Makala

GWIJI WA WIKI: Mwalimu wa Kiswahili mwenye tajriba pevu ya uchoraji

July 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

KUJITUMA bila ya kukata tamaa ni siri kubwa ya kufanikiwa maishani na kitaaluma. Hakuna kitu kinachoridhisha zaidi nafsi ya mwenye kutenda jambo kuliko kuwafanyia watu kazi nzuri itakayodumu katika kumbukumbu zao kutokana na jinsi itakavyoyaathiri maisha yao na mikondo ya fikra zao.

Pania sana kutenda wema siku zote kwa sababu hifadhi ya jina zuri katika fikra za wateja wako ndiyo malipo bora zaidi utakayojipa. Thamani yake yashinda pesa na sifa ambavyo ni vitu vya msimu!

Upeo wa mafanikio ya mtu hutegemea pakubwa juhudi zake binafsi, nidhamu, uvumilivu na imani aliyonayo kuhusu jambo.

Kujiamini ni mwanzo bora katika kulijaribu jambo lolote duniani. Mungu alipokuumba, alikupa kipaji, uwezo wa kukitumia vyema kipawa hicho na jukwaa la kuwadhihirishia walimwengu talanta yenyewe.

Huu ndio ushauri wa Bw Paul Wahinya – mshairi shupavu, mkufunzi wa Kiswahili na mchoraji mwenye tajriba pevu na ya siku nyingi katika ulingo mpana wa sanaa.

Amehudumu katika Chuo cha Walimu cha Nakuru kwa zaidi ya mwongo mmoja akiwa mwalimu na mwanzilishi wa somo la Uchoraji kama sanaa yoyote nyingine.

Wahinya amewaona wengi wakipitia katika mikono yake na kufanikiwa katika nyanja mbalimbali za maisha. Hakuna zaidi ya hiki ambacho humpa msukumo, ilhamu, kariha na mshawasha wa kukiimarisha kipaji chake kila siku kadri anavyojitahidi kujiboresha kitaaluma.

 

MAISHA YA AWALI

Wahinya alizaliwa katika miaka ya sabini katika eneo la Kimathi, Kaunti ya Nakuru akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto watano. Alijiunga na Shule ya Msingi ya Baharini, Nakuru mnamo 1972 na kuufanya mtihani wa CPE mwishoni mwa 1980.

Hatimaye, alijiunga na Shule ya Upili ya Menengai High, Nakuru mnamo 1981 na kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCE) mnamo 1983. Ni wakati akiwa mwanafunzi wa Menengai High ambapo aligundua kipaji chake katika sanaa za kuchora, kuigiza na kukariri mashairi jukwaani.

Anakiri kwamba waliomchochea na kumshajiisha pakubwa kujitosa katika ulingo wa sanaa hizo ni waliokuwa washauri na waelekezi wake katika shule ya msingi, hasa marehemu walimu Laleiya na Bi Tado.

Wawili hao walikuwa walimu wake wazuri sana katika masomo ya sanaa, Jiografia na Kiswahili. Mchango wa Wahinya katika shule yake ya upili haukuwa na mfano. Aliamsha ari ya kuthaminiwa pakubwa kwa Kiswahili na kufufua wimbi la wanafunzi wenzake kutaka kujikuza zaidi katika sanaa za kila nui.

Mnamo 1989, alijiunga na Chuo cha Walimu cha Mosoriot kusomea kozi za kiwango cha P1. Akiwa huko, alianza kujihusisha na shughuli za kutunga mashairi ya aina mbalimbali huku akipania pia kukomaza kabisa kipaji chake katika sanaa ya uchoraji.

Alihitimu mnamo 1991 na baadaye kujiunga na Chuo cha Walimu cha Kagumo, Kaunti ya Nyeri kuendeleza masomo yake, hasa akilenga kukizamia zaidi Kiswahili.

Anaungama kuwa Kiswahili kimemfungulia uwanja mpana, mwafaka na maridhawa zaidi wa kutangamana na weledi wa kila aina katika majukwaa mbalimbali ya kutukuzwa kwa lugha hiyo.

Baada ya kuhitimu mwishoni mwa 1993, Wahinya alijitosa katika uga wa kusaka kazi za kufundisha katika shule mbalimbali za kibinafsi za humu nchini.

Ilikuwa hadi 2010 ambapo msukumo wa kujiendeleza kitaaluma ulimsukuma kujiunga na Chuo Kikuu cha Presbyterian Afrika Mashariki (PUEA).

Akiwa huko, aliendeleza kozi yake ya Ualimu katika Kiswahili na somo la Jiografia hadi mwaka wa 2013 alipofuzu.

Hadi kufikia sasa, amefundisha katika shule anuwai za haiba kubwa ndani na nje ya Kaunti ya Nakuru. Mbali na kujifunza mengi na kunoa vipaji vya wanafunzi wengi katika Kiswahili, Jiografia na fani ya uchoraji, safari ya Wahinya katika juhudi za kufikia mafanikio hayo haijakuwa rahisi.

Nyingi za hatua zake zimekabiliwa na changamoto ambazo zimemweka katika ulazima wa kukumbatia umuhimu wa stahamala na ukakamavu wa hali ya juu.

Wahinya vilevile amewafaa waandishi wabobevu pamoja na wale chipukizi kulenga mbali shabaha zao akisema azma ya mtu haiji kabisa bila ya kushirikisha nia, imani, bidii na ghera.

Mbali na kufaulu pakubwa katika uandaaji wa makala mbalimbali ya kuwasilisha katika makongamano, semina na warsha za kuhimiza uboreshaji wa Kiswahili, Wahinya pia ni gwiji wa kutayarisha tasnifu katika nyanja mbalimbali za kiusomi.

Nyingi za kazi zake zimewahi kutumiwa na idadi kubwa ya watafiti wa mitandaoni, wakiwemo wazawa wa bara Ulaya.

Anasisitiza kwamba baadhi ya kazi zake zimewahi pia kutambuliwa katika Ikulu na makao makuu ya Rais wa Amerika, White House.

 

UALIMU

Kazi ya ualimu ambayo Wahinya anashikilia kwamba ni wito mkubwa kwake, ni jambo aliloanza kulizamia upya kwa mara nyingine muda mrefu baada ya kuhitimu elimu ya Chuo Kikuu. Awali, alikuwa amefundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Mt Kenya Academy kati ya 2005 na 2006.

Akiwa huko, aliacha rekodi ya kuwa mwalimu wa tatu bora zaidi katika uliokuwa Mkoa wa Kati katika somo la Kiswahili. Aliwachochea wanafunzi wake kujizolea alama wastani ya 8.5 katika mtihani wa KCSE Kiswahili mnamo 2006.

Hii inamaanisha kwamba alikuwa mwalimu bora wa Kiswahili katika kiwango cha Manispaa.

Hatimaye, aliyoyomea hadi Elite Schools. Hakuhudumu pale kwa muda mrefu kabla ya maarifa na huduma zake kutwaliwa na Chuo cha Walimu cha Nakuru kilichomwajiri kuwa mwalimu wa somo la Sanaa.

Wahinya anasema kwamba, siku zote alitumia Kiswahili kufundisha sanaa ya uchoraji kwa wanafunzi wa kigeni na wenyeji wazawa wa Afrika Mashariki waliohusudu umilisi wa msamiati na ufasaha wa matamshi yake katika lugha hii ashirafu.

Kwa kipindi cha takriban miaka 11, Wahinya amekuwa akiwanoa walimu watarajiwa katika Chuo cha Walimu cha Nakuru. Ilikuwa hadi 2017 ambapo alianza kusomea Shahada yake ya Umahiri katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya. Aliteua kulizamia somo la Jiografia.

Tangu wakati huo, amehusika pakubwa katika uandishi wa makala mbalimbali ya kitaaluma yanayotumiwa na Taasisi ya Ukuzaji Mitaala nchini Kenya (KICD).

Isitoshe, amekuwa mtahini wa muda mrefu wa Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC) katika somo la Kiswahili na Fasihi.

Tajriba pevu na upana wa uzoefu wake katika uwanja huo umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili, kuwashauri, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.

JIVUNIO

Wahinya anajivunia kufanikisha maandalizi ya makongamano mengi ya Kiswahili ndani na nje ya Nakuru. Fauka ya kuwa miongoni mwa wawasilishaji, waendeshaji na wachangiaji katika makongamano mengi, pia ni mwanachama kindakindaki wa Chama cha Kiswahili cha Nakuru (CHAKINA).

Akiwa mwalimu kipenzi cha wanafunzi wake, anaungama kwamba mtagusano mwema aliouweka awali akiwafundisha darasani unazidi kumfanya akubalike katika tasnia hiyo ya ukufunzi.

Anashikilia kwamba, mengi ya mafanikio yake maishani yametokana na Kiswahili; lugha ambayo imemlea, kumkuza kitaaaluma na kimaadili kiasi cha kumfikisha katika kiwango ambacho ni ndoto ya kila mwanataaluma.

Kati ya watoto wake wote; ni mmoja tu, Erick, ambaye bado ni mwanafunzi katika Shule ya Kitaifa ya Kagumo High, anayeonekana kuzifuata nyayo za baba yake katika suala la uchoraji wa vibonzo na michoro mingineyo.

Wahinya anatambua upekee wa mchango wa mkewe, Bi Beatrice katika kumhimiza pakubwa kukichangamkia Kiswahili alaa kulihali. Beatrice ni mwalimu wa Kiswahili katika Kaunti ya Nyeri.