashara, japo mamia ya kampuni zingine zimekuwa zikiwatimua wafanyakazi wao mwaka huu, hali ambayo imeathiri maelfu ya watu na kupunguzia serikali mapato.

Procter & Gamble (P&G), kampuni ya Amerika inayotengeneza bidhaa za usafi kama sodo ilitimua zaidi ya wafanyakazi 800 na kuondoka nchini Desemba mwaka huu .Sawa na G4S na Tile and Carpet, kampuni ilitaja gharama ya juu ya kufanya biashara nchini.

Utafiti wa hivi karibuni kutoka kwa Benki Kuu ya Kenya (CBK) ulionyesha kuwa, mwaka huu pekee, asilimia 42 ya kampuni zimetimua wafanyakazi wa vibarua, asilimia 31 ya kampuni zimetimua wafanyakazi wa kandarasi na asilimia 25 ya kampuni zimefuta wafanyakazi wa kudumu.

Futa vibarua

Kulingana na utafiti huo uliohoji wakuu wa kampuni katika sekta tofauti, hii ni kumaanisha kuwa, moja kati ya kila kampuni nne nchini zimefuta wafanyaklazi wa kudumu, huku takriban nusu ya kampuni zikifuta wafanyakazi wa vibarua.

Utafiti huo uliofanywa Septemba ulionyesha kuwa, japo hali katika sekta ya benki imekuwa nafuu huku zikizidi kuajiri, sekta zingine za kiuchumi zimekuwa zikitimua wafanyakazi kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

“Kampuni (kando na benki) zilitarajia kuwa gharama kubwa ya uzalishaji, matumizi mengine, faida ya chini, kufifia kwa biashara, kupungua kwa mapato na gharama ya juu ya utendakazi vimepunguza haja ya kuajiri wafanyakazi 2024,” ripoti ya utafiti huo ilisema.