Makala

GWIJI WA WIKI: HEZEKIEL PETER GIKAMBI

March 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 4

Aliyekuwa meneja wa SwahiliHub, tovuti ya Nation Media Group, Peter Gikambi (kulia) amkabithi tarakilishi meneja wa E-Kitabu Will Clurman ambazo zilitolewa kwa hisani ya Taifa Leo na Swahili Hub na kampuni ya Nation Media Group kuwatuza wanafunzi bora wa Kiswahili na shule alizipokea kwenye jumba la habari la Nation Centre Jijijini Nairobi, Septemba 1, 2015. Picha/ ANTHONY OMUYA (NAIROBI)

Na CHRIS ADUNGO

KUKIMILIKI Kiswahili ni sawa na kuwa na malighafi au mtaji sawa na ule alionao daktari, wakili, rubani au mhandisi. Muhimu zaidi ni kufuata msukumo wa ndani ya nafsi hadi lengo lako lifikiwe.

Mungu ana mbinu na uwezo wa kumsaidia binadamu anayewafaa wenzake. Vitu vilivyo bora zaidi maishani hutolewa bila malipo. Mtu hawezi kabisa kukadiria thamani ya afya, uzima na uhai alionao.

Kufaulu maishani na kitaaluma kunamhitaji mtu kuwa mwepesi wa kujifunza kutoka kwa kila anayetangamana naye. Jisake mara kwa mara ili ujue ilipo ari yako.

MAISHA YA AWALI
Bw Hezekiel Peter Gikambi alizaliwa katika kijiji cha Muutine, eneo la Igembe, Kaunti ya Meru akiwa mtoto wa nne kati ya wanane katika familia ya Mama Jennifer Thirindi na marehemu Mzee Peter M’Ituiri Nabea.

Baada ya kupata elimu ya msingi katika Shule ya Kaongo Ka Mau (KK Mau) kati ya 1979 na 1986, alijiunga na Shule ya Upili ya Burieruri mnamo 1987 na kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mwishoni mwa 1990.

Mbali na mwalimu Mugambi aliyemchochea kuandika Insha bora zilizompa tuzo nyingi akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, anatambua pia mchango wa walimu Jeff Irware na Bw Muroki katika kumwelekeza vilivyo na kumhimiza ajitahidi masomoni akiwa katika shule ya upili.

Gikambi alivutiwa sana na watangazaji wa redio za BBC na KBC; hasa Willy Mwangi, Tido Mhando, Mohamed Juma Njuguna na Anderson Kalu. Alipokuwa darasa la tatu, alikuwa tayari ameanza kuiga jinsi walivyokuwa wakitangaza.

Baada ya KCSE, alipata msukumo wa kutaka kujitosa kikamilifu katika ulingo wa Kiswahili na kuwa ama mwanahabari, mhariri au mwandishi.
Hizi ni taaluma alizozipenda ingawa tangu utotoni mwake, alitaka sana kuwa daktari.

 

USOMI
Mnamo 1992, Gikambi alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi, Bewa la Kikuyu kusomea ualimu (Kiswahili na Historia).

Miongoni mwa wahadhiri waliofanikisha safari yake ya elimu chuoni ni Profesa Rayya Timammy, Profesa John Habwe, Dkt Zaja Omboga, Dkt Swaleh Amiri, Dkt Ayub Mukhwana, Dkt Jefwa Mweri na marehemu Profesa Jay Kitsao ambao mbali na kumpokeza malezi bora zaidi ya kiakademia, pia walimrithisha ilhamu ya kukipenda Kiswahili.

Mnamo 2001, Gikambi alijiunga na Chuo cha Kimataifa cha Cambridge, Uingereza kusomea Stashahada katika usimamizi wa mauzo na uvumishaji wa bidhaa.
Alifuzu mwishoni mwa 2002, na mnamo 2011, alisomea Diploma katika Uanahabari na Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Akiwa Nation Media Group (NMG), alienda Afrika Kusini mnamo 2013 kusomea kozi ya Usimamizi wa Habari za Kidijitali katika Chuo Kikuu cha Rhodes katika Taasisi ya Sol Plaatje Media Leadership Institute mjini Grahams Town.

Ilipofika Septemba 2013, Gikambi alirejea katika Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea Shahada ya Uzamili. Alifuzu 2015 baada ya kuwasilisha Tasnifu Teknolojia ya Lugha katika Utafiti wa Kiswahili: Kifani cha Mradi wa SALAMA chini ya usimamizi wa Dkt Zaja Omboga na Profesa Iribe Mwangi.

Mnamo 2016, aliandaa Pendekezo la Utafiti lenye mada Mabadiliko katika Tasnia Ya Uanahabari: Uchanganuzi wa Diskosi kwa Lugha ya Kiswahili na Teknolojia Nchini Kenya kwa minajili ya Shahada ya Uzamifu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Leipzig, Ujerumani chini ya uelekezi wa Profesa Dkt Rose Marie Beck. Anaendelea na utafiti huo katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Bw Ezekiel Peter Gikambi (kulia) akiwa kwa picha na meneja wa E-Kitabu Will Clurman na washindi wa insha nchini katika ukumbi wa Sarit Centre, Septemba 23, 2015. Picha/ ANTHONY OMUYA (NAIROBI)

UALIMU
Baada ya kufuzu mnamo 1996, Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma Gikambi kufundisha katika shule ya upili ya Kitany, eneo la Keiyo, Kaunti ya Elgeyo-Marakwet.

Aliwachochea wanafunzi wake kushiriki zaidi mashindano ya muziki na uigizaji hadi kufikia kiwango cha kitaifa. Isitoshe, aliteuliwa kuwa mlezi wa masuala ya drama na vyama vya Uanahabari na Burudani shuleni Kitany.

Alishirikiana sana na mwalimu mwenzake shuleni humo, Bw Joseph Ngure kuandika makala mengi yaliyochapishwa katika kumbi mbalimbali za gazeti hili.
Akifundisha shuleni Kitany, Gikambi alishiriki mipango ya marehemu Dkt Abel Gregory Gibbe kuendesha Semina Kuu za Kiswahili (SEKUKI) katika sehemu mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.

Mnamo 2003, Gikambi alijiunga na Shule ya Upili ya Riara Springs Girls, Nairobi. Akiwa huko, alihariri vitabu Darubini za Kiswahili (F.M Kagwa, Phoenix) na Heri Subira cha (Omar Babu, Oxford University Press) na kuanza kuandika msururu wa vitabu Johari ya Kiswahili (1-4) vinavyosomwa nchini Tanzania.

Isitoshe, alishiriki pia utunzi wa majaribio ya mitihani ya KCSE inayochapishwa na gazeti hili. Pia alitafsiri makala na ripoti nyingi za mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

 

UANAHABARI
Baada ya kufundisha Riara Springs kwa miaka saba, Gikambi alijiunga na kampuni ya Habari na Mawasiliano ya NMG mnamo 2008 akiwa Mhariri wa Makala ya Elimu katika gazeti la Taifa Leo.

Mwaka mmoja baadaye, alianzisha Shindano la Uandishi wa Insha linaloendeshwa hadi sasa na gazeti hili miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi na upili nchini.

Hadi alipoondoka NMG mnamo 2016, Gikambi ndiye aliyekuwa Meneja Msimamizi wa tovuti ya Swahilihub aliyoizindua rasmi mnamo 2012 katika Kongamano la 25 la Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Bayreuth, Ujerumani.

Wazo la kuanzishwa kwa Swahilihub mnamo 2010 lilikuwa pendekezo lake Gikambi kwa lengo la kujenga jukwaa la kidijitali la picha, video, makala na habari za Kiswahili.

 

UANDISHI
Gikambi anaamini kwamba safari yake katika uandishi ilianza akiwa tineja.

Insha alizozitunga nyakati hizo zilimpandisha katika majukwaa anuwai ya tuzo za Kiswahili. Aliandika michezo na mashairi kwa ajili ya mashindano mbalimbali alipokuwa akifundisha katika shule za upili za Kitany na Riara Springs. Mashairi yake yalitia fora katika tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Ameandika vitabu vingi vya Kiswahili vikiwemo mkusanyiko wa Peak Encyclopedia KCSE Compulsory Subjects uliochapishwa na kampuni ya EAEP mnamo 2006.

Pia alishirikiana na Profesa Collins Mumbo na Dolaria Kyando kuandaa msururu wa vitabu Johari ya Kiswahili vilivyochapishwa na kampuni ya Ujuzi Book Ltd mnamo 2009.

Mbali na kuandaa Miongozo ya vitabu vya Fasihi ya Kiswahili ambavyo vimewahi kutahiniwa katika kiwango cha KCSE, anajivunia pia kuandika vitabu Safari ya Serengeti na Ningependa Kusahau vilivyochapishwa mnamo 2010.

Mnamo 2014, kampuni ya Longhorn ilimchapishia kitabu SmartScore Encyclopaedia kwa Darasa la 8.

 

UHADHIRI
Kwa sasa, Gikambi anafundisha kozi ya Uanahabari na Mawasiliano kwa wanafunzi wanaosomea kiwango cha umahiri katika Chuo Kikuu Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA). Pia anawafundisha kozi ya Mawasiliano ya Kibiashara kwa wanafunzi wa Shahada ya Kwanza chuoni humo.

Amewaelekeza wanafunzi wengi wa Shahada ya Kwanza kutoka Vyuo Vikuu vya Multi-Media na Moi (Bewa la Nairobi) katika kozi za Mawasiliano, Sintaksia ya Kiswahili na Historia ya Kiswahili.

 

UFANISI
Anapojitahidi kupiga hatua, Gikambi anajivunia kuwahi kufundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za juu katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Mbali na kuandika makala ya kitaaluma katika majarida mbalimbali, anajivunia pia kuandaa, kuhudhuria na kuwasilisha katika makongamano mengi kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili katika viwango vya kitaifa na kimataifa.

Amekuwa mjasiriamali na mshauri wa tafsiri, mawasiliano na uhariri wa machapisho ya Kiswahili katika kampuni tofauti za uchapishaji nchini Kenya na Tanzania, kwa wanasiasa,mashirika mbalimbali kutoka Ulaya na Marekani na katika Benki ya Dunia.

Amehariri miswada mingi ambayo sasa ni vitabu mashuhuri katika ulimwengu wa taaluma za Kiswahili. Kwa sasa, anajishughulisha na kampuni ya Fasiri Communications ambayo mbali na kuchapisha vitabu, pia hutoa huduma za uhariri, tafsiri na ukalimani.

Fasiri Communications imewahi kuchapisha Wasifu wa Burudi Nambwera Baba wa Mayatima (kitabu cha Paul H. Boge kilichotafsiriwa na Ken Walibora mnamo 2016), Mwongozo wa Kigogo na Mwongozo wa Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine.

Pamoja na mkewe, Bi Kawira Gikambi, wamejaliwa watoto watatu: Furaha, Faraja na Fadhili.