Makala

GWIJI WA TAARAB: Khadija Kopa

December 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 5

Na CHRIS ADUNGO

WATAKAPOORODHESHWA wasanii ambao wamechangia pakubwa katika makuzi ya Kiswahili ndani na nje ya janibu za Afrika Mashariki, jambo la hakika ni kwamba jina la mwanamuziki Khadija Omar Abdallah Kopa halitakosekana katika orodha hiyo.

Mwangwi wa kusisitiza umuhimu wa maadili katika masuala ya unyumba kwa matumizi ya Kiswahili fasaha na wingi wa busara ni jambo ambalo Khadija amepania mno kuliakisi katika nyingi za nyimbo zake.

Huo ndio upekee wa Khadija – gwiji wa kutumia sana methali, mafumbo na misemo katika uimbaji na utunzi wa nyimbo za Taarab.

Kupitia Ogopa Kopa Band, Khadija anatazamiwa kunogesha hafla ya ‘Toroka Uje Night’ katika Sharks Club iliyoko mkabala na Shelly Beach Hotel Likoni, Mombasa mnamo Disemba 24.

Siku moja baadaye, malkia huyu wa mipasho anatarajiwa kuwatumbuiza wapenzi wa Taarab katika Garden Square, Ukumbi wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC), Nairobi kabla ya kuelekea Moshi, Tanzania kuwaburudisha mashabiki katika hoteli ya Aventure Club mnamo Disemba 26, 2019.

Katika ziara hizi, Khadija ataandamana na kundi lake zima la Ogopa Kopa Classic ambalo linawajumuisha wasanii 15, wakiwemo wanawe Omari Kopa na Black Kopa wanaojivunia kucharaza wimbo maarufu wa ‘Fagilia’.

Kinachomtofuatisha Khadija na wasanii wengine wa muziki ni upevu wa umilisi wake wa Kiswahili na upana wa ujuzi wa kufumbata ujumbe mzito kupitia tamathali mbalimbali za usemi.

Kwa kuzingatia ujumbe uliomo katika tungo zake, ushairi wa Khadija una mawanda mapana zaidi kwa sababu anazungumzia mambo mbalimbali yanayoakisi taratibu za kila siku katika maisha ya binadamu wa kawaida.

Suala la mapenzi silo alilolipa kipaumbele pekee, bali ametunga pia nyimbo zinazozungumzia kwa kina masuala yanayohusu maendeleo ya jamii kitamaduni na mahusiano kati ya binadamu na mazingira yake.

Khadija anasisitiza kwamba muziki si chombo cha kuburudisha tu; bali pia kuonya, kukosoa, kukumbusha na kuadilisha jamii.

Nafasi ya Kiswahili ni dhamira mojawapo muhimu zinazojadiliwa na Khadija katika ushairi wake wenye ubunifu na ufundi wa viwango vya juu. Ni wazi kuwa msanii huyu amepania kukikuza Kiswahili si kupitia kwa masimulizi ya kifasihi tu, bali hata katika vipengele vyake kama vile msamiati na sarufi.

Kwa mujibu wa Mohamed Kabale Sadia ambaye ni promota wa muziki wa Taraab nchini Kenya, nyimbo za Khadija zinaashiria kwamba Kiswahili kimekua zaidi kiasi cha kutumiwa kuendeshea shughuli zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika.

Anasema kiini cha mapenzi ya Khadija kwa Taarab ni thamani ya Kiswahili ambacho kulingana naye, ni kiwanda kikubwa cha maarifa, ajira na uvumbuzi.

MAISHA YA AWALI

Khadija Kopa alizaliwa mnamo 1963 katika mtaa wa Makadara Kisiwani Zanzibar; na ni mtoto wa pekee katika familia ya Kopa. Amejaliwa watoto wanne na wajukuu wawili. Alianza kazi ya sanaa mnamo 1990 katika Kikundi cha Culture Musical Club.

Zaidi ya kujihusisha sana na muziki, Kopa pia ni mama wa nyumbani, mfanyabiashara maarufu na mwanaharakati wa kisiasa nchini Tanzania. Chama Cha Mapinduzi nchini Tanzania (CCM) kiliwahi kumteua kuwa mbunge.

Khadija alikuwa akipenda sana kuimba tangu akiwa mtoto mdogo akisomea madrassa Zanzibar. Akiwa chuoni (madrassa) alikuwa msomaji mzuri wa Qaswida, halafu vilevile alipokuwa Young Pioneer, alikuwa kwenye kikundi cha kwaya.

Mbali na kuigiza na kushiriki tamasha za kila sampuli za kitamaduni, alijishughulisha sana na masuala ya upigaji ngoma na uchezaji wa ala mbalimbali za muziki (filda, dumbaki, ganuni, kinanda na dabalibesi) akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi.

Shule yao ilikuwa bingwa wa kwaya na tamasha za kitaifa za muziki na drama nchini Zanzibar. Aliendelea kuichapukia sanaa hii iliyoanza kujikuza mapema ndani yake hadi katika shule ya upili.

Siku moja alikuwa amekaa huku akiiga mtunzi wa mmojawapo wa nyimbo alizozipenda sana. Akapita babu yake aliyekuwa katika kikundi cha Culture Musical Club cha Zanzibar. Akamsifia mjukuu wake kwamba anajua kuimba sana.

Basi akachukua hatua ya kuandika barua kwa niaba yake bila ya kumshauri, akaipeleka Culture Musical Club kuomba ajiunge nao.

Khadija ameshirikiana na waimbaji wengine kama vile Mwanamtama Amir, marehemu Leila Khatib, Abdul Misambano, Diamond Platnumz, Abdul Misambano, Ali Star, Mzee Yusuph na wanabendi mashuhuri wa Tanzania One Theatre (TOT) kuporomosha nyimbo ambazo zimewahi kutamba sana katika ulimwengu wa Taarab.

Baada ya kuhudumu Culture Musical Club kwa kipindi kirefu, Khadija alijiunga na Muungano Taarab Group kisha East Africa Melody.

Kwa pamoja na Captain Komba, walishirikiana kuunda Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT) chini ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Lengo lao kuu kwa wakati huo lilikuwa ni kutambua, kukuza na kuwalea wasanii mbalimbali waliojivunia utajiri wa vipaji vya utunzi, uimbaji, uchezaji ala na uigizaji.

Khadija kwa sasa anamiliki Bendi ya Ogopa Kopa Classic aliyoianzisha mnamo 2017. ‘Ngwinji’ ndio wimbo uliomtambulisha na kuchangia sana kuinuka kwake akiwa katika Kundi la Muungano ambalo pia lilimpa jukwaa la kufyatua wimbo ‘Mtie Mumeo Kamba’. Aliucharaza wimbo ‘Mwanamke Mambo Utapenda’ akiwa katika Bendi ya East Africa Melody.

Vibao vyake vya hivi karibuni zaidi ni ‘Unaringa Umepima’, ‘Nalijua Jiji’, ‘Top In Town’, ‘Mjini Chuo Kikuu’, ‘Lady With Confidence’, Mama Mkubwa’ na ‘Wigi Linawasha’.

Khadija anasisitiza kuwa kiini cha kutumia misemo ya Kiafrika katika utunzi wa mashairi yake ni jitihada za kimakusudi za kujaribu kuinua utamaduni wa ‘watu weusi’ pamoja na kushikilia mhimili wa itikadi, mila na desturi zinazofungamana na mazingira yao.

Khadija anaamini kwamba huwezi kuwa na matumaini ikiwa siku zote vijiwe vyako ni vile vinavyopania kuyadunisha malengo yako ya baadaye.

“Ukiambatana na watu waliokata tamaa maishani, baada ya muda fulani, utajikuta ndivyo. Jenga ukuruba na watu walio na mtazamo chanya na wenye idili ya kufanikiwa. Marafiki wema ni wale wanaokuhamasisha unawiri na kukuchochea usonge mbele zaidi.

“Wanaotamani uishi maisha yanayompendeza Mungu siku zote. Waaminifu na wenye kutunza siri. Wanaokutia moyo kila unapozungumza nao. Jitafutie marafiki wachache waadilifu ambao watakushika mkono wakuinue juu. Kataa kuamini kwamba huna ubora wowote. Wapo wengi wanaokutamani na kuomba siku zote kuwa jinsi ulivyo,” anasisitiza Kabale.

HISTORIA YA TAARAB

Taarab asilia ilibisha hodi ndani ya Kisiwani Zanzibar mnamo 1870 kutokea katika nchi za Uarabuni. Umaarufu wake ulikuwa ni katika sehemu maalumu za kuwastarehesha viongozi au watawala ambao wengi wao walikuwa na asili ya Kiarabu.

Jambo hili lilichangia nyimbo hizo ziimbwe kwa Kiarabu. Waimbaji na vifaa vililetwa Zanzibar kutoka Urabuni, hasa nchi za Yemen na Misri. Neno Taarab lina asili ya Kiarabu lenye maana ya raha, starehe na furaha (Yego, 2011).

Nyimbo za Taarab zilianza kuimbwa kwa Kiswahili katika miaka ya 1990. Vipaji vya Wazanzibari vimechangia makuzi ya Taarab kiasi kwamba leo hii, baadhi ya wataalamu wanadiriki hata kuandika kuwa, asili ya Taarab ni Uswahilini na makao makuu yake ni Zanzibar.

Kwa mfano Mgana (1996:125) anafafanua kuwa “Zanzibar ndicho Kisiwa kilichodaiwa kuwa chimbuko la muziki wa Taarab yapata miaka 100 iliyopita na ndio makao makuu ya muziki huo”.

Taarab asilia iliingia Zanzibar ikiwa na lengo kuu la kumpatia burudani mfalme wa wakati huo Seyyid Said Bin Sultan na waandamizi wake, pale alipohitaji raha na starehe ya kupumzisha akili yake wakati wa jioni na usiku.

Mtawala huyu alitamani zaidi burudani, starehe na anasa. Haya yanathibitishwa na Sheikh Shaib aliyenukuliwa na Khatib (1992) akisema, Sayyid Said alikuwa mtu wa anasa na starehe na alikuwa hawezi kuishi bila ya kupata muziki wa Taarab.

Hivyo, yeye ndiye aliyeanzisha muziki wa Taarab nchini Zanzibar na baadaye ukaanza kusambaa hadi Tanganyika.

Miongoni mwa viashiria vya ukomavu wa Taarab asilia Zanzibar ni uanzishaji wa vikundi vingi ambavyo vilivuma na kuwa na uwezo mkubwa katika ulimwengu wa Taarab. Vikundi vyenyewe ni pamoja na Naad Ikhwan Swafaa (1905) pamoja na Nadi Suub (1908).

Kadri siku zilivyosonga, vikundi vingine vilianza kuchipuka. (Mgana, 1991, Farhan, 1992 na Khatib, 1992:27) wanaelezea kwamba, mnamo 1945, kuliibuka vikundi vya wanawake pekee; mfano wa vikundi hivyo ni Royal Airforce, Navy, Nurul–Uyuni, Sahibel-An na Banati el Kher.

Vile vile, kuna vikundi vingine vilikuwa na mchanganyiko wa wanawake na wanaume; kwa mfano, Michenzani Social Club (1954), Kwaalimsha Social Club, Miembeni Club (1957), Yaasu Social Club (1960), Ghazy (1961), Kiembe Samaki Musical Club (1963), Culture Musical Club (1965), Sabran Jamil (1985), Vikundi vya Majeshi (1985), Ilyas, Twinkling Star na Bwawani (1989). Waimbaji mashuhuri kwa wakati huo walikuwa ni Siti Binti Saad, Mbarouk Suwed, Bakari Abedi, Maalim Shaaban na wengineo (Rajab, 2016).

Baada ya muziki wa Taarab kusambaa kwa kiasi kikubwa, ulivuka mipaka ya Visiwa na kuingia Tanzania Bara katika sehemu za Dar es Salaam, Bagamoyo hadi Tanga ambapo mwimbaji Shakila Said alizaliwa. Pia muziki huu ulivuka mipaka ya nchi na kuvuma sana sehemu za Lamu na Mombasa nchini Kenya.

Aidha, muziki wa Taarab uliweka maskani yake katika mataifa mbalimbali kama vile Uganda, Rwanda na Burundi.